Kwaheri Profesa Matthew Laban Pimpa Luhanga

Kwaheri Profesa Matthew Laban Pimpa Luhanga

Nimeombwa na familia ya Matthew Laban Pimpa Thompson Alfred Luhanga niongee machache kwa niaba yao kama njia ya kutoa shukrani kwa kadamnasi hii, na wote mliohusika kwa njia mbalimbali kuifariji familia katika kipindi hiki kigumu. Ni kweli nimeombwa lakini nami pia nilitaka iwe hivyo, ili nitumie nafasi hii, ukumbi huu, mahala hapa, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, niweze kumuaga ndugu na rafiki wa karibu, profesa mwenzangu wa teknolojia ya umeme, elektroniki na mawasiliano, mwanafunzi mwenzangu, mhandisi mwenzangu, mwandishi mwenzangu na jirani yangu. Nafanya hivyo pia kwa niaba ya familia yangu, mke wangu Lucy, vijana wetu: Max, Sekela na Emmanuel, na ukoo wote wa Mwandosya na wa Magombe, walio hai na waliotutangulia mbele ya haki.

Nimezoea kutoa mihadhara kama mwalimu hapa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na vyuo vikuu vingine. Kama mtumishi wa umma, nimehutubia mikutano mbalimbali, na maeneo mbali mbali, nchini na duniani kote. Nakiri kwamba hakuna uzoefu unaokutayarisha kutoa salaam za kuomboleza na kutoa shukrani, hasa pale ambapo anayekutoka alikuwa mtu wa karibu sana. Nitajitahidi, na nikiazima maneno ya Mark Anthony alipotoa salaam zake katika maziko ya Juliasi Kaisari, “Wanazuoni, ndugu zangu, naomba masikio yenu”, nikimaanisha, “naomba mnisikilize, mnivumilie”.

Aliyesoma wasifu wa Matthew amefanya kazi nzuri sana, na kwa umahiri mkubwa. Amenirahisishia kazi yangu. Amejibu swali kuu linaloulizwa na litaendelea kuulizwa, “Profesa Matthew Luhanga alikuwa nani hasa?”. Lakini wengi pia wameniuliza, “Profesa Mwandosya, ukaribu wako na Profesa Luhanga umeanzia wapi?” Maelezo yangu yatakuwa mafupi, na yatajikita katika yale mambo ambayo hayaandikwi katika wasifu, lakini ambayo kwayo yametufanya mimi na yeye, na familia zetu kuwa karibu. Ni mchanganyiko wa bahati, hatima na matukio ambayo sio rahisi kujua chanzo chake. Wakati mwingine nadiriki kusema yanatokana na sababuza kiroho zaidi.

Niliingia darasa la tisa (kidato cha kwanza) Shule ya Sekondari ya Serikali Malangali Januari mwaka 1965, wakati ule sisi wanafunzi wa kidato cha kwanza tukiitwa ‘Mugya’. Hapo nilimkuta Matthew akiwa darasa la 10 (kidato cha pili). Hawa vijana wa kidato cha pili walituendesha vilivyo, mithili ya magaidi. Hata hivyo Matthew alikuwa mstaarabu katika kundi hilo. Tukajenga urafiki kwa sababu mbili. Mosi, wote tulikuwa tunatoka Mbeya Mjini, na pili tulikuwa na uwezo mkubwa wa masomo yote, ikiwa ni pamoja na hisabati. Kuhusu hisabati, mimi na yeye tulikuwa tunawasaidia wanafunzi wa kidato cha tatu katika somo la hilo, ikiwa ni pamoja na somo la hisabati ziada (additional mathematics).

Mwaka juzi, Mwalimu Ambangile Mwakilembe, Mwalimu Charles Muhitira, na Mwalimu Clement Bendera walikuja kunitembelea kijijini, Lufilyo, Busokelo, kuhudhuria kumbukumbu ya miaka 70 ya kuzaliwa kwangu. Mwalimu Mwakilembw Akatukumbusha jinsi Matthew na mimi tulivyoweza kugundua makosa katika kitabu maarufu cha hisabati cha Durell, jambo ambalo lilipelekea masahihisho yafanywe katika makala zilizofuata. Nakumbuka siku moja, Matthew akiwa kidato cha nne na mimi cha tatu, Mwalimu Mkuu, Alexander Thobias Mabele, marehemu baba ya mwenzetu Profesa Robert Mabele (ambaye naye ni marehemu. Mwenyezi Mungu awarehemu), aliitisha mkutuno wa wanafunzi na walimu. Akasema alikuwa na neno moja tu, nalo ni kwamba Malangali ilikuwa na bahati ya kuwa na wanafunzi wawili wenye vipaji vya hali ya juu. Kila mtu akatega masikio Mwalimu Mabele atasema nini. “Na wanafunzi hao ni Matthew Luhanga na Mark Mwandosya”. Akafunga mkutano, akaondoka, akituacha na butwaa. Lakini mimi nilihisi alimlenga zaidi Matthew.

Alipomaliza kidato cha nne, Matthew akachaguliwa kwenda Chuo cha Ufundi cha Dar es Salaam (DarTech) ili yeye na wenzake waanzishe kidato cha tano, mchepuo wa Hisabati, Hisabati, Fizikia (Pure Mathematics, Applied Mathematics, Physics-PMM), mchepuo ambao ulilenga katika kutayarisha vijana kwenda vyuo vikuu kusomea uhandisi. Nilimkuta Matthew DarTech mwaka 1969 nilipochaguliwa kuingia hapo kuchukua mchepuo huo wa PMM. Alipomaliza kidato cha sita, Matthew alijiunga na Chuo Kikuu cha California Polytechnic (California State Polytechnic University, Pomona, California) kusomea shahada ya kwanza ya uhandisi umeme, na elektroniki na akufuzu kwa kiwango cha juu (suma cum laude). Akaendelea hapo hapo na kupata shahada ya uzamili. Nami nilipohitimu kidato cha sita, nikapata udhamini wa kwenda kusomea uhandisi umeme Chuo Kikuu cha Aston, Uingereza. Nilipofuzu na kupata shahada ya kwanza daraja la kwanza (first class honours), nikaenda Chuo Kikuu cha Birmingham moja kwa moja kufanya utafiti na kuhitimu shahada ya uzamifu katika fani ya umeme na teknolojia ya elektroniki baada ya miaka miwili na nusu.

Aliporudi kutoka Marekani, Matthew akawa mkufunzi DarTech, kama sharti la ufadhili wake kwenda Marekani lilivyomtaka. Nami nilipomaliza masomo yangu nikaja kuwa mhadhiri, idara ya umeme, kitivo cha uhandisi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Akiwa Dar Tech, na mimi nikiwa UDSM, mimi na Lucy tulipofunga ndoa, Matthew na mkewe Stephania (sasa ni marehemu na apumzike kwa amani) ndio waliosimamia ndoa yetu. Enzi hizo hatukuwa gari. Tulipanda magari ya Usafiri Dar es Salaam (UDA) kwenda kufunga ndoa. Baada yaho apo tukachukua UDA tena kwenda kwa akina Matthew an Stephania hapo DarTech kwa ajili ya chakula cha mchana. Baadaye sisi tukarudi Barabara ya Kileleni, nyumba namba 25, Chuo Kikuu cha Dar es Saam. Gharama za harusi hazikuzidi shilingi mia tano.

Ilikuwaje Matthew akaja kuwa mhadhiri, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam? Kuna wakati nilikaimu kama Mkuu wa Idara ya Umeme, Kitivo cha Uhandisi hapa UDSM. Moja ya majukumu nyangu ilikuwa ni kutafuta na kuwashawishi watanzania wenye uwezo wajiunge na Idara kama wahadhiri. Nilipomshauri Matthew ajiunge nasi, na alipokubali, ndipo nilipomuendea Profesa Awadhi Sadiki Mawenya, aliyekuwa Mtanzania wa kwanza kuwa Mkuu wa Kitivo Cha Uhandisi, kumwomba akubali tuanze mchakato wa kumhamsha Matthew kutoka DarTech kuja UDSM. Profesa Mawenya akakubali kuchukua jukumu hilo na akaomba ridhaa ya Ndugu Ibrahim Kaduma, aliyekuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Naye akakubali. Wizara ya Elimu walionesha ugumu kumruhusu ahamie Chuo Kikuu. Nikachukua jukumu la kumwona aliyekuwa Waziri wa Elimu, nadhani alikuwa Mheshimiwa Nicholas Kuhanga. Waziri akamuagiza Katibu Mkuu atoe kibali husika mara moja. Na kama wahenga walivyosema, yaliyofuata sasa ni historia.

Baaba ya Malangali na DarTech kama wanafunzi, tukaja kukutana Uhandisi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kama wahadhiri. Tukakutana tena Marekani mwaka 1983, yeye akiwa Chuo Kikuu cha Columbia, New York, akisomea shahada ya uzamivu, na mimi nikiwa likizo ya sabato (sabathical leave), Chuo Kikuu cha Princeton, New Jersey. Tuliporudi kutoka Marekani, baada ya muda mfupi mimi nikateuliwa kuwa Kamishna wa Nishati na Petroli, baadaye Katibu Mkuu, halafu Waziri katika Wizara mbalimbali, na hatimaye Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Technolojia Mbeya kama mwanzilishi. Yeye akaendelea na utumishi wa Chuo KIkuu na akateuliwa kuwa Afisa Mkuu Taaluma na baadaye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Tukiwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na hata baada ya mimi kuazimwa na hatimaye kuhamia serikalini, kwa pamoja tumetoa maandiko kadhaa yaliyochapishwa katika majarida ya kutaaluma humu nchini na nje ya nchi. Nilikuwa napitia wasifu wake nikaona ana machapisho zaidi ya 75 na vitabu nane. Vinne kati ya hivyo nane tumeandika pamoja katika fani za uhandisi, nishati na mazingira, hususan mabadiliko ya tabianchi. Suala la mabadiliko ya tabianchi sasa linazungumzwa sana duniani. Matthew na mimi tulilifanyia utafiti miaka 25 iliyopita!

Matthew na mimi tulianza uandishi wa pamoja zamani kidogo, tukiwa wanafunzi wa sekondari. Mwaka 1970 tuliandika makala kuhusu umuhimu wa Tanzania kuwa na wahandisi wanawake. Makala hiyo ilichapishwa katika gazeti la kila siku la serikali, The Standard, Tanzania, toleo Namba 12, 344, chini ya kichwa, Why No Women Engineers?’ Makala hiyo, iliyotoka tarehe 10 Julai 1970, na ikawa ni makala bora ya wiki, na tukapata zawadi ya shilingi 20. Chapisho letu la pamoja la mwisho limetoka miezi michacte tu iliyopita. Yeye na mimi tukiwa waandishi wenza, tumechapisha andiko kuhusu, “Blockchain: A Disruptive and Transformative Technology of the Fourth Industrial Revolution”, andiko ambalo limo katika jarida la kitaaluma la Shule ya Biashara, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (University of Dares Salaam Business Management Review).

Profesa Luhanga ndiye aliyeishauri Idara ya Umeme, Kitivo cha Uhandisi ianzishe Kigoda cha Uprofesa/Kiprofesa cha Usimamizi wa Nishati na Teknolojia (Professorial Research Chair in Energy Technology and Management), Kigoda cha kwanza kuanzishwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Kigoda ambacho nilibahatika kuwa profesa wa kwanza kukikalia. Kilipoanzishwa kigoda cha teknolojia na usimamizi wa mawasiliano, Profesa Luhanga akawa profesa wa kwanza kigoda hicho.

Profesa Luhanga ndiye aliyewezesha kupatikana kwa eneo linalotumika na Chuo cha Teknolojia za Habari na Mawasiliano cha UDSM, kilicho pale Kijitonyama, baada ya Mark Mwandosya, aliyekuwa Waziri mwenye dhamana ya sekta ya mawasiliano, kumshauri aiombe serikali ili Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kipewe eneo hilo, majengo yaliyokuwepo na miundombinu yake.

Lakini Profesa Luhanga atakumbukwa zaidi kwa kubuni na kutekeleza kimkakati, na kwa ufanisi mkubwa, Programu wa Mageuzi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (University of Dar es Salaam Institutional Transformation Programme). Programu hiyo iliongeza ufanisi katika utendaji kazi, ilipanua wigo na kuongeza udahili wa wanafunzi. Ilileta matumizi bora ya majengo na kuongeza miondombinu; na ilifanikiwa kuleta uwiano mzuri wa kijinsia katika udahili. Wote tumeshuhudia matokeo chanya ya mabadiliko hayo.

Moja ya mambo ambayo hayajulikani sana ni kwamba Profesa Luhanga, Profesa Mawenya, Ndugu Enock Kamuzora, Mhandisi Ladislaus Salema, Ndugu Ibrahim Kaduma na sisi wengine, tulikuwa waanzilishi wa kikundi cha kubuni mbinu na mikakati ya kuzuia rushwa katika sekta ya uhandisi, na hasa katika ujenzi (FACEIT-Front Against Corruption in Engineering in Tanzania). Hii ilikuwa hata kaba ya Tume ya Warioba.

Mambo mengine yalikuwa si rahisi kuyaelewa yalivyotokea. Baruany Elijah Luhanga, kaka yake Matthew, ambaye alituchemsha sana tukiwa ’mugya’ Malangali, ndiye aliyenikaribisha Uingereza akiwa Mwanafunzi wa uhandisi wa elektroniki Chuo Kikuu cha Liverpool, Uingereza, mimi nilipokwenda Aston. Tukaja kukutana tena yeye akiwa Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, mimi nikiwa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, wizara iliyokuwa na jukumu la kuisimamia TANESCO. Jambo ambalo lilistaajabisha familia zetu ni pale ambapo mama yao akina Luhanga Mama Edith Talina Nyamkandawire, na baba yetu sisi, Mzee Isaac Mwandosya, walipofariki siku moja hapa Dar bes Salaam mwaka 1995. Tukawa na misiba miwili na misafara miwili ya kwenda kuzika huko Mbeya.

Nilipokuwa nafundisha Control Theory EE441 hapa Chuo Kikuu, kipindi hicho kilikuwa cha dakika 50. Ikifika dakika 40 baadhi ya wanafunzi walikuwa wanaanza kupiga miayo. Nikiwauliza, “Kwanini?” Wanasema, “Njaa Profesa”. Nisingependa baadhi yenu muanze kupiga miayo.

Hivyo basi, nimalizie kama nilivyoanza, na kama nilivyoombwa, kwa kuwashukuru wote mliokuja kumsindikiza ndugu yetu Profesa Matthew Luhanga, au, Uncle Matthew, kama watoto wetu wanavyomfahamu. Tunawashukuru madaktari, wauguzi na wengine waliomhudumia Uncle Matthew hapa nchini na huko India.

Tunanatumbua na kuheshimu uwepo kati yetu wa uwakilishi kutoka serikalini. Tunamshukuru Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ambaye amewakilishwa na Profesa Kitia Mkumbo, profesa mwenzetu na Waziri wa Viwanda na Biashara. Uwepo wa Profesa James Mdoe kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia umetupa faraja.

Tunawashukuru: Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Jaji (Mstaafu) Damian Lubuva, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam; Profesa William Anangisye, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam; Ndugu Nicholas Kuhanga, ambaye amewahi kuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam; Profesa Rwekaza Mukandala, aliyechukua nafasi ya Profesa Luhanga kama Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam; na uongozi wote na jumuiya ya Chuo Kikuu kwa kumuaga Profesa Luhanga kwa heshima anayostahili.

Tunawashukuru pia Chuo Kikuu cha Mzumbe, ambako Matthew alikuwa Mwenyekiti wa Baraza. Chuo hicho kimemuaga Profesa Luhanga vilivyo. Tunamshukuru Mheshimiwa Dk. Ali Mohamed Shein, Mkuu wa Chuo, Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, na Makamu wa Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nilibahatika kufanya kazi chini yake nikiwa Waziri wa Nchi (Mazingira), Ofisi ya Makamu wa Rais; Mheshimiwa Jaji Mkuu Mstaafe Barnabas Samatta, liyekuwa Mkuu wa Chuo Kikuu. Profesa Lughano Kusiluka, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu, na jumuiya yote ya Chuo Kikuu Mzumbe. Chuo Kikuu Mzumbe, tunawashukuru sana kwa kuchangia jeneza, gharama za kaburi na nyinginezo.

Tunatambua pia uwepo wa Mheshimiwa Joseph Sinde Warioba, Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; na ule wa Profesa Anna Tibaijuka, aliyekuwa mbunge mwenzangu na Waziri mwenzangu, ambaye amewahi pia kuwa Mkuu wa Shirika la Makaazi la Umoja wa Mataifa (HABITAT).

Mwisho, lakini sio kwa umuhimu, tunamshukuru Baba Padri Daktari Joseph Mosha, Baba Paroko wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam; Baba Thomas Kilewona, Paroko Msaudizi wa Parokia ya Mtakatifu Andrea Mtume Bahari Beach; Baba Timotheo Polepole, Paroko wa Parokia ya Bikira Maria wa Rozari Takatifu, Chunya Mjini; na kwaya na wanaparokia wote kwa kuongoza na kuendesha sala na misa takatifu ya maziko ya Profesa Luhanga. Asanteni sana.

Tunawashukuru pia Chuo Kikuu cha Ardhi, Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili, Bodi ya Usajili wa Wahandisi (Engineers Registration Board), Chama cha Wanasayansi Tanzania (Tanzania Academy of Sciences), na Huduma za Maktaba Tanzania (Tanzania Library Services).

Tunazishukuru taasisi na wale wote mliochangia kwa hali na mali katika msiba huu ambao hatima yake ni maziko ya yule ambaye wenzetu wa Kenya wanamwita ‘Mwendazake’, yatakayofanyika kesho Jumanne tarehe 21 Septemba 2021 katika makaburi ya Kondo, Tegeta.

Profesa Luhanga ameacha mke, Columba Namkamba, na watoto watatu; Edith, Thompson na Jeremiah. Ameacha pia wajukuu wawili; Miriam na Abigaeli. Aidha Matthew na familia yake wamelea watoto na wajukuu wengi wa ndugu zao.

Sisi tumekuwa majirani na familia ya Matthew pale Tegeta/Bahari Beach kwa zaidi ya miaka 25. Ndugu Kadenge, aliyekuwa mhudumu wa familia yangu, akimwona Profesa Luhanga anaingia nyumbani kwake alikuwa ananitaarifu, “Profesa Luhanga amerudi. Ameingia nyumbani na madigrii yake”, akimaanisha amebeba vitabu. Watoto na wajukuu yatumieni madigrii ya Profesa Luhanga.

Hatujaja kumlilia Matthew. Hapana. Tunasherehekea maisha ya mtu mwenye kipaji na uwezo mkubwa, aliyekuwa mcheshi na mpenda watu, aliyejaliwa busara, hekima na nidhamu ya hali ya juu, na mzalendo aliyetoa mchango mkubwa kitaaluma na katika maendeleo ya elimu.

Nahitimisha kwa kusema kwamba pamoja na sifa zote hizo, Profesa Luhanga alikuwa binadamu wa kawaida tu, kama tulivyo sisi wengine. Lazima katika maisha yake amewakwaza na kuwaudhi baadhi yenu. Kwa hayo yote tunawaomba, tena kwa heshima kubwa, mumsamehe.

Raha ya Milele Umpe Ee Bwana, na Mwanga wa Milele Umwangazie. Apumzike kwa Amani.

Asanteni sana. Mbarikiwe sana.


Mark Mwandosya

Jumanne 21 Septemba 2021