Skip to main content

Kwaheri Mhandisi Ngusa Izengo
Kwaheri Mhandisi Ngusa Laurent Izengo


1972 - 2018


Mwaka 2008, niliteuliwa kuwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji. Awali ya hapo nilikuwa Waziri wa Nchi (Ofisi ya Makamu wa Rais) Mazingira, na kabla ya hapo, Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi. Moja ya changamoto kubwa ya Waziri awaye yote ni kumpata Katibu wa Waziri ambaye ndiye msaidizi mkuu, mratibu na msimamizi mkuu wa ofisi ya Waziri. Katibu Mkuu wa Wizara ambaye ndiye afisa mtendaji mkuu wa Wizara, akisaidiwa na Mkurugenzi wa Utumishi ndio wanaomsaidia Waziri katika kumpata mmoja wa watumishi waandamizi, kuwa Katibu wa Waziri. Kwa kuwa Katibu wa Waziri anafanya kazi na Waziri, basi anayependekezwa lazima akubalike na Waziri.

Katibu ndiye anayepanga ratiba ya kazi ya Waziri. Katibu wa Waziri ndiye anayewaona kwanza wageni wote wa Waziri. Katibu ndiye anayechukua kumbukumbu ya vikao vyote vya Waziri. Katibu wa Waziri ndiye kiungo cha muda wote kati ya Waziri na watendaji wa Wizara. Ingawa Katibu Mkuu na Naibu Waziri au Mawaziri wenzake wana mawasiliano ya moja kwa moja, Katibu wa Waziri ndiye atakayefuatilia utekelezaji wa yale yatokanayo. Kwa kuwa ofisi ya Waziri huwa na mawasiliano ambayo kwa mujibu wa taratibu ni SIRI, ikiwa ni pamoja na nyaraka za Baraza la Mawaziri, Katibu wa Waziri lazima afanyiwe upekuzi na vyombo vinavyohusika.

Ni dhahiri kutokana na yaliyotangulia kwamba Katibu wa Waziri ni mtu muhimu sana katika Wizara. Lazima awe mchapakazi, ikiwa ni pamoja na  kuchapakazi nje ya saa za kazi. Lazima awe mwadilifu, mwaminifu, na awe tayari kumshauri Waziri ipasavyo bila kujali Waziri ataupokeaje ushauri huo, ili mradi ni wa manufaa kwa Wizara na Taifa.

Hivi ndivyo nilivyo kubali ushauri wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Maji na Umwagiliaji alivyopendekeza, nami nikakubali, uteuzi wa Ngusa Izengo, kuwa Katibu wangu. Sifa zote zilizo hapo juu zilimlenga yeye. Zaidi ya hayo Ngusa alikuwa mnyenyekevu, hana makuu, rafiki wa kila mtu, awe mdogo au mkubwa, kwa umri au kwa cheo. Chuki na hasira havikuwemo kabisa katika istilahi ya lugha yake. Aliizoea, bila kinyongo au kulalamika, ratiba yangu ya kazi iliyokuwa ngumu, watumishi wanapoondoka kurudi makwao saa 9.30 mchana, ndio kwanza tunaaza kazi mpaka saa 3 usiku kama tukiwahi. Safari za ghafla ni za kawaida kwa Waziri. Vikao vya dharura vinaweza kuitishwa ama Ikulu, Dar es Salaam, au Dodoma, na Katibu alikuwa tayari wakati wowote.

Tanzania labda ni nchi pekee katika kanda yetu ambapo hata Mkuu wa Nchi anajua, kuhusiana na ujenzi kwamba Zege Halilali. Msemo huu wa wajenzi niliutafsiri kwamba kazi inayobidi kumalizika leo, iishe leo. Niliwakumbusha watendaji kuwa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, alituasa kwamba Linalowezekana kufanywa leo, lisingoje kesho. Ngusa aliusimamia vilivyo mwongozo huu, ndani ya ofisi na kwa wale waliohusika na utekelezaji wa maelekezo ya Waziri. Ilimgharimu muda na afya. Lakini alitekeleza wajibu wake ipasavyo.

Kama ilivyokuwa kwa watendaji wote tuliofanya kazi pamoja, pamoja na ufinyu wa muda, nilimshauri asiishie na shahada ya uhandisi tu bali ajiendeleze zaidi. Ushauri huu aliuzingatia na akajiandikisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuhitimu shahada ya uzamili katika usimamizi wa uhandisi.

Taratibu za Serikali zinamtaka Waziri anapohama asihame na wasaidizi wake. Hata hivyo ilibidi nijenge hoja kwa Katibu Mkuu mwenye dhamana ya Utumishi aruhusu Ngusa aende na mimi Ikulu. Kwani mwaka 2012 niliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi (Ofisi ya Rais) Kazi Maalum.

Ukaribu wa Waziri na Katibu wake unamfanya Katibu awe karibu sana na familia ya Waziri. Hakika Ngusa alikuwa sehemu ya familia ya Mwandosya. Kwa maana hii kifo cha Ngusa kimetusikitisha wote katika familia: Mimi na Mama, na vijana wetu, Max, Sekela na Emmanuel; Godfrey na Joyceline na familia yao; Wananchi wa Busokelo (Rungwe Mashariki); Wizara ya Maji na Umwagiliaji; Ikulu; Halmashauri na wananchi wa Wilaya ya Kongwa; na Watendaji wengi ndani na nje ya nchi. Kama alivyokuwa mwanafamilia, sisi tutashauriana na familia ya Marehemu Ngusa Izengo kuona ni jinsi gani tunaweza kuwajibika katika kuhakikisha watoto wa Ngusa wanaendelea kupata elimu bora.


Walioketi: kushoto Prof. Mark Mwandosya, kulia Mama Christina Nsekela.
Waliosimama, kuanzia kushoto: Ngusa Laurent Izengo, Mama Lucy Mwandosya, Baba Askofu Israel-Peter Mwakyolile, Mama Mchungaji Mwakyolile, Baba Askofu Lusekelo Mwakafwila, na Mama Mwakafwila, tulipomtembelea Mama Nsekela, kijijini Kalalo Juu, Kyimo, Rungwe.Picha ilipigwa 2015.


Nikiwa katika matibabu huko Hyderabad, India, Ngusa alikuja kunijulia hali. Alinikuta katika hali mbaya, nikiwa siwezi kutembea. Nakumbuka Ngusa akisema “Mheshimiwa, mimi naamini utapona kabisa na utaanza kutembea tena. Maadui zako na hao waliokuzushia kifo watashangaa kabisa”.Ngusa Izengo, kulia, akichukua picha ya pamoja na Prof. Mark Mwandosya, kushoto, na Mama Lucy Mwandosya, alipoenda kumjulia hali Waziri Mwandosya, alipokuwa matibabu, Hospitali ya Apollo, Hyderabad, India. Hii ilikuwa mwaka 2011.

Kwa mujibu wa Maelezo Binafsi ya Marehemu, Ngusa Laurent Izengo alizaliwa tarehe 14 Aprili 1972 huko Chato, Geita. Alianza elimu Shule ya Msingi Mweri mwaka 1981 na kuhitimu darasa la saba mwaka 1987. Elimu ya sekondari aliipata Shule ya Sekondari ya Lake, Mwanza, kidato cha kwanza mpaka kidato channe, 1988-1992, na Shule ya Sekondari Kibaha, 1993-1995. Baada ya hapo alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1996 na kufuzu shahada ya kwanza ya Uhandisi Ujenzi mwaka 2000. Marehemu ameacha mke, Flora Lyambogo Izengo, na watoto wawili, Augustine Izengo, na Hellen Izengo.

Kwa familia ya Ngusa, wazazi, mke na watoto, ndugu na marafiki, maneno ya faraja hatunayo. Kwani kwa lolote tutakalosema halitamrudisha Ngusa. Faraja tuliyonayo, na Kama Mfalme Daudi alivyonena katika Agano la Kale, na bila kuharibu maana ya maneno yake: Ngusa ametutoka. Huko aliko hawezi kurudi. Bali faraja tuliyonayo ni kwamba sisi tutaenda huko aliko. Itakuwa furaha iliyoje tutakapoonana naye katika mtaa wa amani ya milele huko mbinguni. Basi wafiwa, ndugu zangu, Mwenyezi Mungu atupe subira, na tuendelee kufarijiana.

Mwenyezi Mungu Amrehemu Ngusa Izengo.

Bwana Alitoa, Bwana Ametwaa. Jina la Bwana lihimidiwe.

Inna Lillahi wa Inna Ilaihi Rajiun.


Mark Mwandosya
Lufilyo
Busokelo
16 Aprili 2018

Ngusa Izengo, kulia kwa mama, akiwa na Profesa Mark Mwandosya na Mama Lucy Mwandosya wakiwa mpakani mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Rwanda (Goma na Gisenyi).

Copyright© 2017 Mark Mwandosya. All rights reserved

Comments

Post a Comment

Popular posts from this blog

Salaam kutoka Matema Beach, Ziwa Nyasa, Tanzania

Salaam kutoka Matema Beach, Ziwa Nyasa, Tanzania
Utangulizi

Mwezi Agosti 2017 nilipata nafasi ya kusafiri kwenda Jamhuri ya Visiwa vya Comoro. Comoro ni umoja wa visiwa vinne; Ngazija, Nzuwani, Mwali, na Maore. Hata hivyo kisiwa cha Maore au Mayotte kinasimamiwa na Ufaransa mpaka hapo wananchi wa Maore watakapoamua kuungana na visiwa vingine. Comoro inaendelea kukitambua kisiwa cha Maore kama sehemu ya Umoja wake. Mimi na familia yangu tulizuru visiwa viwili kati ya hivyo vinne, Ngazija na Nzuwani.

Nikiwa Comoro niliandika waraka niliouita “Salaam kutoka Comoro” na kuusambaza katika mtandao. Watu wengi wamepata nafasi ya kusoma waraka huo. Baadhi yao, pamoja na kunipongeza walinishauri, na hakika walinipa changamoto kuhusu umuhimu wa kuandika waraka kama huo lakini ukilenga kuitangaza Tanzania, kwa watanzania na wageni. Unaanzia wapi kuandika kuhusu Tanzania, nchi iliyojaaliwa na Mwenyezi Mungu kuwa na rasilimali asilia zisizo na mfano duniani? Aidha watu wengi wameandika kuhusu utajir…

Salaam kutoka Comoro

A Letter to Comrade Martin Thembisile (Chris) Hani

A Letter to Comrade Martin Thembisile (Chris) Hani

April 10, 2018
Comrade Chris, To an ordinary mortal it would seem odd that I should communicate with you, us being worlds apart. To a Christian, such as I am, and to you, born a Catholic, being a committed member of the South African Communist Party (SACP), notwithstanding, the belief in and notion of life in the world after comes naturally. Furthermore, very African as both of us are, we firmly believe in the presence in our midst, of the souls of the departed, residing in, among other places, the hills and mountains, the valleys, the pristine forests and woods, and in our homes, among other beauties mother nature has endowed mother Africa. I therefore have no hesitation whatsoever in undertaking this mission of communicating with you Comrade Hani, coming as it does, on the 25th anniversary of your departure.
The chilly southern hemispherical autumn Easter Saturday of 10th of April, 1993, was the longest day in the final struggle for th…