Skip to main content

Salaam kutoka Matema Beach, Ziwa Nyasa, TanzaniaSalaam kutoka Matema Beach, Ziwa Nyasa, Tanzania
Utangulizi

Mwezi Agosti 2017 nilipata nafasi ya kusafiri kwenda Jamhuri ya Visiwa vya Comoro. Comoro ni umoja wa visiwa vinne; Ngazija, Nzuwani, Mwali, na Maore. Hata hivyo kisiwa cha Maore au Mayotte kinasimamiwa na Ufaransa mpaka hapo wananchi wa Maore watakapoamua kuungana na visiwa vingine. Comoro inaendelea kukitambua kisiwa cha Maore kama sehemu ya Umoja wake. Mimi na familia yangu tulizuru visiwa viwili kati ya hivyo vinne, Ngazija na Nzuwani.

Nikiwa Comoro niliandika waraka niliouita “Salaam kutoka Comoro” na kuusambaza katika mtandao. Watu wengi wamepata nafasi ya kusoma waraka huo. Baadhi yao, pamoja na kunipongeza walinishauri, na hakika walinipa changamoto kuhusu umuhimu wa kuandika waraka kama huo lakini ukilenga kuitangaza Tanzania, kwa watanzania na wageni. Unaanzia wapi kuandika kuhusu Tanzania, nchi iliyojaaliwa na Mwenyezi Mungu kuwa na rasilimali asilia zisizo na mfano duniani? Aidha watu wengi wameandika kuhusu utajiri wa Tanzania, hasa kuhusu vivutio asilia. Tukiri kwamba mengi yaliyoandikwa yameandikwa na wageni. Changamoto tuliyonayo kama watanzania ni kuandika kuhusu Tanzania na kwa mtazamo wetu na katika mazingira yetu.

Unaanzia wapi kuandika kuhusu Tanzania kama sio pale ulipo, unapoishi, kuhusu majirani zako, mazingira na mandhari inayokuzunguka? Nimeona vema nikaikabili changamoto niliyopewa na baadhi ya wasomaji wa makala iliyohusu Comoro. Baada ya kustaafu, muda mwingi niko kijijini Lufilyo na kijijini Matema, kwenye ufukwe wa Ziwa Nyasa. Hapo baadaye, nikijaaliwa, nitaandika kutoka Lufilyo. Kwa sasa nawasalimu kutoka ufukweni, Matema, Ziwa Nyasa, Tanzania.


Ufukwe wa Matema

Ufukwe wa Matema, maarufu kama Matema Beach, ni moja kati ya fukwe za Ziwa Nyasa. Ni fukwe yenye madhari inayopendeza zaidi na mvuto wa kipekee kuliko fukwe nyingi nilizowahi kutembelea. Mandhari yake inafanana kidogo na ufukwe wa Bahari ya Pasifiki katika mji wa Santa Barbara, California, Marekani. Nilialikwa kwenda huko kutoa mhadhara katika Chuo Kikuu cha California, Santa Barbara, Novemba 2008. Mandhari zinafanana kwa kuwa milima mirefu inapakana na maji na hivyo kuleta mwonekano wa kipekee. Ufukwe wa Matema unafanana pia na ufukwe maarufu wa Copacabana, Rio de Janeiro, Brazil. Tofauti na Matema, Copacabana ina urefu wa km 4 tu ambapo Ufukwe wa Matema, ni sehemu tu ya ufukwe wenye urefu wa zaidi ya km 20. Ufukwe wa Matema unaendelea kuwa ufukwe wa Lusungo ambao unaendelea kuwa ufukwe wa Mwaya. Tofauti nyingine ni kwamba ufukwe wa Matema una mchanga asilia, ambapo mchanga wa Copacabana huletwa kutoka sehemu nyingine za pwani ya Brazil, ili kuhakikisha ufukwe unakuwepo wakati wote.

Sehemu ya mashariki ya Ufukwe wa Matema (Matema Beach) ikipakana na safu za Milima ya LivingstoneUfukwe wa Matema unaanzia Lyulilo, soko maarufu la vyungu, kuelekea kaskazini magharibi na magharibi kufuata mwambao wa Ziwa Nyasa. Hivyo basi Lyulilo iko kaskazini mashariki, katika ghuba ndogo ikiashiria mwisho wa Ziwa Nyasa upande wa mashariki. Eneo lenye umbali wa km 5 limeendelezwa kiasi, ingawa bado kuna maeneo machache ambayo hayajaendelezwa. Lyulilo ni kitongoji kilicho katika kijiji cha Ikombe. Kitongoji hicho kinapakana na kitongoji cha Ibungu ambacho kiko katika Kata ya Matema, na mwisho wake ni Mto Mwalalo. Kitongoji cha Itukisyo kinaanzia Mto Mwalalo mpaka kwa Boite.

Ufukwe wa Matema upande wa magharibi wakati wa machweo


Kitongoji cha Ntundu Mano kiko katika Kata ya Lusungo. Kinaanzia kwa Boite mpaka Mto Lufilyo ulipokuwa unaingia Ziwa Nyasa kabla mkondo wake haujahamia Mto Mbaka. Boite ni mkaazi maarufu ambaye amehamia Matema kutoka Kata ya Lufilyo, Busokelo, Kata ninakotoka mimi pia. Kitongoji cha Ntundu Mbaka kiko Kata ya Lusungo na kinaanzia ulipokuwa Mto Lufilyo mpaka Mto Mbaka ulipokuwa. Ukivuka Mto Lufilyo unaingia Kitongoji cha Ikubo, Kijiji cha Mwaya, Kata ya Mwaya. Baada ya hapo unaingia Kitongoji cha Ilondo, Kijiji cha Mwaya, Kata ya Mwaya. Ilondo kinapakana na Kitongoji cha Lugombo, Kijiji cha Mwaya, Kata ya Mwaya. Unaendelea kuambaa ufukweni na kuingia Kitongoji cha Ndola, Kijiji cha Mwaya. Baada ya hapo unaingia Lupando, Kitongoji cha Mwaya, Kata ya Mwaya. Kitongoji cha Lupando kinakutana na Kitongoji cha Mbasi, Kijiji cha Mwaya, Kata ya Mwaya. Baada ya hapo unaingia Bandari ya Itungi. Ni ufukwe wenye urefu wa zaidi ya Km 30.

Asilimia 90 ya ufukwe huu ni mchanga tu. Sehemu kubwa ya ufukwe inamilikiwa na ama watanzania walio olewa na wageni, au na taasisi za kidini. Baadhi ya taasisi hizi zimeanzishwa na wageni lakini zimeandikishwa Tanzania. Kwa maana hiyo ardhi inamilikiwa kihalali.

Ghuba ya Lyulilo/Ibungu ina kina kirefu na ufukwe wake ni mchanga na mawe madogo au kokoto ambazo ni ngumu lakini nyororo sana. Zina rangi nyeusi, kijivu na nyeupe au mchanganyiko wa rangi hizi, na ni kivutio cha pekee pia.

Ufukwe wenye mawe ya rangi eneo la Lyulilo


Ni sehemu ambayo meli kubwa hutia nanga katika safari zake kutoka bandari ya Itungi kwenda bandari ndogo za mwambao wa mashariki ya Ziwa Nyasa. Bandari hizo ni Matema (Kyela), Lumbila (Ludewa), Nsisi (Ludewa), Manda (Ludewa), Lituhi (Nyasa), Njambe (Nyasa), Liuli (Nyasa), na Mbamba Bay (Nyasa).

Alama ya kuongoza Meli kubwa mahali pa kutia nanga


Wageni wasio na uzoefu wa kuogelea ziwani wanashauriwa kuepuka eneo la kina kirefu la ghuba. Tahadhari huwa inatolewa kwa wageni wanaotaka kuogelea karibu ya mito Mbaka na Lufilyo inapoingia Ziwani kutokana na kuwepo kwa viboko na mamba wengi. Vinginevyo maeneo mengine yaliyobaki ni mazuri na salama kuogelea na kupumzika ufukweni. Kutokana na wingi wa aina mbalimbali za samaki wenye rangi, baadhi ya waogeleaji hupenda kuvaa kifaa cha miwani na chombo cha kupumulia ili kuona vizuri samaki wa aina hiyo (snorkelling).
Mito inayoingia Ziwa Nyasa kutoka nyanda za juu kaskazini mwa Ziwa huja na kila aina ya vitu, hasa wakati wa masika ambapo mito hiyo huleta mafuriko katika mabonde ya Tarafa za Unyakyusa na Ntebela. Ni kawaida kuona miti mikubwa, vifaa vya majumbani, migomba, na mifugo iliyokufa ikiingia Ziwani na kuletwa ufukweni na mawimbi ya Ziwa.

Mto Lufilyo unapoingia Ziwa Nyasa ukiwa na magugu maji


Mito hiyo vilevile huja na adui mkbwa wa mazingira ya fukwe za maziwa, magugu maji. Kwa bahati nzuri magugu maji hayo, kama ilivyo vitu mbali mbali vinavyoletwa ziwani na mito kama Mto Lufilyo, huishia ufukweni kutokana na mawimbi ya Ziwa.

Magugu maji na uchafu mwingine ukiletwa ufukweni na mawimbi ya Ziwa


Kama ilivyo fukwe nyingi za maji baridi Afrika, mchanganyiko wa maji, mchanga na jua ni bora kwa matumizi mengine zaidi ya kuogelea, kutembea, kufanya mazoezi na michezo mbalimbali kama vile mpira wa miguu na mpira wa mikono. Matumizi hayo ni pamoja na kufua nguo, kuosha vyombo vya matumizi ya majumbani, na kuanika nafaka kama vile mhogo.


Matumizi ya Ziwa kuosha nguo na vyombo vya nyumbani
Kilimo cha mhogo kimeshamiri katika maeneo ya ufukwe wa Matema


Utayarishaji wa mhogo uliolowekwa tayari kukaushwa kwa jua

Matumizi ya Ufukwe wa Matema kukausha nafaka (mhogo)


Mita 300 kutoka ufukwe wa Matema ni bonde ambalo wakati wa masika huwa eneo tepetepe na ni maarufu kwa kilimo cha mpunga ambao huzalisha mchele maarufu wa Kyela.


Kilimo cha mpunga wa Kyela


Uvuvi na Samaki wa Matema, Ziwa Nyasa
Ziwa Nyasa ni sehemu ya nchi tatu: Malawi, Msumbiji, na Tanzania. Linajulikana kwa majina tofauti katika kila nchi: Ziwa Malawi, Malawi; Ziwa Niassa, Msumbiji; na Ziwa Nyasa, Tanzania. Eneo la Ziwa Nyasa ni kilomita za mraba 29,600. Upana wake mkubwa ni km 75 na kina kirefu zaidi ni mita 700. Ziwa liko mita 468 juu ya usawa wa bahari na urefu wa Ziwa ni kilomita 580. Ziwa liko katika Bonde Kuu la Ufa la Mashariki ya Afrika, ambalo ni muungano wa tawi la mashariki na magharibi la mfumo wa bonde la ufa la mashariki ya Afrika. Kama yalivyo maziwa yaliyo katika Bonde la Ufa, mito mingi huingia Ziwani (Ruhuhu, Lufilyo, Mbaka, Kiwira, na Songwe kwa upande wa Tanzania), na ni mto mmoja tu unaotoka Ziwani, Mto Shire.
Ziwa Nyasa lina aina 1000 ya samaki, takwimu ambayo inalifanya Ziwa hili kuwa na aina nyingi ya samaki kuliko maziwa mengine duniani kote. Kati ya samaki hao, aina 600 hawapatikani kokote isipokuwa Ziwa Nyasa tu. Samaki wanaopatikana kwa wingi, ingawa kwa misimu tofauti ni wafuatao: Mbasa (Opsaridium microlepis), ambaye ni samaki maarufu sana kwa ladha yake na wingi wa mifupa na mafuta.


Samaki aina ya Mbasa


Wenyeji wakimpika au kumkaanga Mbasa hutapata shida kumla kwani huwezi ukatofautisha nyama na mifupa; Mbelele, anafanana na Mbasa kwa ladha na wingi wa miiba midogo midogo; Mbagale, naye ni samaki mwenye ladha nzuri. Ana mafuta kiasi lakini mifupa ni michache zaidi ukilinganisha na Mbasa na Mbelele. Ana nyongo kali ambayo inahitaji uzoefu kuitoa. Vinginevyo samaki huharibika; Kambale, anapatikana katika mito inayoingia ziwani, katika mabwawa (matubwi) na katika maeneo ya ardhi tepetepe. Kambale hujulikana kwa majina mengine kama Somba, Makilu au Ngika; Ngosyola ni aina ya kambale ambao wanapatikana Ziwani. Aina nyingine ya samaki ni Ningu. Ni samaki anayepatikana kwenye mito inayoingia ziwani. Hujificha kwenye mapango madogo chini ya maji ambako pia ni mazalia yake. Ana miba mingi na kichwa chake kina ladha nzuri sana. Magege, au Chambo ni jamii ya Sato. Anajulikana kwa jina la kitaalam Oreochromis (Nyasalapia) lidole. Hapatikani kokote isipokuwa Ziwa Nyasa na Maziwa ya kreta za volcano ya Kingili na Kyungululu; Mantula au Njulila ni aina nyingine ya samaki ambao wana umbo dogo na hawazidi urefu wa nchi sita wakiwa wakubwa.


Samaki aina ya Mantula


Ngolokolo au Nkholokolo (Synodontis njassae) kama wanavyojulikana huko Malawi, anafanana na Ngosyolo (kambale wa ziwani). Ana miba mitatu nje ambayo ina sumu kali. Samaki anayejulikana kama kama Ngunga, au Mkunga, ni mrefu na mwembamba mithili ya nyoka. Ana mfupa mmoja tu mgongoni na hutengenezwa baada ya kukatwa kichwa na mkia. Samaki mwingine wa aina hii anajulikana kama Mbande. Ana mdomo mrefu na mazalia yake ni katika mito inayoingia ziwani. Mbuwe au Songole, ni jamii ya Mbande.


Samaki aina ya Usipa


Samaki wadogo, maarufu kama Usipa, Kapenta au Dagaa (Usipa waliokaushwa) wanapatikana kwa wingi pia katika Ziwa Nyasa.

Usipa waliokaushwa ambao ni Dagaa wa Ziwa Nyasa


Magugu ni samaki wa aina nyingine anayepatikana Ziwa Nyasa. Ni samaki weupe (wa kike) na samawati (wa kiume) anapatikana kandokando ya Ziwa, kwenye mawe mengi. Mbufu naye ni aina ya samaki ambaye anapatikana pia katika Ziwa Nyasa, na hujulikana kwa jina lingine kama Kitoga. Huishi katika kina kirefu, chini kabisa ya maji kwenye matope. Samaki mwingine ni Nchochoma au Njelwa. Huishi kwenye kina cha kati. Samaki mwingine anaitwa Lyapwa. Ni mwembamba na mrefu wa wastani wa mita tatu. Ni jamii ya Mbande. Samaki mwingine ni Mwalukolombe. Ana umbo kama Mantula na anakula macho ya samaki wakubwa. Itukulisi ni samaki mwenye mabaka meusi na huwa kwenye kina kifupi. Ni maarufu kwa kukwepa nyavu. Kaa hupatikana kwa wingi Ziwa Nyasa. Hawaliwi na wenyeji. Ni waharibifu wa nyavu.

Majina ya samaki hawa nimeyapata kutoka kwa jirani yangu Mzee Abudile John Mwangalaba, mkaazi wa miaka mingi wa Matema na mvuvi maarufu, ambaye asili yake ni Kijiji cha Mbongo, Manda, Ludewa; Binti yake Elizabeth Nyamwiga Ngalaba (45); Joseph Ben Alfred Ndomba (aka Mkapa)(22), na Cynthia Hilda Ngoye, wa Kiwira, Rungwe, na Makonde, Ludewa.

Uvuvi katika Ziwa Nyasa bado ni wa kijima zaidi kuliko kibiashara, pamoja na kwamba samaki wa Ziwa Nyasa wana soko kubwa. Wavuvi hutumia mitumbwi midogo inayoendeshwa kwa makasia kutumia nguvu za misuli. Wanatumia nyavu ambazo huelea ndani ya maji baada ya kuwekewa nanga na chambo. Samaki wakubwa huvuliwa mchana kwa kutumia dagaa kama chambo.

Taa zinazotumika katika uvuvi wa Usipa ziwani usiku


Wavuvi huenda majini alfajiri na hurudi alasiri. Uvuvi wa usiku unahusika na kuvua Dagaa na Mantula. Wavuvi hutumia chupa kubwa za maji zilizotumika zilizounganishwa pamoja zikikielea kama boya na kushikilia jiwe kubwa kama nanga. Uvuvi wa usiku unahusisha taa. Kwani samaki huvutwa na mwanga wa taa hizo. Taa hizo huwashwa kutumia betri zilizo kwenye mtumbwi. Betri hizo hupata nguvu zake kutumia mionzi ya jua wakati wa mchana (solar panels).

Solar kwa ajili ya kuoneza nguvu za betri za taa za uvuvi wa usipa usiku


Kuna aina zifuatazo za nyavu: milimita 10 (Usipa); inchi moja; inchi moja na nusu; inchi moja na robo tatu (Mantula, Utapi); inchi mbili na inchi mbili na nusu (Mbelele wadogo); inchi tatu (Mbelele, Magege, Kambale mdogo); nne, tano mpaka sita (Mbasa, Kambale, Nchochoma, Mbagale, Kitoga). Makolokolo ni aina ya utumiaji wa nyavu uliopigwa marufuku. Ni nyavu za inchi moja au inchi moja na nusu ambazo hutegwa ili kuvuna samaki wa kila aina ya ukubwa ikiwa ni pamoja na mazalia ya samaki.


Mzee Abudile akitengeneza nyavu kwa matayarisho ya uvuvi.


Mitumbwi au ngalawa hutengenezwa chini ya miti maeneo ya ufukweni au kwenye makaazi ya watu. Miti inayotumika kuchonga mitumbwi ni pamoja na Samundelele (Cedrella Mexicana), ambao una mbao ngumu na mtumbwi wake unaweza kuishi miaka mitano mpaka nane; mwembe wa asili (Mangifera indica), ambao mtumbwi wake huishi miaka mitatu kwa wastani; Mlaina (Gmelina arborea), na Mzeituni, Ndilolo (Trichillia emetica) na Mlingoti (Eucalyptus grandis) mtumbwi wake huweza kutumika miaka minne.


Uchongaji wa mitumbwi hufanyika karibu na ufukwe


Wavuvi waliozungumzia suala la huduma za ugani na mafunzo ya uvuvi bora wanadhibitisha kutokuwepo kwa huduma za aina hiyo. Wanasema huwa wanaambiwa kama wanataka mafunzo inabidi waende Kyela. Hivyo basi wao hutumia uzoefu wa asilia waliorithishwa na wazazi wao. Wamekiri kukutana na baadhi ya maafisa wa uvuvi, lakini ni katika mazingira ya wataalamu hao kukagua leseni za uvuvi. Wavuvi wanashangaa kuhusu kutakiwa kuwa na leseni. Kwani kwao uvuvi ni kama kilimo. Maafisa hao wakiwakuta wavuvi na samaki katika mitumbwi na kama hawana leseni, basi huondoka na samaki hao na kusema, “mmetuvulia mboga”.

Tabia hiyo inaendelezwa na Maafisa uvuvi wanapokagua nyavu. Kwa mujibu wa wavuvi hata kama nyavu zinazotumika ni halali, hunyag√°nywa na nyavu hizo huuzwa sehemu nyingine bila kutolewa risiti za mauzo.


Wavuvi wakitengeneza nyavu


Uvuvi wa kisasa na wa kibiashara ni pale mitumbwi ya kisasa au meli ndogo za uvuvi zinazoweza kwenda mbali, zinapotumika. Wavuvi wadogo inabidi waungane katika vikundi ili waweze kukopeshwa na vyombo vya fedha ili wanunue vifaa vya uvuvi vya kisasa. Ni muhimu pia idara ya Uvuvi ikawa na mitumbwi ya kisasa ili kutoa huduma za ugani na mafunzo ya uvuvi endelevu.


Ngunga (Lake Nyasa flies)

Ukikaa ufukweni Matema wakati Ziwa Nyasa likiwa limetulia, kwenye upeo, kwa mbali kabisa unaweza kuona umbile kama vile moshi unaobaki nyuma kama meli imepita. Mara ya kwanza nilibishana na wenyeji wangu nikiwaambia meli ya MV Songea ilikuwa ikipita kwa mbali kutoka bandari ndogo zilizo mwambao wa Ziwa. Wenyeji wakanicheka kama vile sijui kitu. Na hakika sikuwa najua. Kwani ule ulikuwa sio moshi bali makundi makubwa ya wadudu wenye umbo la mbu ambao huletwa mwambao na upepo mkali unaotoka ziwani. Ngunga (Chaoburus edulis) utokana na mabuu (larvae) ambao huzaliana juu ya maji. Baada ya kukua hubadilika kuwa kama mbu au inzi wazima na huelea katika makundi makubwa ambayo huonekana kwa mbali kama moshi.


Ngunga


Mabuu ni chakula cha muhimu cha samaki na Ngunga wenyewe ni chakula cha ndege na binadamu. Makundi ya ngunga yanapofika ufukweni wenyeji hujitokeza na ndoo na vikapu ili kuwakusanya.


Ngunga walioletwa pwani na upepo kutoka Ziwa Nyasa


Kwa taarifa za wenyeji wa hapa, baada ya kuwatengeneza kama keki, Ngunga huwa chakula kutamu sana na chanzo muhimu cha protini kwa ajili ya mwili.


Chakula kinachotengenezwa kutokana na Ngunga


Wenyeji huku hawakosi maelezo kuhusu asili ya Ngunga. Ukiongea na baadhi yao watakwambia Ngunga wanatoka kwenye miamba iliyo chini ya Ziwa. Wakifika ufukweni, baada ya siku moja hurudi majini na hukua na kuwa samaki wadogo, dagaa au usipa, kama dagaa wanavyojulikana huku. Wengine watakwambia Ngunga wanatokana na Nyifwila anapofuka moshi.

Nyifwila

Nyifwila ni tafsiri ya kinyakyusa ya neno la kiingereza dragon, ambalo kwa mujibu wa Kamusi ya Ufafiti wa Kiswahili ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (TUKI) lina maana zimwi, au myama mtambaachi mkubwa mwenye mbawa na kucha, na daima hupumua moto. Ni myama wa kutisha mithili ya joka kubwa sana, lenye vichwa vingi, na ambaye anaishi katika fikra tu akiwa ni kielelezo cha nguvu na uwezo mkubwa. Mataifa mengi ya Asia ya Mashariki yanatumia zimwi hili kama alama ya kidini na kitaifa. Wachina wameupa mwaka mmoja kati ya mzunguko wa miaka 12, wa miaka ya wanyama 12, kuwa ni mwaka wa dragoni. Kwa jamii ya kichina, watoto wengi zaidi huzaliwa mwaka wa dragoni kwa sababu ya imani kwamba watoto hao huwa na bahati katika maisha. Kwa kalenda ya wachina, mwaka wa 2012 ulikuwa ni mwaka wa dragoni na utafuatiwa na mwaka 2024.

Jamii nyingi zina hadithi au simulizi (anecdotes) zinazorithishwa kizazi hadi kizazi kuhusu uwepo wa matukio ya ajabu yanayohusisha matukio yanayotokana na nguvu za ajabu za mazimwi ya kila aina (mythical). Wengi wetu tuliopata nafasi ya kupata elimu Uingereza, au wale ambao wamesoma kuhusu mila na desturi za waingereza hatuwezi kusahau simulizi za mara kwa mara za kuonekana au kutoonekana kwa Zimwi la Loch-ness (Loch-ness monster), zimwi ambalo inadaiwa ni zimwi la bahari linaloishi katika ziwa linalotokana na sehemu ndogo ya bahari kuzungukwa na ardhi. Loch maana yake ziwa kiskoti na kiirish. Zimwi liliotajwa awali linasimuliwa kuishi katika Ziwa Ness huko Uskoti, Uingereza ya kaskazini.

Kwa maelezo ya jirani yangu, Mzee Abudile (85), Nyifwila anaishi chini kabisa ya Ziwa Nyasa. Haonekani na binadamu isipokuwa kwa miujiza. Ni zimwi kubwa lenye vichwa takriban kumi na mbili. Nyifwila ana macho mengi kama nyota. Huko aliko akichukia basi Ziwa Nyasa linachafuka. Akilala, Ziwa linatulia. Akitoka huko aliko na kuja mwambao basi huacha mawimbi makali na dhoruba ziwani na pwani. Mara chache anapofanya hivyo huelekea milimani, milima ya Livingstone. Tunajua alikuwa huko pale anaporudi ziwani. Kwani huacha mawe yakiporomoka kutoka mlimani, na njia anayochukua hufuatiwa na mto. Anapopita huacha mafuta yanayowaka moto. Ukikanyaga mafuta hayo utadhurika.

Ni wazee wa kimila tu wanaoruhusiwa kuchukua mafuta yaliyo katika mapito ya Nyifwila kwa ajili ya shughuli zao za kijadi kama vile kutengenea dawa au kufanyia matambiko. Kama ilivyo kwa Zimwi la Loch-ness hakuna anayeweza kuthibitisha kuiona Nyifwila. Kama ilivyo kwa “binamu’’ ya Nyifwila aliyeko Uskoti, watu hushindana kuangalia Ziwa kuona kama anaweza kuonekana. Mzee Abudile anaapa yeye amewahi kusindikizwa na Nyifwila usiku wa manane akitokea Malawi kuvuka Mto Songwe mpaka karibu na Itungi akirejea Matema. Ndugu zake hawaamini hadithi yake. Kwani wanasema kwa kuwa karibu tu na Nyifwila, leo Mzee Abudile angekuwa ametangulia mbele za haki. Loch-ness ni kivutio kikubwa, kila mtalii akijaribu kuingia katika rekodi ya kuliona Zimwi. Ni zoezi linaloendelea kwa zaidi ya miaka 1500 mpaka sasa na utalii huo huiingizia Halmashauri ya eneo hilo wastani wa shilingi bilioni 90 kwa mwaka.


Pango la Matambiko la Pali-Kyala

Mila na desturi za jamii nyingi duniani kote zinahusu uwepo wa maeneo ambayo hutumika na kulindwa kijadi kwa ajili ya matambiko. Kwa jamii za kiafrika kusini mwa jangwa la Sahara, utamaduni huo unahusu kutoa matambiko kushukuru kwa kile jamii imetendewa na asili, maombi ya jamii kwa miungu wao kwa ajili ya mvua ili kuondokana na ukame, jamii kuepushwa na na majanga asilia ikiwa ni pamoja na magonjwa, na mambo mengine ambayo mtu mmoja mmoja, familia au ukoo wanashauriwa kutoa sadaka kwa sababu mbalimbali ambazo wanashauriwa na uongozi wa jadi.

Pango la Pali-Kyala, au kwa ufupi Likyala kama linavyojulikana na wenyeji wa huku, liko umbali wa km 2 hivi kusini mwa kitongoji cha Lyulilo mwambao wa Ziwa Nyasa kuelekea kitongoji cha Ikombe. Pango la Likyala liko katika kitongoji cha Lyulilo, ambacho kiko katika kijiji cha Ikombe. Safu za Milima ya Livingstone zinaingia Ziwa Nyasa kuanzia Lyulilo na inaambaa kusini mpaka Manda na Mbamba Bay. Unaweza kufika pango la Likyala ama kwa kutembea kuambaa ufukweni kutoka Lyulilo au kwa mtumbwi kutoka mwalo wa Matema. Ni mwendo wa dakika 15 kwa mtumbwi unaotumia mota.


Pango la Pali-Kyala


Umaarufu wa pango la Likyala unatokana na kwamba ni mahala pa matambiko ya kijadi. Linalindwa na wazee maalum wa kimila wanaotoka Ikombe. Kihistoria ni mahala ambapo wazee walifanya matambiko ya kuombea mvua. Akisimulia umaarufu wa eneo hilo, Joseph (43) anaeleza kwamba wazee wa kimila walipokuja kufanya matambiko ya mvua, mara tu baada ya wao kumaliza matambiko, mvua zilinyesha. Kwa maelezo ya Joseph na Charity (25) kuna maajabu ya kila aina hapo. Wakati mwingine unaweza ukakuta kuku wakizunguka zunguka maeneo hayo ingawa ni mbali sana kutoka kwenye makaazi ya watu. Anasisitiza Charity Ngalawa, ambaye ni nahodha wa boti iliyotupeleka, na mwenyeji wa Matema mwenye asili ya Manda, “ukimtamani kuku unayempata hapa na ukamchukua, ukamchinja na kumla, utadhulika. Unaweza kupooza mwili au ukapata kichaa, na unaweza ukafa. Lazima watu watakaojua suala hilo mapema waharakishe kuwaona wazee wa kimila ili waweze kukuokoa”. Inasemeka pango hilo ni refu na linafika mpaka Ukinga, Makete. Lakini kwa mujibu wa Joseph, ambaye amewahi kuingia kwenye pango hilo, pango ni kumbwa mwanzoni lakini upenyo unakuwa mdogo baada ya mita zipatazo hamsini hivi.

Katika kumbukumbu zao kama zilivyokaririwa katika historia fupi ya kanisa la Kiinjili la Kiluteri Tanzania, Daosisi ya Konde 1891-1991, iliyohaririwa na mwaka 1991, Mwalimu Andalalisye Mwaihabi na wenzake wanaeleza jinsi ambavyo wamisionari wa kwanza walivyopata shida kupenyeza injili kwa sababu ya dini za kiasili ambazo zilikuwa zimejengeka katika jamii za wenyeji wa maeno haya. Pango la Pali-Kyala limeelezwa kama ni mahali ambapo Wakisi wa Ikombe walikuwa wakiabudu Mungu wao. 


Ufukwe wa mawe, Pali-Kyala, wanapopatikana samaki wa rangi


Umaarufu wa eneo hilo la pango unatokana pia na kuwepo kwa samaki wa mapambo katika kina kifupi cha Ziwa. Hawa ni samaki wa rangi za aina mbalimbali ikiwa ni pamoja na; pundamilia, weusi, bluu, weusi na manjano. Hata bila ya uwa na mawani ya kuogelea majini, samaki hao wanaonekana. Wageni wengi hufika eneo hilo li kuvua samaki wa mapambo. Wao na wavuvi wenyeji huwavua samaki hao bila udhibiti wowote na kuashiria kupungua kwa samaki wa aina hiyo. Ziwa Nyasa ni maarufu sana kwa samaki hao wenye rangi za kila aina na zinazovutia. Kama ilivyoelezwa awali, inakadiriwa kuwa kuna aina 700 mpaka 1000 ya samaki wa aina ya cichlids katika Ziwa, wengi wao hawapatikani duniani kote isipokuwa Ziwa Nyasa tu (endemic). Katika eneo la Matema samaki wa mapambo wanapatikana kwa wingi maeneo ya Likyala; kwa Katulemi, karibu na Lyulilo; na Isumba, kusini karibu na Ikombe. Wageni wengi huwatafuta samaki hao kwa ajili ya matankimaji yaliyotengenezwa kwa vioo kwa ajili ya maonesho (aquarium).


Maporomoko ya Maji ya Mwalalo (Mwalalo Waterfalls)
Baada ya kukaa kwa muda Matema kama mwanakijiji, nilipata kufahamu kwamba moja ya vivitio vya Matema ni maporomoko ya maji yaliyo katika Mto Mwalalo. Mwalalo ni moja ya mito inayoingiza maji katika Ziwa Nyasa karibu na Kitongoji maarufu cha Lyulilo.


Mandhari ya Korongo la Mto Mwalalo


Kuipata njia ya kuanza safari ya kwenda kwenye maporomoko ilitubidi, mimi na walioniongoza kwenda huko, Joseph Sinyangwe (43) na Mario Mwaitulo (25), twende kwa gari mpaka lilpo tanki la maji la kijiji cha Matema, lililo km 4 kutoka ufukwe wa Matema katika kitongoji cha Bulinda. Ndipo safari inapoanza kupanda kupita kandokando ya Mto Mwalalo unaopita katika korongo kubwa katikati ya milima miwili. Kabla ya kuanza safari niliwauliza wenzangu ingechukua muda gani kufika kwenye maporomoko? “Sisi kawaida huchukua dakika 55. Tukiwa na wewe inaweza ikachukua saa moja na nusu tu.” Nikawaelewa. Walikuwa na maana utokana na umri wangu tungeenda polepole. Hawakunikatisha tamaa. Pamoja na kwamba waelekezi wangu hao walinitahadharisha ugumu wa safari, nilipigamoyo konde na kuwakumbusha kwamba umri ni namba tu!


Maporomoko ya Mto Mwalalo


Unaanza kuona ugumu wa safari mapema sana. Kwani ukiangalia huku na huko kingo zote mbili za mto ni miamba ya mawe iliyo wima. Kilichobaki ni kutafuta upenyo mahali unapoweza kuweka mguu huku ukishikilia mwamba ili usidondoke lakini upige hatua mbele. Sehemu nyingine hakuna nafasi ya namna hiyo hivyo inabidi kupita kwenye maji ndani ya mto. Kwa kuwa ilikuwa wakati wa kiangazi, kina cha maji kilikuwa kimepungua. Sehemu nyingine maji yanafika katika magoti na sehemu nyingine kina ni kirefu na maji yanafika kifuani. Aina ya nguo na viatu kwa safari ya namna hiyo ni muhimu. Nguo na viatu vya mazoezi vinafaa kwa matembezi ya aina hiyo.

Njiani tunapata mambo mengi ya kujifunza kuhusu bonde hilo la Mto Mwalalo. Tunakutana na watu waliobeba mbao kichwani wakitokea huko tunakokwenda. Nashawishika kuongea na mmoja wao kuhusu mazingira ya bonde hilo. Aggrey Elias Mwakilasa (35) ni mwenyeji wa Matema. Alizaliwa Shinyanga. Baba yake, Elias Mwakilasa alikuwa askari polisi kituo cha Mgodi wa Mwadui. Mambo mawili yananijia kichwani. Hakika Tanzania ni nchi moja na yenye umoja. Kwani kukutana na mzaliwa wa Shinyanga katika mazingira ya Mto Mwalalo ni jambo ambalo lisingeweza kutegemewa katika nchi nyingine. Jambo la pili lililonijia kichwani ni uhusiano wangu na Mgodi wa Almasi wa Mwadui. Kwani kwa miaka mitatu, 1990 mpaka 1993 nilikuwa Mwenyekiti wa Kampuni ya Willliamson ya Almasi iliyokuwa inamiliki mgodi wa almasi wa Mwadui, wakati huo ukiwa unamilikiwa nusu kwa nusu kati ya Kampuni ya De Beers ya Afrika ya Kusini na Serikali ya Tanzania. Kwa kuwa Serikali ya Tanzania iliiwekea Afrika ya Kusini vikwazo vya kibiashara, hatukuwa na uhusiano wa moja kwa moja na De Beers, bali kupitia kampuni yake tanzu iliyojulikana kwa jina la Wilcroft Company Ltd iliyosajiliwa Bermuda. Ilibidi tuwe na mfumo huo kwani wakati ule, mpaka sasa, biashara ya almasi duniani, ingawa huendeshwa katika soko huria, inahodhiwa kwa kiwango kikubwa na De Beers, na sasa Petra, yenye asili ya Afrika ya Kusini.


Sehemu ya Mto Mwalalo


Inawezekana Elias Mwakilasa, baba yake Aggrey, alikuwa Mwadui wakati nikiwa Mwenyekiti wa Mgodi huo wa almasi. Kuhusu aina ya mbao alizokuwa amebeba, Aggrey anaeleza kuwa mbao nyingi zinazopatikana huko zinatokana na mti aina ya “Mgwina’’ (Filcahoa lauriforia), ambao hutoa mbao ngumu kama Mninga. Kwa maelezo ya Aggrey, Mgwina hutoa mbao nyingi zaidi ya Mninga kwani ugumu wa Mninga kwenye kiini ambapo mbao za Mgwina ni ngumu sehemu zote. Miti mingi iko juu zaidi ya maporomoko ya Mwalalo kuelekea kijiji cha Usililo kilicho Wilaya ya Makete. Hakubali kwamba ukataji miti utaathiri chanzo cha Mto Mwalalo kwani kwa imani yake msitu ni mkubwa!


Mti aina ya Mgwina


Kuna maeneo kumi ambayo ni hatari au magumu kupita. Lakini mnapomaliza kupita eneo moja waelekezi wanakwambia, “Mzee, yamebakia maeneo mawili au matatu hivi”. Elimu haitolewi darasani tu. Kwani walikuwa wakisema hivyo kutumia saikolijia ya uzoefu tu ili kutomkatisha tamaa Mzee.

Kama ilivyoelezwa katika moja ya aya zilizotangulia, kingo za Mto Mwalalo ni milima mirefu pande zote mbili. Kuna eneo sehemu moja katika mlima ulio ukingo wa kusini ambalo waelekezi wangu waliona vema nilione. Ni eneo lenye msitu. Hapo ndipo wananchi walipowakurupusha wahamiaji haramu kutoka Ethiopia na Somalia wapatao 20 au 30. Walipogundua wamezingirwa upande wa mto, kwa maelezo ya Joseph, walikimbia upande wa mlima kwa kasi kama vile walikuwa wanyama wa porini. Walitokomea upande wa Makete bila kupatikana. Nilipodadisi zaidi kuhusu tukio hilo, nikaambiwa Matema Beach ilikuwa ni kituo cha kupitishia wahamiaji hao haramu. Meli ndogo zilikuwa zinakuja na mapipa tupu kwa kisingizio cha kununua mafuta ya diseli. Wahusika na biashara hiyo ya kuvusha wahamiaji kutoka Ethiopia na Somalia hupakia mapipa na hungoja mpaka jioni. Giza likiingia basi abiria wao hupandishwa kwenye meli na meli hizo zisizojulikana huelekea mahali kusikojulikana.

Kwa wahamiaji haramu kutoka Uhabeshi na Somalia, kupita Kenya au Uganda, kuvuka mpaka na kuingia Tanzania, kusafiri kutoka kaskazini mpaka kujificha katika msitu ulio ndani ya Mto Mwalalo, ufanikishaji wake lazima utokane na mtandao mpana na wa kisasa (sophisticated). Tukio hili linadhihirisha umuhimu wa ulinzi na usalama katika maeneo yenye fukwe na yaliyo mpakani kama ilivyo Matema. Pamoja na kuwa mlinzi wa nchi ni mwanachi mwenyewe, kwa maeneo kama haya yaliyo mstari wa mbele, mafunzo maalum na ya kitaalam ya usalama yanahitajika kwa raia na vikundi maalum kuweza kutambua aina ya wageni, shughuli zao, mahala wanapotoka, na mwenendo wao, bila kuathiri utalii.


Matembezi katika Bonde la Mto Mwalalo


Tulianza matembezi hayo saa 5.15 asubuhi. Ilipofika saa 8 mchana bado zilibaki sehemu “tatu au nne’’, zambazo ni ngumu kupita kabla ya kuyafikia maporomoko. Hatimaye tuliweza kuyafikia saa 9.30 mchana. Kama msomaji atakavyoona kwenye picha, mandhari ya bonde la Mto Mwalalo inapendeza sana, kutokana na uwepo wa maji, mawe ya kila aina yenye ukubwa wa kila aina, uoto wa asili, misitu, na hatimaye maporomoko yenyewe. Waelekezi wanaeleza kwamba maji tuliyoyaona yalikuwa yamepungua kutokana na majira ya kiangazi. Kwa maelezo yao maporomoko huwa na maji mengi zaidi kipindi cha mvua na hupendeza zaidi majira hayo. Hata hivyo wanasisitiza maji hujaa sana mtoni na hivyo kuyafikia maporomoko kama tulivyoweza huwa ni changamoto kubwa zaidi, lakini ni changamoto ambayo haikosi watu wa kuikabili. Nusu saa ilitutosha kushuhudia maporomoko hayo ambayo hakika ni kivutio kikubwa. Tuliondoka huko saa 10 kamili jioni kuanza safari ya kurudi Matema.

Kama ilivyo dhahiri kwa watu wengi, kupanda mlima ni afadhali zaidi kuliko kushuka. Kama ilivyoelezwa hapo awali, kutokana na kuwepo kwa majabali yaliyo wima, ilibidi tunapopanda tujishikiza kwenye sehemu za mawe ambazo tuliweza kufanya hivyo. Si rahisi hata kidogo kufanya hivyo wakati wa kushuka. Kwani ni lazima uone unakwenda wapi. Staili tuliyotumia ni kukaa, kuvuta mwili polepole hatua kwa hatua na mwishowe kutereza na kuingia kwenye maji na kuendelea na safari kwa jinsi mazingira yalivyoruhusu. Nilikuwa kichekesho kwa Joseph na Mario jinsi nilivyovyokuwa nachukuwa tahadhari kubwa katika kushuka miamba hiyo. Sehemu hizo za safari zilinikumbusha jinsi Mzee Isaac alivyonipa kichapo kila nikirudi nyumbani nikiwa na kaptula zilizotoboka kwenye makalio kutokana na mchezo wa kutereza na wezangu tukiwa kwenye miteremko! Max bila shaka anakumbuka jinsi kaptula zake mpya zilivyokuwa zikichakaa saa mbili tu baada ya kuvaliwa pale Barabara ya Kileleni, Nyumba Namba 25, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Tulifika mahali tulipoanzia matembezi saa 1 kamili usiku, tukiwa hoi, lakini mwandishi wa Makala hii akiwa hoi zaidi. Nakubali umri ni zaidi ya “namba”.

Matembezi haya, pamoja na ugumu wake kwa watu wenye umri kama wangu, ni kivutio kizuri, ni utalii wa ndani ya nchi. Vijana wanaweza kutumia muda mfupi zaidi ya ule tuliotumia. Pamoja na kasi ya mwendo wangu kuwa ndogo, walinivumilia. Ndipo nikakumbuka maneno ya rafiki yangu Linford Mboma, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania, kila tukiwa katika msururu wa magari kikazi akitutahadharisha kwamba “mwendo wa magari yanayosafiri katika msururu, hutawaliwa na gari lenye kasi ndogo”.

Katika matembezi yangu ya kawaida ufukweni nakutana na vijana wawili, Lisa Schnider(28) na Paul Aspreon (31) kutoka Freiburg, Ujerumani. Wamekuja Matema kama watalii. Nikakumbuka safari yangu ya mwaka 1972 kutoka Birmingham, Uingereza, kwenda Freiburg, kupitia Dover na Calais, kwa meli, na Heidelberg, na Munich mpaka Freiburg kwa treni. Ilikuwa wakati wa likizo ndefu ya kipindi cha kiangazi, na nilienda kuitikia mwaliko wa Mchungaji Helge Heisler (Mwenyezi Mungu Airehemu Roho yake), Mjerumani ambaye aliwahi kufanya kazi ya Kanisa Kongwa, Chunya na Rungwe. Hivyo basi ilikuwa bahati kukutana na vijana waliotoka Freiburg. Walinihakikishia ile treni ya zamani sana ya kitalii inayopita katika msitu mkubwa (Black Forest) kusini mwa Freiburg bado inafanya kazi. Moja ya maeneo waliyotembelea baada ya kushauriwa, ni Maporomoko ya Mwalalo.

Wananisimulia kwamba walipita jengo dogo lililokuwa na watu wakati wakieliekea Mto Mwalalo kuanza safari ya kwenda kwenye maporomoko. Baada ya km 1, wakafuatwa na mtu aliyewaambia wamevunja sheria kwa kuanza safari kabla ya kulipa ushuru wa Halmashauri ya Kijiji. Ilibidi warudi kwenye ofisi walizozipita awali na ndipo walipoambiwa walipe faini ya dola za kimarekani 100. Wakalalamika kwamba hakuna aliyewataarifu kuhusu kulipa ushuru. Walishangaa kwanini waliachwa waendelee na safari bila kusimamishwa ili watii sheria. Baada ya kulalamika kwamba wao ni wanafunzi na hivyo dola mia ni fedha nyingi sana kwao, walitozwa faini ya shilingi elfu ishirini na kulipia ushuru na kupewa mwelekezi. Pamoja na kusifia sana mazingira ya Mto Mwalalo, na Maporomoko ya maji ya Mto huo, walionekana kusononeshwa sana na kitendo cha Ofisi ya Mtendaji wa Kata. Ndipo nilipoamsha saikolojia ya ualimu na kuwaambia, “vijana, sikillizeni, haiwezekani safari yenu kutoka huko mbali, bara la ulaya, mpaka mtakaporudi kila kitu kiwe poa tu. Lazima wakati mwingine mpate matatizo ili simulizi zenu kwa wenzenu ziwe na mizania nzuri”.


Mtalii apigwa faini kwa kuelekea Maporomoko ya Mwalalo bila “kibali”.


Mto Mwalalo ni mmoja ya mito inayoingia Ziwa Nyasa. Chanzo chake na bonde lake dogo liko katika safu za milima ya Livingstone. Ni mto mdogo ukilinganisha na mito kama Lufilyo, Mbaka, Kiwira na Songwe. Safu za milima ya Livingstone ni chanzo muhimu cha mito ambayo maji yake hatimaye huingia katika Ziwa Nyasa. Changamoto kubwa kimazingira katika safu za milima hiyo zinahusu: uchomaji moto wakati wa kiangazi; kilimo kandokando ya vyanzo vya maji; ukataji miti katika misitu, na uwindaji haramu. Miteremko ya safu za milima hii ni mirefu na mikali. Miteremko hiyo ni mpaka kati ya mikoa ya Mbeya na Njombe; Wilaya za Mbeya Vijijini, Rungwe na Kyela, kwa Mkoa wa Mbeya; na Makete na Ludewa, Mkoa wa Njombe. Sio rahisi kwa Halmashauri za Wilaya za Mkoa wa Njombe kusimamia maeneo yanayowahusu, na Halmashauri za Wilaya za Mkoa wa Mbeya huona kama vile maeneo hayo hayawahusu. Sehemu ya kaskazini ya milima ya Livingstone iko chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Hifadhi ya Kitulo. Kutokana na umuhimu wa kutunza vyanzo vingi vya maji, na kuhifadhi ardhi na bioanuwai ya safu za milima hii, ni vema eneo lote liwe chini ya usimamizi wa TANAPA, na Halmashauri za Wilaya na Mikoa inayopakana, pamoja na Bodi ya Bonde la Ziwa Nyasa, kuwa na mkakati wa pamoja wa kuiwezesha TANAPA kutekeleza wajibu huo.

Tukio lililowapata vijana wa kijerumani, Lisa na Paul, linaonesha umuhimu wa kuwa na kituo kidogo cha utalii Matema. Hapo patakuwa ni mahali ambapo watalii wa ndani na nje watapata taarifa zote kuhusu vivutio vya utalii vilivyopo, namna ya kuvifikia, tozo mbalimbali, hoteli na nyumba za wageni, na gharama zake, usafiri, ramani, na maelezo mbalimbali yanayoweza kutolewa kuwezesha utalii.


Miamba ya Mto Mwalalo

Mwanamazingira yeyote au mtu mwenye udadisi anayetembelea bonde la Mto Mwalalo kutoka mwanzo mpaka kwenye Maporomoko ya Mwalalo hatakosa kuvutiwa na aina mbalimbali za miamba na mawe yaliyo katika bonde hilo. Picha nilizochukua za mawe na miamba hiyo zilipelekwa kwa majiolojia waandamizi, waliobobea katika fani hii muhimu, na wenye uzoefu wa miaka mingi katika kazi, na kuwaomba maelezo kuhusu miamba ya Mto Mwalalo. Maelezo yafuatayo yametolewa na Ndugu Asa Mwaipopo na Dr. Dalaly Kafumu: “Bonde la Mto Mwalalo, Matema lina mpangilio wa mawe wa upekee fulani na unavutia.


Miamba ya Mto Mwalalo ikionesha mkondo wa mshipa (vein) kwa chini


Kijiolojia, miamba hii inaonesha kuwa na sura (lithology) kubwa mbili, lakini zote zikiwa na chembechembe ndogo ndogo. Moja ni aina ya “granite” ambayo ni aina maarufu ya mawe yanayopatikana upande wa Ziwa Victoria, hasa Mwanza, na ya pili ni “delorite’’ mawe ambayo ni matokeo ya volkano iliyotokea baadaye na ambayo majivu yake yenye joto kali sana (lava) yalijipenyeza (cross cutting veins) kwenye miamba iliyotangulia. Miamba ya Mto Mwalalo inaonesha matukio ya kijiolojia; kuanzia mwagiko la kivolkano la awali na baadaye tetemeko au mmeguko wa ardhi uliopelekea kuwepo kwa nyufa ambazo zilijazwa na lava ya volkano iliyotokea miaka mingi baadaye, na lava ilipopoa ikatengeneza mkondo mithili ya mishipa (veins) katika miamba ya awali. Picha Na… inaonesha miamba aina ya “delorite’’. Picha Na….ni ya miamba aina ya “xenolith’’. Aidha nyufa zilizojitokeza (veins) inaonesha zilizibwa na miamba aina ya “microline’’.


Miamba ya Mto Mwalalo ikionesha ‘’veins’’ za juu


Miamba inayopatikana Mto Mwalalo (granite na dolerite) huwa haina vyanzo vya madini yenye thamani (precious metals) au madini mengine ambayo kiasilia hupatikana kwa wingi na kirahisi ardhini. Hata hivyo kama mwamba una chembechembe ndogo ndogo na ni mkubwa na hauna nyufa nyingi, unaweza kutumika katika uchimbaji wa mawe ya kuchonga (dimensional stones). Mawe hayo (cut and polished stones, slabs) hutumika katika ujenzi.

Miamba ya Mto Mto Mwalalo inaweza kuwa na sifa za kuwa mgodi wa mawe ya kuchonga (dimensional stone) kama ni miamba mikubwa, endelevu na isiyokuwa na nyufa nyingi. Ili mgodi uwezekane, unahitajika utafiti wa kjiolojia na uchorongaji ili kujiridhisha na uwezekano huo. Aidha, kwa kuwa miamba hii ipo katika bonde la Mto, tathmini ya athari kwa mazingira itahitajika”.

Pamoja na yaliyotangulia, eneo hili inabidi lifanyiwe uchunguzi wa kijiolojia, wanafunzi wa jiolojia, jiografia, mazingira, na wengine, wahamasishwe kutembelea eneo hilo, na litangazwe kuvutia watalii.


Lyulilo

Lyulilo ni kitongoji cha kijiji cha Ikombe. Kitongoji hiki kiko kwenye ghuba ndogo inayoashiria mwisho wa Ziwa Nyasa unapoambaa mashariki kutoka kusini kwenda kaskazini. Ghuba hiyo imekaa kimkakati. 


Soko la vyungu Lyulilo


Ufukwe wake ni mchanganyiko wa mchanga na mawe madogo. Ufukwe uko kwenye kina kirefu kiasicha kwamba meli kubwa kama vile MV Songea inayosafirisha abiria na mizigo hutia nanga mita 200 hivi kutoka sokoni Lyulilo.


Soko la Lyulilo


Lyulilo ni soko maarufu kwa samaki wa Ziwa Nyasa na kwa vyungu na bidhaa mbalimbali zinazotengenezwa kwa udongo wa mfinyanzi. Mitumbwi na boti hutia nanga Lyulilo zikisafirisha vyungu kutoka Ikombe na bidhaa kwenda Ikombe.

Umaarufu wa Lyulilo unatokana na kuwa soko la vyungu vya asili vinavyotokana na udongo wa mfinyanzi. Si rahisi hasa kwa vijana wetu waliokulia mjini kufahamu umuhimu wa vyungu hivi. Kwani vijana wa zamani tunakumbuka jinsi mama zetu, shaangazi zetu na bibi wazaa mama au baba jinsi walivyotumia vyungu hivi kupikia na jinsi chakula kilichotoka humo kilivyokuwa na ladha na utamu wa aina yake. Lakini pi tunakumbuka jinsi ambavyo vyungu hivi vilitumika kama jokovu. Kwa kuweka chungu kilichojaa maji juu ya mafiga matatu, na kuweka mchanga chini ya chungu na kunyunyizia maji mchanga huo, maji yaliwea kupoa na kuwa ya baridi kana kwamba yametoka kwenye jokofu.


Aina mbalimbali ya vifaa vinavyotengenezwa na udongo wa mfinyanzi


Mnada wa vyungu hufanyika jumamosi. Hata hivyo mauzo ya samaki, vyungu, mchele, ndizi na bidhaa nyingine hufanyika kila siku.


Mchele maarufu wa Kyela ukiuzwa sokoni Lyulilo


Halmashauri ya Wilaya ya Kyela imejenga soko la samaki kwa matarajio ya ongezeko la biashara. Soko hilo lenye majokofu ya kutunzia samaki halitumiki. Kwani umeme haujafika Lyulilo.


Mauzo ya jumla ya Dagaa katika Soko la Lyulilo


Ikombe

Moja ya vivutio vikubwa kwa wageni na watalii wanaofika matema ni kitongoji cha Ikombe kilicho katika kijiji cha Ikombe katika kata ya Matema. Kitongoji cha Ikombe kiko kando kando ya Ziwa Nyasa kwenye mitelemko ya Milima ya Livingstone. Ni kitongoji cha mwisho kusini mwa Matema kinachopakana na Wilaya ya Ludewa, Mkoa wa Njombe. Ikombe ni peninsula au rasi ndogo inayoingia Ziwa Nyasa. Haifikiki kwa urahisi kwa nchi kavu. Kwani miteremko ya Milima Livingstone ni mikali. Barabara inajengwa. Yanahitajika madaraja kukamilisha ujenzi huo. Hat hivyo baadhi ya watalii hupenda kutembea kwenda Ikombe. Njia rahisi kwa sasa kufika Ikombe ni kutumia boti, safari inayochukua dakika 20. Wenyeji hutumia ngalawa kwa usafiri na kupeleka bidhaa mbalimbali Ikombe.


Safari ya kwenda Ikombe 
                                                                  Matembezi kwenda Shule ya Msingi Ikombe


Ras ya Ikombe ina mvuto wa kipekee. Ufukwe wake ni wa mawe madogo na kawaida. Ufukwe umejaa ngalawa. Kwani Ikombe ni kijiji cha wavuvi na pia usafiri kwenda sehemu nyingne za Kata nikutumia ngalawa. Madhari ya kitongoji inapendeza kutokana na miti mingi ya asili na iliyopandwa inayoipa Ikombe tabiachi ya kipekee. Hapa ndipo vyungu vya asili hutengenezwa na huvushwa kwa mitumbwi kupelekwa Lyulilo kuuzwa. Udongo mfinyanzi unaopatikana Ikombe ndio unaofaa kutengeneza vyungu. Ikombe pana zahanati na shule ya msingi.


Huduma za Kijamii

Afya

Baada ya kuugua kwa muda mrefu na kutibiwa India na hapa nchini kati ya mwaka 2011 na 2013 kila ninapoulizwa kipaumbele cha maendeleo kiwe nini, hasa pale ambapo rasilimali ni kidogo, huwa najibu afya na elimu. Kabla ya hapo jibu langu lilikuwa elimu na elimu tu. Kwa upande wa Matema, suala la afya linaweza kugawanywa katika sehemu mbili; elimu ya usafi wa mazingira, na tiba.

Maeneo ya mwambao wa maziwa na bahari barani Afrika bado yana changamoto kubwa inayohusu usafi wa mazingira, maneno ya kistaarabu yanayomaanisha uwepo au la wa vyoo. Jamii nyingi, vijijini na mijini katika mwambao wa maziwa na bahari hutumia bahari na maziwa kama vyoo vya kudumu. Nilipotembelea Pangani nikiwa Waziri wa Nchi mwenye dhamana ya Mazingira, nilikumbana na changamoto mbili. Kwanza, mji huo wa kihistoria ulikuwa unaharibiwa na mawimbi ya bahari yaliyokuwa yakimeza ufukwe pole pole, na kuharibu nyumba na miundombinu, kutokana, kwa kiwango kikubwa, na mabadiliko ya tabianchi.

Changamoto ya pili ilikuwa ni uhaba wa vyoo. Kwani jamii ilikuwa ikienda ufukweni mwa bahari ili kujisaidia. Ilitupa taabu sana kukagua uharibifu wa pwani ya Pangani. Kwani ilitubidi kukagua eneo lote kwa kutembea ufukweni, na kila mara kuruka kinyesi. Nilipata changamoto ya aina hiyo Mikindani, Lindi. Ukikaa katika hoteli nzuri ya kitalii na ukiwa makini unaweza kugundua kuwa makaazi mengi ya Mikindani hayana vyoo. Wakaazi hutumia Bahari ya Hindi kama eneo la kutimiza wito asilia. Pangani na Mikindani ni miji midogo.

Kuna wakati nilienda Accra, Ghana kuhudhuria mkutano wa kimataifa kuhusu madhara ya mabadiliko ya tabia nchi. Kama ilivyo kawaida yangu, alfajiri huwa natoka hotelini ili kufanya mazoezi ya matembezi. Umbali kidogo kutoka hoteli ya kitalii niliyokaa kuna ufukwe wenye mchanga na mawe. Nililoliona na lililonishangaza ni kwamba jamii kutoka kitongoji cha jirani walishuka ufukweni kila asubuhi kwa kile nilichodhani wanaenda kuoga au kuogelea. Haikuwa hivyo. Walikuwa wamekaa tu. Nilipouliza nini kilikuwa kinaendelea, wahudumu pale hotelini wakaniambia kuwa wale wote niliowaona walikuwa wameenda baharini kujisaidia.

Utamaduni kama huu nimewahi kushuhudia Luanda, Angola, na Addis Ababa, Ethiopia miaka 20 iliyopita. Katika kutangaza kukua kwa uchumi kama kielelezo cha maendeleo tunatumia takwimu kama vile pato la taifa kwa kila mwananchi. Mimi naamini takwimu ambayo inaweza kuonesha maendeleo ya mwanadamu kwa haraka zaidi ni idadi ya uwepo wa vyoo vya kudumu kati ya wananchi 1000 au kaya 1000. Rafiki yangu mmoja, Lionel Mawalla amewahi kuniambia, “Profesa tusihangaike na takwimu za pato la taifa au kipato cha mtu kama kiashiria cha maendeleo. Idadi ya watu wanaokojoa njiani hadharani kati ya watu 1000 ni kipimo kinachoeleweka zaidi”. Nakiri hii ni tabia yetu sisi wanaume. Huwa tunapata soni inapokuja kuelezea suala hili linalohusu usafi wa mazingira pamoja na kwamba ndani yake linabeba dhana nzima ya elimu, afya, kipato, mlipuko wa maradhi, uwezo wa uzalishaji na utamaduni wa jamii husika.

Nimeeleza kwa kirefu zaidi kuhusu usafi wa mazingira kwa kuwa hi ni changamoto kubwa vijijini, iikiwa ni pamoja na Matema. Katika taarifa yake kwa mwandishi wa Makala hii, Ndugu Edson Rugalabamu, Afisa Mtendaji wa Kata ya Matema anakiri kwamba, “Robo tatu ya kaya za Matema wana vyoo visivyo na hadhi. Wao hulichukulia suala la kuwa au kutokuwa na choo kama ni la kawaida. Kati ya Januari na Aprili 2016 watu walioathirika na ugonjwa wa kipindupindu katika kata ya Matema walifikia 36. Wengi wao hawakuwa na vyoo kwenye kata zao”. Juhudi zinaendelea katika kutoa elimu ya afya na usafi wa mazingira, ikiwa ni pamoja na kutumia sheria kuhakikisha kaya zinakuwa na maliwato.


Ilani kuhusu Usafi wa Mazingira


Mhudumu mmoja katika makaazi yetu Matema aliwahi kuniambia, “Mzee naomba uwahi kunipa mshahara wangu wa mwezi. Najenga choo na ningependa kumaliza ujenzi haraka. Kwani wakaguzi wa afya kutoka kyela wanakuja mwisho wa mwezi’’. Hata hivyo, changamoto kubwa katika ujenzi wa vyoo vya shimo Matema na maeneo mengi ya Wilaya ya Kyela ni maji yaliyo chini ya ardhi kupatikana katika kina kifupi sana. Changamoto hii, bila shaka iko ndani ya uwezo wa wataalam wa afya na usafi wa mazingira katika kusanifu aina ya vyoo bora katika mazingira kama haya.


Matibabu

Huduma za tiba hutolewa na Hospitali ya Kiluteri ya Dayosisi ya Konde. Kwa mujibu wa Dk. Christopher Mwasongela, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Matema, chanzo cha huduma za tiba Matema ni kituo kidogo cha afya kilichoanzishwa na wamisionari wa kijerumani mwaka 1905. Huduma katika kituo hicho zilisitishwa mwaka 1916 wakati wa vita kuu ya kwanza ya dunia. Huduma zilianza tena mwaka 1930 na kuendelea mpaka mwaka 1948 wamisionari kutoka Finland walipoamua kujenga zahanati. Mwaka 1985 zahanati ilianza kulaza wagonjwa na mwaka 1998 ikapandishwa hadhi na kuwa Kituo cha Afya cha Matema. Mwezi Septemba, 1997 Kituo cha Afya kikapandishwa hadhi na kuwa hospitali kamili.

Dk. Mwasongela, katika Ripoti ya Mwaka 2015 ya Hospitali ya Matema anafafanua kuwa Hospitali inatoa huduma kwa wakaazi wapatao 13,000 wa eneo la Matema na Ikombe. Nje ya eneo hilo Hospitali inahudumia wagonjwa kutoka vijiji vya jirani vya Kisyosyo, Mababu, Makwale, Ngeleka, Lusungo, Ndobo, na vinginevyo. Wagonjwa wengine hutoka: Makete na Ludewa, Mkoa wa Njombe; Mkoa wa Mbeya; na Mkoa wa Songwe. Wagonjwa wengine wanatoka nchi ya jirani, Malawi.


Hospitali ya Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Tanzania, Matema


Hospitali inatoa huduma kwa wagonjwa wa nje na wa kulazwa katika maeneo yafuatayo: magonjwa ya kawaida; magonjwa ya akili; tiba ya macho; tiba ya meno; uchunguzi wa awali wa saratani ya kizazi na matiti; kliniki ya afya ya uzazi na mtoto; na upasuaji. Hospitali ina vitanda 96 vya kulaza wagonjwa katika wadi za uzazi, watoto, na wadi ya magonjwa mbalimbali ya wanaume na wanawake. Asilimia 46 ya wagonjwa wa nje waliotibiwa katika Hospitali ya Matema mwaka 2015 walikuwa wakiumwa maralia. Asilimia 8 walitibiwa shinikizo la damu. Magonjwa mengine ni minyoo, magonjwa ya zinaa, kuhara, kikohozi, vidonda vya tumbo, kichome, na kisukari. Jumla ya wagonjwa wa nje 14,463 walipatiwa huduma ikilinganishwa na wagojwa 2,668 waliolazwa.

Hospitali ya Matema ina madaktari wanne na wauguzi wapatao 30 na wafanyakazi wa aina mbali mbali. Hospitali hushirikiana na Hospitali ya Wilaya ya Kyela kwa kuazimana wafanyakazi wanaohitajika kwa muda mfupi. Kwa huduma zinazohitaji rufaa wagonjwa hupelekwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda, Mbeya na Hospitali ya Mkoa, Mbeya. Changamoto zinazoikabili hospitali ni pamoja na uhaba wa nguvukazi, hasa katika kada ya wauguzi. Kwani wao wengi hujiuzuru baada ya muda mfupi wa kazi kwa kuwa hupata ajira serikalini ambako kuna masilahi bora zaidi. Mahitaji mengine ni pamoja na wadi ya uzazi, upanuzi wa chumba cha upasuaji, jengo mahsusi kwa ajili ya matibabu ya ukimwi, na vifaa mbali mbali vya uchunguzi na tiba. Hospitali inapokea wanafunzi wa uuguzi na udaktari wanaofanya mafunzo ya muda mfupi ya vitendo. Hospitali pia hupata misaada mbali mbali ikiwa ni pamoja na madaktari wanaokuja kufanya kazi kwa muda mfupi kutoka Ujerumani na Finland wakiletwa kwa msaada wa mashirika ya Berlin Mission Work, Andi Fuerch Foundation, na Finnish Christian Medical Association, kwa ushirikiano na Idara ya Afya ya Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Tanzania.


Elimu

Elimu ya awali, elimu ya chekechea hutolewa kwtika shule za msingi na katika madarasa yaliyoanzishwa na madhehebu za dini za kiluteri na kikatoliki.

Kata ya Matema ina shule za msingi mbili, Shule ya Msingi Matema na Shule ya Msingi Kisyosyo. Shule ya Msingi Matema ilianzishwa na kanisa la Kiluteri na baadaye ikachukuliwa na serikali kuwa shule ya Halmashauri. Imejengwa katika eneo linalomilikiwa na kanisa. Kwa mujibu wa Ndugu Edson Rugalabamu, kitaaluma matokeo ya mitihani ya darasa la saba ni ya wastani. Madarasa ni machache na hivyo hayakidhi idadi kubwa ya wanafunzi. Changamoto nyingine, asema Ndugu Rugalabamu, ni wanafunzi kukosa chakula cha mchana.


Mwalimu wa watoto wa shule ya chekechea ya KKKT Matema


Matema ina shule ya sekondari moja, Nyasa Lake Shore. Jina la shule hii ya sekondari lingepaswa kuwa Matema Beach kwa kuwa iko km 1 kutoka ufukwe wa Matema. Lakini Sekondari inayoitwa Matema Beach iko km 10 hivi kutoka Matema.


Wanafunzi wa Shule ya Msingi Matema wakifurahia ufukwe na kuchota maji


Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Matema, Lusajo Syabo Mwakitalima anaeleza kuwa shule hiyo isiyo ya bweni ilianza mwaka 2009. Ina wanafunzi 275, kati yao 125 ni wasichana na 150 ni wavulana. Ina walimu 24, kati yao mmoja anatoka Shirika la Peace Corps la Marekani. Kitaaaluma shule inafanya vizuri. Mwaka 2016 ufaulu kidato cha pili ulifikia asilimia 100 na kidato cha nne asilimia 88. Mwalimu Mwakitalima anaorodhesha changamoto zinazoikabili shule hiyo kuwa ni pamoja na : ukosefu wa vifaa vyakutosha vya kujifunza na kufundisha; uhaba wa vitabu; upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi na hisabati; bajeti finyu; na upungufu wa majengo.


Ujumbe wa MUST pamoja na Walimu na Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Lake Nyasa Shore


Shule ya Sekondari ya Nyasa Lake Shore ilikuwa shule ya kwanza kutembelewa na Mwandishi wa Makala hii kwa wadhifa kama Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) katika juhudi za Chuo hicho kukutana na walimu na wanafunzi wa shule za sekondari. Nia ni kuelezea umuhimu wa sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati katika maendeleo ya binadamu.


Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Lake Nyasa Shore waisikiliza ujumbe kutoka MUST


Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika hapo shuleni tarehe 27 Septemba 2017, ujumbe wa MUST uliwasisitizia wanafunzi kuwa sayansi na hisabati si masomo magumu kama wanafunzi wengi wanavyofikiria. Bali kama ilivyo katika masomo mengine wanahitaji kuwa na maamuzi sahihi, kujiamini, kuwa na nidhamu, kuheshimu muda, kujiamini, na kuwaheshimu walimu na wazazi wao. Madhumuni pia ilikuwa ni kuwashawishi wasichana kutokuwa na woga kuingia mchepuo wa sayansi na kuwasisitizia kwamba wanaweza kuwa wanasayansi na wahandisi wazuri. Katika ziara hiyo Mwandishi wa Makala hii alifuatana na Profesa Luoga, Naibu Makamu Mkuu wa MUST na Dr. Minja (Mrs), Mhadhiri wa MUST.


Walimu na Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Lake Shore wakijadiliana na ujumbe kutoka MUST


Maji

Maji ni muhimu kwa uhai na kwa shughuli nyingi za kibinadamu ikiwa ni pamoja na shughuli za kiuchumi. Maji safi na salama ni muhimu sana katika kusaidia jamii kupunguza magonjwa kama kuhara, homa ya tumbo, na kipindupindu. Maji safi na salama ni kinga dhidi ya magonjwa yanayotokana na kunywa maji machafu. Umoja wa Mataifa umetamka kwamba upatikanaji wa maji safi na salama ni haki ya kila binadamu.

Kwa matumizi ya majumbani, ikiwa ni pamoja na kunywa, wakaazi walio kandokando ya Ziwa Nyasa hutumia maji ya Ziwa. Shughuli nyingi za kijamii zinafanywa katika ufukwe wa ziwa ikiwa ni pamoja na kuoga, kuogelea, kufua nguo, na kusafisha vyombo, kukausha samaki, kukausha nafaka, na kuanika nyavu. Zaidi ya hapo, mito inayotoka milimani na kuingiza maji ziwani huleta kila aina ya uchafu na takataka. Kama ilivyoelezwa awali, baadhi ya wakaazi wasio na vyoo, au walio na vyoo visivyo na hadhi hutumia Ziwa kama choo kikubwa. Wanashauriwa kuyachemsha kabla ya kuyatumia ili kupunguza uwezekano wa kupata magonjwa.

Mradi wa maji kutoka Mto Mwalalo ulibuniwa na KKKT kwa ajili ya matumizi ya hospitali na kituo chake pamoja na jamii inyozunguka hospitali. Idadi ya watu imeongezeka na huduma za kijamii kama vile hoteli na nyingine, zimeongezeka. Mradi huo hautoshelezi mahitaji makubwa yaliyoongezeka. Kwa bahati nzuri maji yaliyo chini ya ardhi hupatikana kwa urahisi kwa kuchimba visima vifupi na virefu. Hospitali, Hoteli zilizo ufukweni, na baadhi ya wakaazi wamechimba visima virefu kwa ajili ya matumizi yao. Bado Mradi wa maji kutoka Mto Mwalalo unahitaji ukarabati mkubwa ikiwa ni pamoja na kuongeza uwezo wake ili kuhudumia wakaazi wengi katika eneo ambalo baada ya muda mfupi litakuwa mji mdogo. Kutokana na umuhimu wa Matema kama kituo cha utalii, Halmashauri ya Wilaya ya Kyela, kwa kushirikiana na Wizara ya Maji na Umwagiliaji inabidi ione umuhimu wa kutekeleza Mradi wa Mwalalo ikizingatia Sera ya Taifa ya Maji.


Huduma za Kiroho

Katiba ya Nchi yetu inatamka wazi kwamba kama Taifa, Tanzania haina dini, lakini wananchi wake wanaruhusiwa kuwa waumini wa dini mbalimbali, na wanaweza pia kutokuwa na imani za dini yeyote. Hivyo basi wananchi waishio Matema ni wakristo wa madhehebu za kiluteri, kikatoliki, pentekoste, na madhehebu nyingine. Kuna Waislamu wachache. Baadhi ya wenyeji huabudu miungu yao na baadhi yao hawana dini.


Kanisa la Kiijili la Kiluteri Tanzania, Dayosisi ya Konde, Usharika wa Matema


Kati ya madhehebu ya Kikristo waluteri ndio wengi zaidi. Kwani madhehebu hayo yalianzishwa na ujio wa wamisionari wa kijerumani wa Berlin Mission waliowasili Matema mwaka 1893 wakitokea Ujerumani na Afrika ya Kusini. Waliendelea na safari yao mpaka Kipangamansi, au Ipagika katika Kata ya Lufilyo, Busokelo. Baadaye wakaazisha vituo vya dini Itete, Manow, na Mwakaleli, Busokelo. Walianzisha pia vituo Matema na Ikombe. Majengo mawili yaliyojengwa na wamisionari hawa maka 1910, kwa kushirikiana na wenyeji wa Matema mpaka leo yapo na ni kivutio kizuri. Kama ilivyoelezwa awali, mbali na huduma za kiroho, KKKT Dayosisi ya Konde hutoa huduma za afya kupitia hospitali yake. Kituo cha Waluteri kina shule ya chekechea na hutoa huduma za malazi kwa wageni na kumbi za mikutano.


Kanisa la Katoliki, Jimbo Katoliki la Njombe, Parokia ya Matema


Padre Thomas Mwenda, Paroko wa Matema, anaeleza kuwa madhehebu ya Katoliki inatoa huduma zake kupitia Parokia ya Matema ambayo ilianzishwa na wamisionari wa Benediktini mwaka 1968 kama kigango chini ya Parokia ya Lumbila, Wilaya ya Ludewa, kama sehemu ya Jimbo Katoliki la Njombe. Parokia ilianza rasmi mwaka 2009 kutokana na changamoto za kiuchungaji katika mwambao wa Ziwa Nyasa. Parokia inahudumia vijiji vinne; Nkanda, iliyo Wilaya ya Ludewa; Ikombe; Ipuli/Kisyosyo; na Matema. Parokia ina shule mbili za chekechea, Matema na Ikombe. Kituo cha vijana cha kuweka na kukopa kina wanachama 700. Mwaka huu wanawake 106 wamewezeshwa kukopa shilingi 43.9 milioni. Padre Mwenda amemweleza Mwandishi kuwa Parokia pia hutoa semina kwa akina mama na vijana.

Pamoja na idadi ndogo ya waumini wa dini ya Kiislamu, idadi hiyo inakua, na umuhimu wa kuwa na msikiti kwa ajili ya wenyeji na wageni ni dhahiri. Ujenzi wa barabara ya Matema-Kikusya kwa kiwango cha lami utaongeza idadi ya waumini wa madhehebu mbalimbali. Ili kutoa huduma kwa waumini wa dini ya Kiislamu, juhudi za ujenzi wa msikiti zinaendelea katika kitongoji cha Itukisyo, Matema. Mfadhili mkubwa wa ujenzi wa Msikiti huu ni Ndugu Mustafa Kambona Ismail, Mkurugenzi Mshiriki, Benki Kuu, Dar es Salaam. Ujenzi wa Msikiti huu ni mradi unaoendelea. Ni juhudi ambazo inabidi ziungwe mkono na sisi sote bila kujali imani zetu, kama ilivyo desturi zetu Watanzania.


Huduma kwa Wageni na Watalii

Ufukwe wa Matema ni eneo zuri sana na la kuvutia kwa wenyeji, wageni na watalii kutoka ndani na nje ya nchi. Ni ufukwe wenye mvuto wa kipekee. Nadiriki kusema Ziwa Nyasa, safu za Milima ya Livingstone na Ufukwe wa Matema, unaoungana na Ufukwe wa Lusungo, na Ufukwe wa Mwaya, ni zawadi ya Mwenyezi Mungu kwa Tanzania. Kuna baadhi ya huduma kama vile hoteli chache ambazo zimejengwa na nyingine zinaendelea kujengwa. Mahitaji ya vyumba vya wageni vya kulala yataongezeka hasa baada ya barabara ya km 34 inayojengwa kwa kiwango cha lami kutoka Kikusya, Kyela, kuja Matema itakapokamilika. Barabara hii ilianza kujengwa Agosti 2015. Ilitarajiwa kukamilika Julai 2017. Hata hivyo mpaka sasa haijakamilika. Inatarajiwa kukamilika mwakani 2018. Inajengwa na kampuni ya China New Era International Engineering Corporation chini ya usimamizi wa TANROADS Engineering Consulting Unit (TECU).


Ujenzi wa Barabara ya Matema-Kikusya kwa kiwango cha lami


Kituo cha Waluteri

Kwa maelezo ya Mama Gema Moi, meneja wa Kituo cha Waluteri (Matema Beach Lutheran Centre) kituo hiki kilijengwa kwa mara ya kwanza na wamisionari wa kijerumani mwaka 1910 kwa ajili ya mapumziko yao. Baadaye walipoondoka, Kanisa likaamua kuanzisha Kituo. Mwaka 1992, Mkutano wa LMC, unaowashirikisha Waluteri dunia nzima ulifanyika Matema, Dayosisi ya Konde ikiwa ndio mwenyeji wa Mkutano huo. Ilibidi vibanda vichache vya kulala vijengwe ikiwa ni pamoja na ukumbi wa mikutano ambao unatumika mpaka sasa. Lengo la Kituo ni kuwahudumia watu wa Kanisa wanapokuwa na mikutano, ingawa wananchi na wageni wengine wanahudumiwa pia. Kituo kina vyumba 35 na kina uwezo wa kulaza watu 85. Kuna kumbi tatu za mikutano. Ukumbi mkubwa unaweza kuchukua watu 100. Ukumbi wa pili unaweza kuchukua watu 80.


Kituo cha Waluteri, Matema


Kuna ukumbi mdogo ufukweni ambao uko wazi, unaweza kuchukua watu 50 na zaidi. Kwa kuwa eneo hilo ni la wazi, mahema yanaweza kutumika kwa ajili ya mikutano. Baadhi ya wageni huja na mahema yao na kuyafunga ufukweni kwa ajili ya malazi.


Kituo cha Waluteri Matema kilichojengwa zaidi ya miaka 100 iliyopita


Kituo kinatoa huduma ya chakula. Kituo kinashirikiana kwa karibu sana na Hospitali ya Itete na Shule ya Biblia. Kwani vituo hivi vitatu viko chini ya KKKT Dayosisi ya Konde.


Matema Lake Shore Resort

Hoteli ya Matema Lake Shore Resort iko ufukweni. Ilianza kujengwa mwaka 2000 na kukamilika na kuanza kutumika mwaka 2002. Hoteli hii inamilikiwa na Kanisa la Uinjilisti (Evangelistic Church). Hoteli ilijengwa chini ya usimamizi wa Bwana Markus Lehner, raia wa Uswisi ambaye ndiye mwanzilishi wa Kanisa la Uinjilisti, na Mwenyekiti wake wa kwanza. Sasa amestaafu. Chini ya usimamizi wake, katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya Vijijini, Kanisa limejenga: Hospitali Teule ya Ifisi; Chuo cha Ufundi Mbalizi; Kituo cha Wageni na Mikutano Ifisi (Ifisi Community Centre-ICC); na Shule ya Sekondari Sunrise, Songwe. Kanisa pia linasimamia Hifadhi ya Korongo la Ifisi (Ifisi Ravine).


Matema Lake Shore Resort


Kwa mujibu wa Ndugu Joseph Paulo Sinyangwe, Meneja wa Matema Lake Shore Resort (www.mec-tanzania.ch/matema), Hoteli ina vyumba vya kulala wageni na ukumbi wa chakula. Ndugu Sinyangwe anaeleza kuwa kuna jumla ya vyumba 22. Vyumba 4 havina bafu wala maliwato na kila chumba kina vitanda viwili. Vyumba 18 ni kamili kwa maana ya kuwepo kwa huduma ya kuoga na maliwato. Kati ya hivi vyumba 9 vina vitanda viwili, vyumba vitatu vina vitanda vitatu kila kimoja, vyumba 6 ni vya familia ambavyo kila kimoja kinaweza kuchukua familia ya watu wanne. Hoteli ina uwezo wa kuchukua wageni 60 mpaka 68. Hoteli ina wafanyakazi 62, ikiwa ni pamoja na Meneja, Msaidizi wake, na Mweka Hazina. Hoteli ina boti yenye injini kwa ajili ya wageni kuvinjari maeneo ya Ziwa Nyasa.


Matema Lake Shore Resort


Landmark Hotel Matema


Hoteli ya Landmark Matema ni sehemu ya mfumo wa hoteli za Landmark ambazo zinamilikiwa na kampuni ya Landmark Hotels Ltd (www.landmarkresort.co.tz) inayomilikiwa na Mheshimiwa Saul Amon, Mbunge wa Rungwe. Hoteli zake nyingine ni Landmark Tukuyu, Landmark Zanzibar, Landmark Ubungo, Landmaerk Sinza, Landmark Kariakoo, na Landmark Jangwani Beach, Dar es Salaam. Ndugu Amon ni mmiliki pia wa nyumba za wageni zinazojulikana kama Pattaya za Dar es Salaam, Kyela na Tukuyu.


Hoteli ya Landmark, Matema


Hoteli ya Landmark Matema, ambayo iko ufukweni mwa Ziwa Nyasa katika kitongoji cha Ntundu Mano, kijiji cha Lusungo, kata ya Lusungo, ilianza kujengwa mwaka 2014 na kufunguliwa rasmi tarehe 25 Desemba 2016. Kwa maelezo ya Mheshimiwa Saul Amon, hoteli ina nyumba ndogo 18 zinazojitegemea. Kati ya hizo, nyumba 12 zina vyumba viwili kila moja na tano zina vyumba vinne kila moja. Hoteli ina kumbi 3 za mkutano. Ukumbi mkubwa unaweza kuchukua watu 300. Ukumbi wa pili una uwezo wa kuchukua watu 100 na ukumbi mdogo utaweza kuchukua watu 50. Ukumbi wa chakula unaweza kutumika na watu 200 kwa wakati mmoja. Sehemu imetengwa kwa ajili ya kambi ya watalii wanaojitegemea kutumia maturubai au magari yao. Hoteli ina mpango wa kununua boti ya matumizi ya wageni kutalii katika ziwa pamoja ikiwa pamoja na na kuvua samaki. Kwa wale ambao hawapendi kuogelea Ziwani au kama wanapenda lakini kufanya hivyo inakuwa hatari kutokana na mawimbi, hoteli inajenga bwawa la kuogelea.


Moja ya vyumba vya wageni Hoteli ya Landmark, Matema


Blue Canoe Safari Camp

Kambi ya Blue Canoe Safari iko magharibi ya Ufukwe wa Matema. Iko ufukweni pia, Kitongoji cha Ntundu Mano, Kijiji cha Lusungo, Kata ya Lusungo. Kambi hii inamilikiwa na Bi Railat Hamad Nassoro na mumewe Thomas Reinhardt. Kwa maelezo ya Ndugu Michael George Mwamakamba (36) mwajiriwa wa Kambi hiyo, Kambi ilianza kujengwa mwaka 2009 na kukamilika na kuanza kutumika mwaka 2011. Kambi ina vyumba vinne vilivyo ufukweni na vyumba vinne vilivyo upande wa kaskazini.


Kambi ya Blue Canoe Safari


Kila chumba kina uwezo wa kulaza watu wawili. Jumla ya wgeni wanaoweza kujaza vyumba ni 16. Vyumba vilivyo nyuma ya ufukwe havina bafu wala vyoo. Badala yake kuna vyoo na bafu za pamoja za nje. Ukumbi wa chakula unaweza kutumiwa na wageni hamsini kwa pamoja. Sehemu ya ufukweni inatuika pia kama kambi kwa wageni ambao huja na magari yao na kuweka mahema kwa ajili ya kulala. Nafasi inatosha kwa ajili ya mahema yapatayo 20.


Kambi ya Blue Canoe Safari


Kabla ya kubadili jina, kambi hii ilikuwa inajulikana kama Crazy Crocodile Camp. Jina hili lilitokana na uwepo wa mamba Mto Lufilyo ulipokuwa ukiingia Ziwani. Sasa Mto umehamia pale Mto Mbaka ulikuwa ukiingia Ziwani. Mto Mbaka nao umehama na unaingia Ziwani maeneo ya Mwaya. Hata hivyo yamebaki madimbwi katika uliokuwa mkondo wa Mto Lufilyo. Mabwawa hayo ni kivutio kwa watalii kutokana na uwepo wa viboko, mamba na ndege.


Sehemu za Bei Nafuu za Burudani na Wageni Kulala

Hoteli, vituo na kambi za wageni zilizoelezwa katika aya zilizotangulia, pamoja na uzuri wake, ni ghali kwa mwananchi wa kawaida, au mgeni wa kipato cha chini.


Matema Bistro & Restaurant


Kama ilivyo kawaida kwa maeneo mengi ya aina hii, kuna nyumba za kulala wageni na sehemu za burudani ambazo bei ya vyumba vya kulala na hata vinywaji pia, ni nafuu. Uamuzi ni pochi yako mwenyewe. Baadhi ya wageni hulala kwenye hoteli za bei ya juu lakini hutafuta mahala pa kula chakula na vinywaji vya bei nafuu. Sehemu kama hizo ni pamoja na: Matema Bistro & Restaurant; Noah’s Ark Spot Sweden Cafe; na Kwa Paroko.


Noah’s Ark Spot Sweden Cafe


Kwa Paroko


Kuishi “Mpakani”

Imeelezwa katika aya zilizotangulia kwamba Ziwa Nyasa limezungukwa na nchi tatu; Msumbiji, Malawi na Tanzania. Mpaka kati ya Msumbiji na Malawi hauna utata. Kwani kama ilivyo kwa mito na maziwa karibu yote duniani mipaka hupita katikati ya maji hayo. Kwa upande wa Tanzania na Malawi hali haiku hivyo. Tanzania inashikiria taratibu za kimataifa kuhusu majishirikishi yanayozihusu nchi mbili; kwamba mpaka unapita katikati ya Mto Songwe na kupita ndni ya Ziwa Nyasa mpaka unapokuwa katikati ya Ziwa na uko katikati ya Ziwa kuelekea kusini mpaka unapokutana na mpaka wa Msumbiji na Malawi. Malawi ina tafsiri tofauti. Mpaka unaambaa uukweni mwa Ziwa kutoka Msumbiji mpaka Mto Songwe. Suala hili linashughulikiwa na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini wa Afrika kupitia Tume ya Watu maarufu ikiwajumuisha Marais Wastaafu: Festus Mogae wa Botswana; Thabo Mbeki wa Afrika ya Kusini, na Joaquim Chissano wa Msumbiji.

Bila kuingilia upatanishi wa Wazee hawa, wenyeji waishio mwambao wa Ziwa upande wa Tanzania wanashangaa kuwapo kwa sintofahamu kuhusu mpaka. Kwao Ziwa Nyasa ni zawadi yao kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Wanasema wamekuwa wakisafiri, wakivua, na wakitumia maji ya Ziwa bila kikwazo chochote kuanzia vizazi na vizavi vilivyopita. Wengi wao wana asili ya upande wa pili wa Ziwa kama ilivyo kwa walio upande mwingine walivyo na asili ya huku. Wanashangaa kuambiwa wakikanyaga maji basi wako nchi nyingine.

Picha iliyo hapo chini inaonesha jinsi ambavyo ukiamini kwamba ukingo wa maji ndio mpaka, mpaka huo unabadilika kila dakika kufuatana na mawimbi. Tofauti ya mpaka inaweza ikawa zaidi ya mita 40 katika msimu mmoja. Nchi ipi itakubali mpaka wake uhame mita hizo? Picha hii ni kielelezo cha busara zilizotumika katika kutambua mipaka ya majishirikishi ipite katikati ya maji hayo.


Ufukwe wa Matema ukionesha jinsi mpaka kati ya Ziwa na Nchi Kavu unavyobadilika


Majumuisho

Waraka huu umeandikwa kujibu changamoto Mwandishi aliyopewa na wwasomaji wa Waraka wake wa kwanza uliotoa Salaam Kutoka Comoro. Kwa mfumo ule ule ameona vema akaandika na kuwapa Salaam Kutoka Matema. Amelenga katika kuelezea, na hivyo kusambaza yale aliyoyaona, aliyojifunza na yale ambayo angependa wengine wajifunze kuhusu eneo hili la Ziwa Nyasa, lenye mvuto wa kipekee na lililosheheni mandhari na mazingira mazuri. Wageni wengi wanaofika Matema huvinjari kwa kutembelea maeneo mengi. Ni wachache kati ya wenyeji wa Nyanda za Juu Kusini wanaofika Matema. Wengi wao, ikiwa ni pamoja na Watanzania wengine wanaofika Matema huishia kuogelea au kupumzika ufukweni. Waraka huu unaonesha Matema ni zaidi ya ufukwe, mchanga na jua.

Kwa wale ambao wangpenda kufika Matema, Waraka huu umejaribu kuwaeleza watarajie nini watakapofika, kwa maana ya mandhari, huduma za kitalii ikiwa ni pamoja na mahali pa kulala, migahawa, vyumba vya mikutano, na nyumba za ibada. Huduma nyingine ambazo wageni wangependa kujua zipo ni pamoja na maji na hospitali.

Umuhimu wa usafi wa mazingira inabidi uzingatiwe na serikali ya Kijiji na Kata ya Matema ili kupunguza uwezekano wa milipuko ya magonjwa ya kuambukiza. Utunzaji wa mazingira hasa mazingira na uoto asili wa safu za milima ya Livingstone ni suala ambalo bado halijapewa kipaumbele. Ukataji miti ya asili unaendelea bila usimamizi. Kilimo kisicho endelevu kinafanyika kwenye miteremko ya milima bila udhibiti wowote. Uchomaji moto milimani wakati wa kiangazi umekithiri. Mito mingi inayoingia Ziwa Nyasa kutoka Kaskazini huanzia kwenye milima ya Livingstone. Baadhi ya samaki wa Ziwa nyasa hutumia fukwe za mito hiyo kama mazalio. Uharibifu wa mazingira ya milima hatimaye utaathiri ikolojia ya Bonde la Ziwa nyasa. Ushauri unatolewa kwa Wizara, Mikoa, Wilaya, Halmashauri, Kata, Vijiji na taasisi zinazohusika kuandaa mkakati kabambe wa utunzaji wa mazingira na vyanzo vya maji katika Bonde la Ziwa Nyasa.

Wasaalam


Mark Mwandosya
Matema Beach
Ziwa Nyasa
Tanzania


Oktoba, 2017


Copyright© 2017 Mark Mwandosya. All rights reserved

Comments


 1. Asante sana kwa Salam kutoka Matema Beach. Zaidi ya Salam Ni ile kazi kubwa uliyoifanya ya kutujuza kuhusu yaliyopo Matema. Inshallah ipo Siku tutatembelea eneo hilo. Be blessed
  Nicholas Mbwanji

  ReplyDelete
 2. Prof. Shikamoo, asante kwa salama kutoka Matema Beach! Utalii ulioufanya umenitia hamasa kuu ya kutembelea Matema siku si nyingi!

  Nimetamani sana kufika nijionee mwenyewe na kuwala samaki Kama Usipa ambao ninahisi hawatakua na tofauti sana na dagaa Wa Mwanza ama basi watafanana kwa radha na Migebuka ya kigoma kwao Peter Serukamba, Zitto Kabwe na Sanzukwanko. Nikifika huko nitawala kitoga, mbasa na Kambale na wengineo

  Nikifika Matema nitakwenda pia kwenye bonde la Pali-Kyala na maporomoko ya mto Mwalalo. Siku ya kuondoka nitamnunulia zawadi mama yangu Elizabeth Lwahaha ya vyungu vyenye mapambo toka kwenye soko la Lyulilo, Bernadetha mke wangu nitamnunulia mchele Wa Kyela.


  Waraka wako toka Matema pamoja na kutangaza utalii na uzuri Matema umenipa somo Kama mwanasiasa mchanga, somo la kwanza ni la Utawala Bora, nimewaza kulikua na haja gani ya mtalii Wa kizungu kutozwa faini kwa kosa ambalo pengine hapakua na kibao ama tahadhali yeyote?

  Nimejiuliza mtalii huyo Wa kijerumani akirejea kwao atahubiri uzuri wa Matema kwa wengine ili tupate fedha nyingi zaidi toka kwa watalii zaidi? Nawaza kwa sauti tu hivi gharama ya dola 100(hata Kama angelipa) inaweza kutupotezea watalii wangapi?
  Kwanini kuviziana??

  Somo la Pili kuinua maisha ya wananchi kiuchumi.

  Professor, nimewaza wavuvi ambao toka Zama za mababu zao waliishi kwa kuvua katika ziwa Nyasa kwa mfumo wanaoendelea nao. Nini tumefanya kuwabadilishia mfumo kwa kuwapa mafunzo na elimu ya uvuvi Wa kisasa?
  Najiuliza unapowanyang'anya nyavu na kuziuza upande Wa Pili lengo ni kuwasaidia ama kuwafanya masikini.

  Lakini hizo nyavu si huuzwa sokoni na huingizwa kwa Njia zinazojulikana? Kwanini tusidhibiti uingiaji ili zisimfikie mvuvi asiye na maarifa ya vipimo vya nyavu!

  Aaaaah basi nisikuchoshe Profesa, najaribu kuwaza tu kwa kuandika.

  Ziara yako Matema imenipa hamasa ya kutembelea maeneo hayo, najua kwa kuembelea huko nitakuja na misamiati michache ya kinyankyusa nimewasikia wenyeji Wa kikusalimia na wewe ukijitabulisha kuwa wewe ni Mwandosya.

  Naamini wengi walitamani kukuuliza mengi juu ya maisha yako, naamini wangekuuliza maisha yako ya kitaaluma na wengine maisha yako ya kisiasa na baada ya kustaafu, wapo ambao wangetaka maoni yako juu ya chama cha mapinduzi kinavyotawala hata sasa; wasingekosa wachache wangekuomba tathimini yako juu ya serikali yetu ya awamu ya tano!!!!

  Nawaza tu maana q
  mtu akikutana na wewe atatamani aandike kitabu kwa siku moja!

  Binafsi nakumbuka sana hotuba yako ya wakati unaomba kuteuliwa na CCM kugombea urais Wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2005 pale Chimwaga na ile uliyoitoa kwenye mahafari ya chuo kikuu cha mtakatifu Agustino Mwanza.

  Hotuba hizo nazikumbuka na zinaishi hata leo na ninafikiri wale ambao wangepata nafasi ya kuongea na wewe hapo Matema wangevuna mengi.
  Asante sana kwa waraka Wa salaam toka Matema na msalimie sana Mzee Mwangalaba.
  Karibu sana Bukombe
  Doto Biteko

  ReplyDelete
 3. Kuna mahali uliongelea loch-ness monster.. did u mean binamu?
  Nimekua interested na mzee Abudike John Mwangalaba..85yrs na ameweza kukutajia aina zote za samaki
  Anonymous

  ReplyDelete
 4. Kweli wewe Professor hiki ni kitabu kizuri kikamilishe na hongera sana.
  Joyceline

  ReplyDelete
 5. Asante sana Kaka M.Mwandosya KWANZA salaam zako kitoka hapo Matema Beach. Mimi ni mzima wa afya njema. GOD BLESS YOU MY DEAR BROTHER.STEPHEN MASHISHANGA

  ReplyDelete
 6. PROFESA nimeangalia sana blog yako, ni nzuri, ushauri wangu, kule juu mwanzo ulikoweka picha yako ungeweka picha madhari ya mlima Rungwe, pili ungeanza kwa kuelezea historia ya wilaya ya Rungwe ilivyoanza, idadi ya watu, vivutio vya utalii nk, tatu kuna wale machifu nao watajwe, Nne,kuna zile meli zinazotoa huduma ziwa nyasa picha zake zingewekwa, Tano, taja aina ya samaki wanaopatikana ziwa nyasa, idadi ya watalii wanaotembelea Matema Beach.
  Thobias Mwanakatwe

  ReplyDelete
 7. Shikamoo mzee wangu asante kwa hizi reflections zako. Ila nina shida moja, niliwahi kulitaja suala la climate change kama moja ya threat to our national security, nikwataka wahusika walitizame kwa dimension hiyo, kwa sababu ya ignorance ya mtu mweusi, hilo hawakuliona kabisa.
  [27/10, 13:26] Nyakikotyo TISS: mambo uliyoelezea humu ni muhimu mno, lakini utakuta ukiwaeleza wanakwambia kipaumbele ni kukusanya kodi na miradi ya maendeleo. hainijii akilini kwa binadamu mwenye akili timamu, haoni kama huwezi kukusanya kodi, huku mito inakauka, samaki wanapotea, jangwa linazidi kunyemelea nchi, ukame na njaa vinaikumba nchi na dunia kwa kasi. msisitizo wa nchi ya viwanda na miradi mikubwa iende sambamba na mkazo katika suala zima la kutunza mazingira, hili ni suala lisiloepukika na linahusu zaidi uhai wa binadamu kuliko hata kukusanya kodi.
  Anonymous

  ReplyDelete
 8. Prof.kwa kweli nashindwa jinsi ya kukushukuru kwa elimu kubwa niliyoipata kutokana na maelezo yaliyo katika salaam zako toka matema beach. Nakushukuru sana na Mungu akupe nguvu zaidi ili uendelee kutufumbua macho. Ahsante sana.
  Balozi Raphael Korosso

  ReplyDelete
 9. Ndugu Mhe. Mark Mwandosya, kwanza kabla ya yote; Shikamoo.
  Nimesoma waraka wako wa salaam kutoka Matema Beach toka mwanzo mpaka mwisho kwa furaha na kupendekezwa kwa yale ambayo nilikua nayasoma bila kuonyesha uchovu wowote. Nimefurahi na kushangazwa sana kufahamu mahali hapa, Tanzania, ambapo nilikua sipafahamu kabisa.
  Mke wangu atakuja Tanzania kutoka Uswizi mwezi wa novemba na nitafurahi sana kama nitaweza kukuibia muda wako kwa siku 1 au 2 na kuja kukutembelea pamoja na mke wangu!
  Kwa sasa nakutakia usiku mwema na asante sana kwa kushare nami waraka ya Matema Beach. Asante sana kwa kunijulisha zaidi kuhusu nchi yangu.

  ReplyDelete
 10. Mark. Hongera Kwa Kazi kubwa ya kukusanya na kuandika "salaam kutoka Matema Beach". Umeiweka kwa namna ambayo inatamanisha watalii wa ndani kuiweka Matema Beach kwenye "bucket list". Indeleze kazi nzuri uliyo anza. Strato.

  ReplyDelete
 11. Mwenyekiti, Mzee wetu Mwandosya analo jicho jingine katika utalii. Amefanya kazi kubwa kuutangaza utalii wa kwetu ziwa Nyasa. Mwaka huu, yeye,Felix Mwakyembe na Albano Midelo wamenisisimua sana. Hakika waliongeza hamasa ya juhudi zangu kuandika mengi kuhusu Nyasa. Mwisho nimsahihishe kidogo; hakuna bandari ya Lituhi, bali bandari ya Ndumbi. Bandari za ziwa Nyasa;Itungi,Lupingu,Manda,Ndumbi,Lundu,Mkili,Njambe,Liuli na Mbamba Bay.

  Wasalaamu
  Markus.

  ReplyDelete
 12. Mwenyekiti napenda kuchukua nafasi kukiri kuwa Prof Mark Mwandosya napenda sana maandiko yake, nimebahatikabkusoma vitabu vyake vinne kwa kweli ni katika vitabu nilivyovisoma haraka sana kutokana uzuri na utamu wa maandiko.
  Leo nimebahatika kusoma hii salam kutoka Matema beach huku nikitabasamu.
  Hakika Max Mwandosya inabidi unikutanishe na Mhandisi mawasiliano mwenzangu
  Makuliro James

  ReplyDelete
 13. Ahsante sana kwa andiko zuri kuhusu Matema Beach. Mimi ni mtembeleaji mzuri sana wa eneo hilo. Nimefurahi kupata maelezo ya kina.

  ReplyDelete
 14. Mzee Mwandosya,nimesoma makala yako kuhusu ziwa Nyasa, mm ni AFISA Uvuvi Niko wizarani. Kwa kweli umetusaidia naomba. Umeandika masuala ya Uvuvi km mvuvi mbobezi. Mungu akubariki sanaaaa
  Owen Kibona
  31 Desemba 2017

  ReplyDelete
 15. Tulifanikiwa kufika hapo matema mwezi uliopita,tulikuja kama staff,mazingira ni mazyri sana ,Prof hongera kwa nyumba nzuri .Mungu awe nanyi

  ReplyDelete

Post a Comment

Popular posts from this blog

Salaam kutoka Comoro

A Letter to Comrade Martin Thembisile (Chris) Hani

A Letter to Comrade Martin Thembisile (Chris) Hani

April 10, 2018
Comrade Chris, To an ordinary mortal it would seem odd that I should communicate with you, us being worlds apart. To a Christian, such as I am, and to you, born a Catholic, being a committed member of the South African Communist Party (SACP), notwithstanding, the belief in and notion of life in the world after comes naturally. Furthermore, very African as both of us are, we firmly believe in the presence in our midst, of the souls of the departed, residing in, among other places, the hills and mountains, the valleys, the pristine forests and woods, and in our homes, among other beauties mother nature has endowed mother Africa. I therefore have no hesitation whatsoever in undertaking this mission of communicating with you Comrade Hani, coming as it does, on the 25th anniversary of your departure.
The chilly southern hemispherical autumn Easter Saturday of 10th of April, 1993, was the longest day in the final struggle for th…