Kwaheri 

Mzee 

Al Noor Kassum

KWAHERI MZEE AL NOOR KASSUMPatrick Rutabanzibwa*


Mark Mwandosya**
Mzee Al Noor Kassum, maarufu “Nick” kwa marafiki zake, alifariki tarehe 18 Novemba na kuzikwa tarehe 20 Novemba 2021. Pamoja na kwamba alizaliwa katika familia tajiri ya wafanyabiashara wenye asili ya Kihindi, wakati wa harakati za kutafuta uhuru wa Tanganyika alikuwa mmoja wa watu wa karibu sana wa Mwalimu Julius Nyerere. Baada ya uhuru aliteuliwa kuwa Waziri Mdogo wa Elimu, na baada ya hapo alitumikia katika Umoja wa Mataifa kama Balozi wa UNESCO na Katibu wa Baraza la Masuala ya Kiuchumi na Kijamii (ECOSOC). Alirejea Tanzania mwaka 1970 ambapo aliteuliwa na Serikali kushika nafasi ya Naibu Meneja Mkuu wa kampuni ya Williamson Diamonds, Mwadui. Baada ya hapo aliteuliwa kuwa Waziri wa Fedha na Utawala wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Jumuiya ilipovunjika mwaka 1977, Mwalimu Nyerere alimteua kuwa Waziri wa Maji, Nishati na Madini, nafasi ambayo aliishika kwa miaka 13 mfululizo hadi mwaka 1990 alipostaafu. Akiwa Waziri Mdogo wa Elimu, alishughulikia uanzishwaji wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Dar es Salaam kikiwa sehemu ya Chuo Kikuu cha Afrika Mashariki. Alihusika pia na upatikanaji wa eneo la ‘Observation Hill’ (Mlimani) ambako kimejengwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.


Tulipata bahati ya kufanya kazi na Al Noor Kassum kuanzia mwanzoni mwa miaka ya 1980 alipokuwa Waziri wa Maji, Nishati na Madini. Alikuwa kiongozi mwenye upeo mkubwa: Mchapakazi; mfuatiliaji sana wa utekelezaji wa kazi; mtu aliyependa kuwahamasisha watendaji kuiga mwenendo wake badala ya kuwashurutisha; mwenye kipaji cha kujenga ushirikiano wa karibu kati ya wote aliowaongoza; na aliyesikiliza na kuthamini ushauri wa wataalamu bila kujali umri wao wala vyeo vyao. Aliheshimu sana sheria na taratibu zote husika katika utekelezaji wa majukumu yake. Uzalendo wake haukuwa wa kujinadi. Ulijidhihirisha katika vitendo, siyo maneno.


Kwa lengo la kukabiliana na changamoto za sekta ya nishati zilizojitokeza duniani kote mwishoni mwa miaka ya 1970 na mwanzoni mwa miaka ya 1980, alijenga hoja Serikalini ya kuanzisha idara maalumu ya kushughulikia na kuratibu masuala yote ya nishati. Yeye binafsi alihusika katika kujenga timu ya kufanikisha lengo hilo. Alimtafuta mhadhiri mmoja kijana wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambaye alikuwa anafundisha na kufanya utafiti juu ya masuala ya nishati, akamchukua kuwa mshauri wake, na baadaye akapendekeza Rais Julius Kambarage Nyerere amteue kuwa kamishna wa Masuala ya Petroli kwa mujibu wa sheria. Hivyo ndivyo Prof. Mark Mwandosya alivyoteuliwa kuwa Kamishna wa kwanza wa Nishati na Petroli na Mkuu wa Idara ya Nishati. Vilevile, alimuazima kijana mwingine kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na kumfanya msaidizi wake katika kufuatilia miradi ya mafuta na gesi, na baada ya kumpa uzoefu katika ufuatiliaji na uratibu akamhamishia katika Idara ya Nishati. Ndivyo Patrick Rutabanzibwa alivyokuja kuwa msaidizi mmojawapo wa Mark Mwandosya mwaka 1985 na kuteuliwa katika nafasi yake ya Kamishna wa Nishati na Petroli baada ya Mark Mwandosya kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Nishati na Madini mwaka 1990.


Juhudi za Waziri Kassum za kuijenga na kuiwezesha Idara ya Nishati kupata rasilimali watu hazikuishia hapo. Alielekeza vijana wengine wahandisi wa Idara ya Maji wenye uwezo mkubwa, Bashir Mrindoko, Estomih Sawe na Shaban Mgana, wahamishiwe kwenye Idara ya Nishati. Aidha, alimvuta kijana mwingine, Theodore Kapiga, mchumi, kutoka Mamlaka ya Bonde la Mto Rufiji (RUBADA) kujiunga na Idara, pamoja na mhandisi, Vincent Gondwe (sasa marehemu) ambaye kabla ya kuanzishwa kwa Idara ya Nishati alikuwa akishughulikia masuala ya nishati akiwa katika Idara ya Sera na Mipango ya Wizara.


Baada ya kuanzishwa ikiwa na watendaji hao wachache, Idara ya Nishati iliendelea kukua na kuongeza uwezo wake wa kusimamia utekelezaji wa sera, mikakati na mipango ya uendelezaji wa sekta ya nishati. Prosper Victus, Lutengano Mwakahesya, Ngosi Mwihava, Theophillo Bwakea na Charles Omujuni ni baadhi tu ya watendaji walioajiriwa Idara ilipokuwa changa kabisa, na baadaye wakahamishiwa na kutoa mchango mkubwa katika taasisi nyingine za Serikali zilizo ndani na nje ya sekta ya nishati.


Waziri Kassum alijenga uhusiano mzuri wa kikazi na Mawaziri wenzake, pamoja na Makatibu Wakuu wake Frederick Lwegarulila (marehemu); Harith Bakari Mwapachu (marehemu); Athumani Janguo; Fulgence Kazaura (marehemu); na Paul Mkanga. Uhusiano huo uliwezesha maamuzi juu ya masuala mbalimbali ya Wizara yake kufikiwa na kutekelezwa kwa ufanisi. Pia alitumia uzoefu wake katika mahusiano ya kimataifa kuwashawishi Washirika wa Maendeleo kutoa fedha kwa ajili ya miradi ya nishati na kugharimia wataalamu washauri kutoka nje ya nchi ambao waliletwa katika Wizara na mashirika yake kuwasaidia watendaji kushughulikia masuala ya uendelezaji wa umeme, mafuta na gesi, na nishati jadidifu. Baadhi ya wataalamu hao – kwa mfano Roger Nellist kutoka Uingereza (aliyeletwa na Sekretariati ya Jumuiya ya Madola), Sigurd Heiberg na Farouk Al Kasim kutoka Norway (waliotoka Statoil na Norwegian Petroleum Directorate), Dr. Kokitil Narayanan kutoka India (Oil & Natural Gas Commission) na Paul Precht kutoka Canada (Canadian International Development Agency) – waliendelea kujihusisha na juhudi mbalimbali za kuendeleza rasilimali watu katika Idara ya Nishati, TPDC na Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) kwa miaka mingi baada ya kurejea katika nchi zao.


Idara ya Nishati ilijenga utamaduni ambao uliipa sifa ya kuwa moja ya Idara za Serikali zilizokuwa na watendaji wachapakazi, wawazi na weledi. Mwaka 2004, wakati mrithi wa Waziri Kassum, Mhe. Jakaya Kikwete, alipokabidhi ofisi ya Waziri wa Maji, Nishati na Madini kwa mrithi wake Mhe. Jackson Makwetta (marehemu), alimtahadharisha kwamba Idara hiyo ina watendaji wabishi sana lakini wako makini, na ole wake apuuze ushauri wao. Kwa kiasi kikubwa tahadhari hiyo ilitokana na uongozi bora wa Waziri Kassum, ambaye aliwaandaa na kuwaendeleza kiutendaji maofisa wengi wa Idara waliopata fursa ya kufanya kazi naye.


Hivyo basi, si jambo la kushangaza kwamba Waziri Kassum aliweza kuchangia maendeleo ya sekta za maji, nishati na madini kwa kiwango tunachokishuhudia hadi leo na kuacha urithi wa kudumu. Yafuatayo ni baadhi tu ya mambo muhimu aliyoyafanya wakati alipokuwa Waziri wa Maji, Nishati na Madini:


Pamoja na mafanikio aliyoipatia Serikali akiwa kiongozi wa umma, Mzee Kassum aliweza kutunukiwa na Mtukufu Shah Karim al-Husayni, Mkuu wa Madhehebu ya Ismailia duniani, kuwa Vazir na mwakilishi wake nchini Tanzania. Aidha, baada ya kustaafu aliteuliwa kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine, Morogoro.


Miaka michache iliyopita, Mzee Kassum alianza kudhoofika kiafya, hasa kutokana na umri wake mkubwa, wa zaidi ya miaka 90. Mwezi Septemba 2018 tulipata nafasi ya kumtembelea nyumbani kwake kumjulia hali na kumpa pole. Mmoja wetu, Patrick Rutabanzibwa, alibahatika kumuona alipokuwa amelazwa katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam siku nne kabla hajaaga dunia, na kufikisha kwake salamu na shukrani za dhati kwa niaba ya watumishi wote aliowaongoza, kuwalea na kuwaendeleza katika kipindi chote alipokuwa kiongozi mkuu wa Wizara ya Maji, Nishati na Madini. Mzee alikuwa amedhoofika kiasi kwamba hakuweza kuongea, lakini tabasamu yake iliashiria kuwa ujumbe ulifika.


Pumzika kwa amani, Mzee Al Noor Kassum.


Sisi sote ni wa Mwenyezi Mungu, na hakika Kwake tutarejea.

*Patrick Rutabanzibwa amewahi kuwa Kamishna wa Nishati na Petroli, na Katibu Mkuu wa Wizara za Nishati na Madini; Maji na Umwagiliaji; Mambo ya Ndani ya Nchi; na Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi


**Prof. Mark Mwandosya amewahi kuwa Kamishna wa Nishati na Madini, Katibu Mkuu wa Wizara za Maji, Nishati na Madini; Nishati na Madini; na Viwanda na Biashara. Amewahi pia kuwa Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi; Maji na Umagiliaji; Maji; na Waziri wa Nchi (Mazingira), Ofisi ya Makamu wa Rais; na Waziri wa Nchi (Kazi Maalum), Ofisi ya Rais