Salaam Kutoka Fort Portal

Salaam Kutoka Fort Portal, Tooro, Uganda


Utangulizi


Kuielezea Uganda ni sawa na kurudi miaka mingi nyuma tulipojifunza jiografia ya Afrika ya Mashariki tukiwa shuleni. Lakini Uganda ni moja ya nchi tatu zilizoanzisha iliyokuwa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki mwaka 1967 (East African Community), iliyovunjika mwaka 1977. Katika makubaliano yaliyoanzisha Jumuiya hiyo iliyovunjika, ili kuleta uwiano katika kusimamia maendeleo, taasisi za jumuiya ziligawanywa ili kila nchi baina ya Kenya, Tanzania, na Uganda kila moja ya nchi hizi iwe mwenyeji wa makao makuu ya taasisi hizo. Kwa mfano; makao makuu ya Shirika la Posta na Simu yalikuwa Kampala, makao makuu ya Taasisi ya Takwimu yalikuwa Kampala, makao makuu ya Benki ya Maendeleo ya Afrika ya Mashariki yalikuwa Kampala na Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi ilikuwa Jinja. Uganda pia ilikuwa mwenyeji wa shule ya kujifunza urubani, Soroti. Kenya ilikuwa mwenyeji wa makao makuu ya Shirika la Ndege la Afrika ya Mashariki, na Shirika la Reli la Afrika ya Mashariki. Makao makuu ya Shirika la Bandari yalikuwa Dar es Salaam, Chuo cha Takwimu cha Afrika ya Mashariki kilikuwa Dar es Salaam, na Bunge la Afrika ya Mashariki lilikuwa Arusha. Taasisi za kiutafiti nazo ziligawanywa kufuatana na mazingira na uhalisia wa madhumuni ya taasisi hizo.


Baaada ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki mwaka 1977, kukatokea sintofahamu baina ya nchi hizi tatu, kiuchumi na kisiasa. Uhasama huu hakika haukuwa kwa manufaa ya wananchi wa nchi hizi tatu ambao baada ya uhuru na baada ya kuanzishwa kwa Jumuiya walikuwa wakijitambua kama wananchi wa Afrika ya Mashariki. Kipindi hiki kigumu kilipelekea viongozi wa wakati ule, kwa ushawishi wa Benki ya Dunia, kukubaliana kuwa na msuluhishi huru, Victor Hermann Umbricht, mwanasheria na mwanadiplomasia, raia wa Uswisi, ambaye angesimamia ugawaji wa mali na madeni ya Jumuiya iliyovunjika. Suluhu ilipatikana mwaka 1984 na ikaleta hali ya utulivu katika ushirikiano wa nchi za Afrika ya Mashariki.


Hali hii ya utulivu ndio iliyozaa matunda ya ushirikiano kuanza upya kupitia Mkataba wa kuanzishwa kwa Jumuiya mpya ya Afrika ya Mashariki, Mkataba uliotiwa saini mjini Arusha na Rais Daniel arap Moi wa Kenya, Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda na Rais Benjamin Wiliam Mkapa wa Tanzania. Jumuiya iliyovunjika ilijijengwa katika msingi wa maendeleo ya miundombinu ya pamoja na taasisi za pamoja. Jumuiya mpya ya Afrika ya Mashariki imejikita katika kukuza biashara na kutambua nafasi ya sekta binafsi katika kuleta maendeleo. Katika kutekeleza madhumuni hayo ushirikiano baina ya nchi hizi unatekelezwa katika hatua tatu: Umoja wa Forodha; Soko la Pamoja; Umoja wa Sarafu; na hatimaye umoja wa kisiasa. Jumuiya ya Afrika ya Mashariki imekua baada ya Burundi, Rwanda na Sudan ya Kusini kujiunga.


Mbali na mandhali na hali ya hewa nzuri, Uganda ina historia iliyosheheni matukio muhimu. Baadhi ya matukio hayo ni pamoja na yafuatayo: Uganda ni nchi iliyo na watakatifu wengi wa Kanisa Katoliki kuliko nchi nyingine Afrika wanaotokana na mashahidi waliouawa wakitetea imani. Mwanzoni mwa karne ya ishirini, jumuiya ya kimataifa ilipoamua kuwatafutia Wayahudi mahali ya kuhamia na kuishi, Uganda ilipendekezwa. Hata hivyo pendekezo hilo halikukubaliwa na Wayahudi. Chuo cha Makerere kilikuwa moja ya vyuo vya kwanza Afrika kutoa elimu ya juu.


Mwezi Agosti 1972 Idi Amin aliwafukuza jamii ya waasia wa Uganda baada ya kuwapa amri ya kuondoka katika kipindi kisichozidi siku 90. Waganda hao wapatao 80,000 baadaye wengi wao wakaishia uhamishoni Uingereza na Canada. Idi Amin alikuwa kiongozi wa kwanza kuanzisha vita katika Afrika ya Mahariki alipovamia eneo la Kagera mwaka 1978. Akashindwa vita mwaka 1979 na kukimbilia uhamishoni Saudi Arabia ambako aliishi mpaka alipofariki dunia mjini Jeddah tarehe 16 Agosti 2003.


Yaliyotangulia yanaweka muktadha wa waraka huu. Kwani amani, usalama, utulivu, ujirani mwema na ushirikiano baina ya nchi za Afrika ya Mashariki umewezesha wananchi wa nchi hizi kufanya biashara kwa urahisi na kusafiri kwa urahisi.


Ufalme wa Tooro


Fort Portal ni mji mkuu wa Ufalme wa Tooro. Ufalme huu ni moja kati ya falme za kijadi za Buganda; Bunyoro; Tooro, Ankole; Busoga, and Acholi. Ufalme wa jadi wa Tooro sasa umegawanyika katika sehemu tatu: Tooro, ikiongozwa na Omukama, mji mkuu ukiwa Fort Portal: Rwenzururu, ikiongozwa na Omusinga, mji mkuu ukiwa Kasese; na Bwamba, ikiongozwa na Omudingiya, mji mkuu ukiwa Bundibugyo.


Kwa mujibu wa historia, Ufalme wa Tooro ulikuwa sehemu ya himaya ya Bunyoro-Kitara ambayo ilitawala eneo lote la kaskazini magharibi, magharibi, na kusini mwa Uganda, Rwanda, mpaka Kagera, kaskazini magharibi mwa Tanganyika (Tanzania), na Congo (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo), magharibi na kaskazini mwa Mto Semliki, kuanzia karne ya 16 mpaka karne ya 19. Himaya ya Bunyoro-Kitara ilihusisha Bunyoro, Tooro, Ankole, mpaka Kiziba, Bukoba. Mfalme wa Bunyoro-Kitara alitawala pia Busoga, Lango, Teso, Acholi, Madi, Aruru, na Bukonjo.


Mwaka 1830, mwana wa kwanza wa Omukama(Mfalame) Nyamutukura Kyebambe III wa Bunyoro-Kitara, aliamua kuhama na kuchukua eneo la Tooro na kujitangaza kuwa mfalme wa kwanza Rukirabasaija Omuhundwa Kasusunkwanzi Kaboyo Olimi I, Omukama wa Tooro. Baada ya kifo cha baba yake huko Bunyoro, aliitwa ili achukue nafasi ya ufalme, akakataa. Kaboyo Olimi I alipofariki, mwanae Omubiito Kazaana Ruhaga akarithi ufalme kwa muda mfupi mpaka alipopinduliwa na kaka yake ambaye akajitawaza kama Mfalme (Omukama) Nyaika Kasunga. Utawala wa Mfalme Kasunga nao ulikatishwa pale alipopinduliwa na ndugu yake Mwana wa Mfalme Kato Rukidi ambaye katika mapinduzi hayo alisaidiwa na jeshi kutoka Ufalme wa Buganda. Nyaika Kasunga alikimbilia uhamishoni eneo la Mboga. Hata hivyo alipopata habari kwamba wanajeshi wa Buganda wamerudi kwao, naye akavamia Tooro na kumpindua Kato Rukidi na kujitawaza tena kuwa Mfalme. Baada ya kifo cha Nyaika Kasunga, mwanae Mukabirere Olimi II akarithi ufalme. Katika utawala wake kulitokea migogoro mingi ikiwa ni pamoja na ndugu yake, Mukarusa kunyakua eneo la Busongora. Mwaka 1876 ufalme wa Tooro ulirudi kwenye himaya ya Bunyoro-Kitara baada ya Omukama Kabalega kumshinda katika vita na kumteka Omukama Olimi II. Mwezi Agosti mwaka 1891 Tooro ilirudi kuwa ufalme kamili tena chini ya Omukama Daudi Kyebambe Kasagama, baada ya Mfalme Kabalega kushindwa katika vita ambapo wapiganaji wa Tooro walisaidiwa wa Luteni Lugard na kikosi cha askari wa Kinubi ambao ndio chanzo cha jamii ya wanubi iliyo Fort Portal mpaka sasa. Baada ya kufariki Omukama Kyebambe Kasagama, mwanae akatawazwa kuwa Omukama George Karamusi Rukidi III mwezi Januari 1929.


Omukama Rukidi III ndiye aliyekuwa baba wa Omubiito Patrick Kaboyo, ambaye baada ya kifo cha baba yake, 21 Desemba 1965, akatawazwa kuwa Mfalme wa Tooro, Omukama Patrick Matthew Kaboyo Olimi VII. Utawala wake haukudumu muda mrefu. Kwani tarehe 8 Septemba 1967 Apollo Milton Obote akabadilisha katiba ya Uganda, akafuta utawala wa kifalme, na Uganda ikawa Jamhuri. Mwaka 1971 yalitokea mapinduzi ya kijeshi nchini Uganda yaliyoongozwa na Idi Amin Dada. Mwaka 1979 Idi Amin Dada aliivamia Tanzania na kutangaza sehemu ya Kagera kuwa sehemu ya Uganda. Majeshi ya Tanzania yakajibu uvamizi huo kwa kuwafukuza wanajeshi wa Uganda mpaka Uganda na kuuondoa utawala wa Idi Amin ambaye akakimbilia na hatimaye kufia uhamishoni Saudi Arabia.


Baada ya vita vya Tanzania na Uganda hakukuwa na maelewano baina ya makundi mbalimbali ya Uganda kiasi cha kwamba viongozi wafuatao walitawala: Profesa Lule, Geoffrey Binaisa, Milton Obote aliyerudi kuwa kiongozi kwa mara ya pili, na Tito Okello. Baadhi ya wananchi wa Uganda ambao hawakuridhika na jinsi nchi ilivyokuwa ikiongozwa walianzisha vita vya msituni mwaka 1981 wakiongozwa na Yoweri Kaguta Museveni. Akiongoza Vuguvugu la Kitaifa (National Resistance Movement- NRM), Januari 1986 Museveni alifanikiwa kuuondoa madarakani uongozi wa Tito Lutwa Okello ambaye Julai 1985 aliongoza mapinduzi dhidi ya Milton Obote ambaye hatimaye alienda uhamishoni Lusaka, Zambia. Mwaka 1993, Museveni alirejesha upya utawala uliojikita zaidi katika utamaduni na jadi kupitia zilizokuwa falme za Buganda, Tooro, Bunyoro, na Busoga, na kuelekeza utawala huo ujikite zaidi kwenye misingi ya kitamaduni kuliko utawala. Ndipo Omukama Kaboyo Olimi VII akarudi tena kuwa Mfalme wa Tooro.


Omukama Patrick Matthew Kaboyo Olimi VII

Babu na baba ya Kaboyo Olimi walikuwa ni wafalme wenye upeo wa mbali na ambao walithamini sana elimu ya watu wao. Upeo huu ndio uliomfanya Omukama Rukidi III kuwapeleka watoto wake shule. Mmoja wao, Elizabeth Bagaya, dada yake Kaboyo Olimi alikuwa mmoja wa wanafunzi wa kike wa mwanzo wenye asili ya kiafrika kusoma, kuhitimu na kupata shahada kutoka Chuo Kikuu maarufu cha Cambridge, Uingereza. Kabla ya Museveni kurudisha utawala wa kifalme Uganda, Kaboyo Olimi aliwahi kuwa Balozi wa Uganda nchini Tanzania (1987-1990) na Cuba (1990-1993).




Balozi Kaboyo Olimi, kulia, akiwa na Balozi George Magombe, katikati, na Best Kemigisa, Mke wa Balozi Olimi, wakiwa nyumbani kwa Lucy na Mark Mwandosya, Ada Estate, Dar es Salaam

Akiwa Tanzania alikuwa karibu sana na familia ya Mwandosya. Balozi Kaboyo Olimi alikuwa mtu wa kawaida sana, anayependa watu. Alikuwa hana ubaguzi wa rika au nafasi ya mtu katika jamii. Alikuwa mcheshi na anayependa mazungumzo. Hakukalia kiti cha mfalme wa Tooro kwa muda mrefu. Kwani mauti ilimpata tarehe 26 Agosti 1995. Mwenyezi Mungu airehemu roho yake na apumzike kwa amani milele. Mrithi wake ni Omukama Oyo Nyimba Kabamba Iguru Rukidi IV, ambaye wakati anarithi alikuwa na umri wa miaka mitatu na nusu, akiwa ni mfalme mwenye umri mdogo zaidi duniani. Watu watatu waliteuliwa kutawala kwa niaba ya Omukama Oyo mpaka afikie umri wa miaka 18. Waliochaguliwa kuwa walezi wake walikuwa Rais Museveni; mjomba wake, Omubiito James Mugenyi; shangazi yake, Omubiitokati Elizabeth Bagaya, na Wafalme wengine wa Uganda.

Kutoka Kampala kwenda Fort Portal


Muyenga ni moja ya viunga vizuri vya jiji la Kampala. Kama ilivyo sehemu nyingi za Kampala, Muyenga iko katika moja ya vilima ambavyo kwa pamoja ndio jiji la Kampala. Miongo mitano iliyopita Kampala ilikuwa ni muunganiko wa vilima saba, kama ilivyo Roma, Italia. Kwa kawaida miji iliyo kwenye vilima, ikipangwa vizuri, inapendeza na kuvutia. Ndivyo ilivyokuwa Kampala ya zamani. Hivi sasa Kampala ni muunganiko wa vilima zaidi ya kumi, na kama ilivyo katika miji mingi ya nchi zinazoendelea, mipango miji inafuata wananchi badala ya wananchi kujenga kufuatana na mipango miji.


Ili kuifikia barabara iendayo Mityana na ambayo hatimaye inakufikisha Fort Portal, inabidi uchukue mojawapo ya mizunguko ifuatayo: Muyenga-Kabalagala-Nsambya-Makindye-Kibuye-Ndeeba-Nateete hadi Busega; au Muyenga-Kabalagala-Nsambya- Clock Tower-Kibuye-Ndeeba-Nateete hadi Busega. Njia ya kwanza ni ndefu ina kona na mizunguko mingi, lakini inapitika kwa urahisi. Njia ya pili, kupitia Clock Tower ni fupi na ya moja kwa moja kufika Busega. Hata hivyo kwa miji kama Kampala na Dar es Salaam ufupi wa barabara hauna uhusiano na muda wa safari. Kwani ukidhani kuna taizo la misururu ya magari ambayo yanaenda mwendo wa kinyonga, basi unakuwa hujafika Kampala. Mwendo wa kilomita moja unaweza ukachukua saa mbili na zaidi!


Msongamano wa magari Kampala

Barabara ya Mityana inaanzia Busega, kupitia Bulenga, Buloba, Bujuuko, Zigoti hadi Mityana. Kutoka Mityana unaenda Myanzi, Kawungera, Kitenga hadi Mubende. Kutoka Mubende unaingia Nabingora, Kyegegwa, Kakabara, Humura, na hatimaye Kyenjojo. Kyenjojo ndipo ilipo njia panda ya kwenda Hoima, mji ambao umepata umaarufu kutokana na kugunduliwa kwa mafuta katika Ziwa Albert. Hapo ndipo litakapoanzia bomba la mafuta kutoka Uganda kuja Tanzania, likiishia bandari ya Tanga, kwa ajili ya kusafirishwa nje.


Uganda hakika ni nchi iliyopendelewa na Mwenyezi Mungu, kwa maana ya tabianchi, hali ya hewa na rutuba. Msafiri yeyote atokaye Kampala mpaka Fort Portal anaweza kuthibitisha. Kwani utadhani uko katika mkoa wa Mbeya, Tanzania, isipokuwa eneo la Mbeya linalofanana na Uganda ni dogo. Eneo lote kutoka Kyenjojo mpaka Fort Portal ni sawa na kufika Wilaya ya Rungwe. Siku zote nimeisifia sana Rungwe. Nikiulizwa Rungwe kukoje huko? Nawambia watu Rungwe ni zawadi ya Mwenyezi Mungu kwa Tanzania. Kusisitiza uzuri wa Rungwe huwa naeleza kuwa Msaafu Mtakatifu unaeleza kwamba Mwenyezi Mungu alitumia siku sita kuumba ulimwengu. Siku ya saba akapumzika. Imani yangu ni kwamba aliiumba Rungwe siku ya nane, alikuwa ametulia na akaona mapungufu ya maeneo mengine na ndio maana Rungwe na Busokelo zinavyopendeza kwa mandhari, mazingira, hali ya hewa, rutuba na ukarimu wa wenyeji wake. Hata hivyo, nilipofika Tooro kwa mara ya kwanza mwaka 1985 nikakubali kwamba eneo hilo nalo liliumbwa siku ya nane.


Soko la ndizi Fort Portal

Unaposafiri kutoka Kyegegwa kwenda Fort Portal, kilomita tano ni kituo kidogo cha biashara kinachojulikana kama Kakabara. Mwanzoni mwa karne ya ishirini, eneo hilo lilikuwa sehemu ya Kaunti ya Kyaka, iliyokuwa ikiongozwa na Chifu Noah Bwabashaija. Yeye ndiye aliyekuwa baba mzazi wa Susana Bonabana Adyeri (Mwenyezi Mungu Airehemu Roho Yake). Adyeri alikuwa mama Mzazi wa: Nesta Abwooli, Emmanuel Kahigwa Apuuli (Mwenyezi Mungu Airehemu Roho Yake); Bessie Adyeri; Margaret Mbabazi Amooti; na Lucy Akiiki Mwandosya na Mama mkwe wa Mwandishi wa Waraka huu. Susana Adyeri alizaliwa eneo hilo la Kakabara tarehe 18 Novemba 1911 na mauti ikampata tarehe 5 Novemba 2006 akiwa na umri wa miaka 95.


Baada ya Kakabara unafika Humura na Kyenjojo, makao makuu Wilaya Kyenjojo. Baada hapo unaingia Butiiti, Rugombe, na hatimaye kituo cha biashara kinachoitwa Kagorogoro, eneo la Mwenge. Mzee Sepiriya Kahigwa Abooki alihamia Mwenge kutoka Ibonde, karibu na safu za milima ya Rwenzori ili apate eneo kubwa zaidi kwa ajili ya mifugo. Baadaye akaja kuwa mmoja ya wafanyabiashara mashuhuri wazalendo wakati wa ukoloni, akishindana wa wafanyabiashara wa asili ya kiasia. Mzee Kahigwa (Mwenyezi Mungu Airehemu Roho Yake) ndiye aliyekuwa baba mzazi wa Emmanuel Kahigwa, Bessie, Margaret, na Lucy Mwandosya, na Baba mkwe wa Mwandishi wa Waraka huu, na babu yao akina Max, Sekela, na Emmanuel. Kutokana na rekodi alizoziacha Mzee Kahigwa, Baba ya babu yake alikuwa karibu sana na Kaboyo Olimi I, Omukama wa kwanza wa Ufalme wa Tooro. Kwani alikuwa mmoja ya wale walio ongozana na Kaboyo Olimi I alipohamia Tooro kutoka Bunyoro, na kuishi eneo la Ibonde.


Ukitoka Kagorogoro, kuelekea Fort Portal, baada ya kilomita 5 hivi unakutana na Msitu wa Kibale ambao ni sehemu ya Hifadhi ya Taifa ya Kibale. Barabara inapita msituni kwa umbali wa km 6. Hii ni sehemu ya kaskazini ya Msitu na Hifadhi ya Taifa. Ni msitu weye mvua kipindi kirefu cha mwaka. Msitu huo kwa ujumla wake kutoka kaskazini mpaka kusini una eneo la km za mraba 766. Ni msitu wenye uoto mkubwa wa asili na uko kijani mwaka mzima. Msitu na Hifadhi hii inaendelea kusini na kuungana na Hifadhi ya Taifa ya Malkia Elizabeth. Wanyama wengi katika Hifadhi ya Kibale ni sokwe, tumbili, nyani, kima na ngedere. Tembo ni mnyama ambaye ni rahisi sana kumwona katika msitu huu.




Msitu wa Kibale

Baada ya msitu huo mashamba ya chai ya eneo la Sebitoli yameshamiri na yanaangaliwa vizuri kuliko mashamba ya Rungwe. Idi Amin lipowafukuza wananchi wa asili ya kiasia, mashamba yote yaligeuka kuwa mapori ya miti mikubwa ya chai. Tulishuhudia hili tulipotembelea Uganda na kufika Fort Portal mwaka 1985. Museveni alipoingia madarakani mwaka 1986 akawarudishia mashamba yao wale walioweza kurudi na kuyaendeleza. Mmoja wa waganda hao maarufu ni Alykhan Karmali na familia yake, ambao kampuni yao ya Mukwano imewekeza katika mashamba ya chai, viwanda, na benki.

Mashamba ya Chai ya Kampuni ya Mukwano

Ukitoka Sebitoli unaingia miji midogo ya Kyakatimba, Mukaswa, Buzira Sagama, Busoro, Kitumba, na Hakabale unafika katikati ya Manispaa ya Fort Portal. Mji ulipangwa ufuate barabara ya Fort Portal-Kasese, na barabara nyingine na mitaa ikiungana na barabara ya Kasese. Barabara hizi kubwa za lami ni pamoja na ile inayokwenda Bundibugyo, na nyingine mpya inayotoka Fort Portal, kupitia Hospitali ya Rufaa mpaka Mbarara. Pamoja na changamoto za maendeleo, Serikali ya Uganda imejitahidi kuboresha miundombinu ya barabara. Ukiwa popote mjini Fort Portal huwezi ukakosa kuona jengo kubwa, lililo mlimani, ambalo ndio makazi rasmi ya Omukama, Mfalme wa Tooro. Jengo hili lililo kileleni mwa mlima na eneo lote la mlima limetengwa kwa ajili ya Mfalme na shughuli za kiutamaduni zinazohusu ufalme. Eneo hili linapakana na Barabara ya Fort Portal-Kasese.

Jengo la Omukama wa Tooro. Kutoka kushoto ni: Ngusa Izengo, Dr. Mpapalika, Dada Christina Masika, Mzee Agen Mwandosya, Meck Mwakipunga, Bupe Kamugisha, na Dan Rubombora Atenyi; walipotembelea Tooro wakiwa na Lucy Akiiki na Mark Mwandosya, Agosti 2013
Barabara ya Lugard
Jengo lililokuwa duka la Kahigwa & Son, Barabara ya Fort Portal-Kasese
Mtaa wa Rukidi III
Duka la Wachina la Madawa ya Mitishamba, Barabara ya Bwamba
Kasiisi kijiji kilicho katika Barabara ya Fort Portal-Kamwenge. Hapa ndipo alipoishi Bibi Mzaa Mama wa Lucy Akiiki
Barabara ya Fort Portal-Kamwenge (66km) iliyojengwa na Kampuni ya Chinese Railway Seventh Group

Empaako


Mgeni yeyote unapofika Tooro, kitu cha kwanza unapokutana na wenyeji ni kuulizwa swali “Empaako Yawe?” Unashangaa naulizwa nini? Kila utakapokutana na Mutooro wa kila rika hili ni swali utakaloulizwa kwanza. Baada ya muda utaelewa kwamba unaulizwa jina lako ni lipi kati ya majina 12 tu ambayo Watooro wote hupewa mara baada ya kuzaliwa. Ni ustaarabu ambao Watooro wamekuwa nao na umeendelezwa vizazi na vizazi ikiwa ni ishara ya heshima, upendo, maelewano, umoja na mshikamano baina yao. Mtoto anapokutana na mtu wa rika kubwa, atapiga magoti na kuelekeza bega moja kwake, atamuuliza “Empaako Yawe?” Baada ya kujibiwa ndipo atamsalimia kutumia hilo jina kwa kusema “Oraire ota Araali?” Araali likiwa ni moja ya majina 13 yanayotumika na jamii yote ya Watooro.


Empaako, kama jina la heshima hutumika na jamii ya Banyoro, Batooro, Banyamwenge, Banyakyaka, Batagwenda, Batuku, na Banyabindi. Majina 11 yanaanzia na A na moja tu linaanzia na O. Majina hayo ni Abala; jina ambalo kihistoria lilitengwa kwa ajili ya wale walio karibu na Omukama; Abooki; Okaali; Atwoki; Araali; Ateenyi; Akiiki; Apuuli; Acaali; Adyeri; Amooti; na Abwoli.


Empaako kijadi hutolewa siku tatu baada ya msichana kuzaliwa, na siku nne baada ya mvulana kuzaliwa. Kabla ya hapo mtoto na mama yake hukaa ndani ya nyumba kwa muda wote bila kutoka. Wakati huo taarifa ya ujio wa mtoto huwafikia ukoo ikiwa ni pamoja na Bibi, Babu, Wajomba, Shangazi na ndugu wengine wa karibu. Kutoa jina hilo ilikuwa ni sherehe maalum ikiwahusu ndugu na jirani wa karibu sana. Sherehe inahusu mama na mwana kutolewa nje ya nyumba (Kwarura), kumtambua mtoto (Kutonda), na mtoto kupewa empaako. Baada ya hapo wahusika wote hupewa chakula kilichotayarishwa maalum kwa sherehe hiyo. Baadaye mama anapanda mgomba mtoto akiwa wa kike, na baba hupanda mmea uitwao mnyaa (Omutoma). Majina manne; Araali, Acaali, Apuuli, na Abala yametengwa ka ajili ya wanaume. Okaali linatumika kwa Mfalme. Majina yaliyobaki yanaweza kutumika na jinsia zote mbili. Abala ni mwenye upendo. Abooki ni mwenye heshima kwa wazazi. Abwooli ni yule ajuaye taratibu na itifaki. Acaali linamaana ‘tunayefanana’. Adyeri ni yule menye upendo na moyo mkubwa. Akiiki ni yule anayependa na kujitolea kuhusu jamii. Amooti ni yule anayeheshimu watu wengine. Ateenyi anatambua na kurekebisha makosa baina ya watu. Atwooki ana upendo, myenyekevu na wenye nidhamu ya hali ya juu. Apuuli yule mwenye uwezo mkubwa na anayependwa na watu. Araali ni yule mwenye uwezo wa kuokoa watu wengine.


Majina haya yana uhusiano na maneno ya kijaluo yanayofanana fanana. Hiki ni kielelezo cha uhusiano wa karne nyingi kati ya wenyeji wa kaskazini mashariki ya Uganda, Walango, na jamii ya Sudan ya Kusini ambao ni asili moja na Wajaluo. Kwa heshima, wageni nao hupewa empaako wanapofika Tooro kwa mara ya kwanza. Ndivyo ilivyokuwa kwa Mwandishi, ambaye amepewa Araali kama empaako. Max yeye ni Amooti, Sekela ni Abwooli, na Emmanuel ni Apuuli. Mama yao ni Akiiki, jina alilopewa baada ya kuzaliwa.


Ukiwauliza Watooro majina haya yalitoka wapi, wazee watakwambia yalishushwa kutoka Mbinguni. Pamoja na umuhimu wake katika kuendeleza umoja, upendo, mshikamano, fahari na heshima katika jamii, utamaduni huu umepungua. Kwa kuzingatia majukumu yake, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), kupitia uamuzi wake 8.COM 7.a.12 wa mwaka 2013 (Decision of the Intergovernmental Committee: 8.COM 7.a.12) liliamua mfumo wa Empaako uwe ni suala la haraka na muhimu kutunza na kuendeleza kama urithi wa dunia. Shirika la kujitegemea liitwalo “Engabu za Tooro” Ngao za Tooro limewezeshwa na UNESCO kuanzisha mradi wa kuenzi, kulinda, na kueneza utamaduni wa Empaako.


Kielelezo kilichotengenezwa kwa shaba chenye Majina ya Asili (Empaako) iliyotolewa na UNESCO kama zawadi kwa Manispaa ya Fort Portal

Huduma za Kijamii


Miji ya Afrika ya Mashariki imefanana sana kwa jinsi ilivyosanifiwa wakati wa ukoloni. Unapoutembelea mji unasafiri miaka mia moja nyuma na kuona jinsi miji ilivyoanza na kukua ikizingatia mahitaji ya kiutawala ya watawala wa kikoloni. Eneo muhimu kwao ilikuwa ni Boma. Hapo ndipo ilikuwa ngome ya utawala, ulinzi na usalama. Majengo ya kuishi watawala yalikuwa maeneo hayo. Kwa maana ya Mbeya, huko ndiko kulikuwa kuinaitwa uzunguni. Wazungu hawa walikuwa na mahitaji ya kawaida ya maisha na hivyo walihitaji na kuwezesha uanzishaji wa vituo vya biashara ambavyo vilianzishwa na kuendeshwa na familia za jamii ya asili ya kiasia. Kwa Mbeya hao ndipo tulipopaita uhindini.


Kwa wasafiri wenye urafiki na mazingira na mazingira yaliyojengwa, historia na mvuto wa mji unatokana na majengo ya ibada ya imani mbali mbali zinazohusiana na mji huo. Kwa Fort Portal lazima utavutiwa na Misikiti na Makanisa. Unapoingia mji mkongwe kutoka Mubende, baada ya kuvuka Mto Mpanga, kushoto kilimani ni msikiti wa Shia Ismailia, na kulia bondeni ni Msikiti Mkuu wa Baraza la Waislamu Uganda, kama inavyo onekana kwenye vielelezo. Msikiti mwingine mkubwa unajengwa kilomita mbili pembeni mwa barabara ya Fort Port Portal-Bundibugyo.




Msikiti Mkuu wa Baraza la Waislamu Fort Portal
Msikiti Mkuu wa Shia Ismailia Fort Portal
Ujenzi wa Msikiti Barabara ya Bwamba eneo la Mugunu Kisenyi (Masjid Jaamiah)

Katika barabara ya Kasese mkabala na eneo la Omukama ni Makao makuu ya lililokuwa kanisa la Kianglikana (Church Missionary Society-CMS), ambalo jina lake rasmi sasa ni Kanisa la Uganda. Inanikumbusha wazazi wangu (Mwenyezi Mungu Awarehemu) walipohamia Dodoma kutoka Mbeya mwaka 1961, kanisa la kikristo la kiprotestanti lilikuwepo hapo wakati ule na tulilojiunga nalo lilikuwa ni CMS. Madhehebu inaendesha pia Hospitali ya Kabarole, ambayo wakati Mwandishi wa Makala hii na familia wakiwa safari, ilikuwa inafanyiwa matengenezo makubwa. Ujenzi wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Yohana (St John’s Cathedral) ulikamilika na Kanisa kuanza kutumika mwaka 1939.

Kanisa Kuu la Mtakatifu Yohana

Moja ya taasisi za kwanza za elimu zilizoanzishwa na Kanisa ni iliyokuwa shule ya msingi na kati na ambayo sasa ni shule ya Sekondari ya Kyebambe. Hapa ndipo aliposoma Lucy Akiiki darasa la saba mpaka la nane, kabla ya kuendelea na masomo ya sekondari Gayaza, Kampala. Margaret Amooti, shemeji yangu, alimtangulia Akiiki hapo Kyebambe. Wengine waliosoma hapo ni Norah Abwooli, Gertrude Amooti; Betty Abooki. Kama shule ya wasichana Kyebambe ilianzishwa mwaka 1910, na mmoja ya waliosoma hapo ni Mama Mkwe Susana Adyeri (1911-2006) (Mwenyezi Mungu Amrehemu), Bibi ya akina Max, Sekela, na Emmanuel.

Shule ya Sekondari ya Kyebambe

Mbele ya ofisi na duka la vitabu la Kanisa la Uganda, kwenye bustani inayopakana na Barabara ya Kasese, katikati ya mji, huwezi ukapita bila kuona sanamu kubwa ya Aberi Kakomya Balya. Aberi Kakomya alizaliwa mwaka 1877 katika Kaunti ya Kyaka, Wilaya ya Kyenjojo, Tooro. Wazazi wake walikuwa wahamiaji kutoka eneo la Ntungamo, Ankole. Aliishi maisha yake yote Uganda magharibi na hususan Tooro. Alifariki mwaka tarehe 26 Novemba 1979 akiwa na umri wa miaka 102. Alipata wito wa kueneza injili akiwa na miaka 30.

Hospitali ya Kanisa la Uganda

Ndipo Kanisa lilipogundua uwezo wake mkubwa wa kuhubiri na kumtumia katika maeneo mbali mbali ya Tooro, Ankole na Mashariki ya iliyokuwa Congo ya Wabelgiji ambayo sasa ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Baada ya kusomea theolojia, Aberi Balya akapanda ngazi katika kanisa kuanzia udikonia na hatimaye akawa Kasisi wa Kanisa la Mtakatifu Paulo, Fort Portal, Kabarole. Yeye ndiye aliyependekeza na kusimamia ujenzi wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Paulo ambalo mpaka leo ni imara na kivutio kikubwa cha Fort Portal. Aliwekwa wakfu kama Askofu wa Sudan na baadaye akawa Msaidizi wa Askofu wa Uganda akisimamia majimbo ya Kigezi, Ankole na Bunyoro. Katika utumishi wake Aberi Balya amewahi kuwa kaimu Askofu Mkuu wa Kanisa la Uganda. Aberi Balya alihusika pia na kazi muhimu ya kutafsiri Biblia na Kitabu cha Sala (Liturgy) kwa lugha ya Runyoro/Rutooro kutoka kiingereza. Kwa hayo machache yaliyotangulia, na kutokana na mchango wake mkubwa katika masuala ya elimu, afya, maji na mengineyo, ndipo kiu changu cha kutaka kumfahamu Askofu Aberi Kakomya Balya kikawa kimepata jawabu. Mwenyezi Mungu Airehemu Roho ya Marehemu.

Sanamu ya Askofu Mkuu Aberi Kakomya Balya

Kilomita mbili kutoka Jengo la Mfalme wa Tooro katika barabara ya Kasese upande wa kushoto unavutiwa na mabango yapatayo saba hivi yakionesha shughuli mbalimbali zinazoendelea zikisimamiwa na Kanisa Katoliki. Kwa msafiri unayetoka Tanzania wazo linakujia kuwa mabango yote hayo yangewekwa alama nyekundu ya X hata kama ujenzi au upanuzi wa barabara utafanyika na wajukuu wa wajukuu zetu!

Vibao vikionesha shughuli mbali mbali za Kanisa Katoliki Fort Portal

Virika ni kiunga muhimu cha Fort Portal. Kwani ndiko kwenye makao makuu ya Kanisa Katoliki Jimbo Kabarole. Kitovu cha eneo hilo ni Kanisa Kuu la Virika la Mama Mtakatifu wa Theluji (Virika Cathedral of our Lady of Snows), ambalo limejengwa kwa usanifu wa kisasa na wa hali ya juu. Ni kanisa la mviringo ambalo linafana kwa mwonekano kutoka upande wowote ule. Faida ya usanifu wa jengo kimduara ni kwamba unaweza kwaeneo dogo ukapata matumizi makubwa. Hapa ndipo marafiki zetu Mathew Kasanga Amooti na Norah Abwoli walipofunga pingu za maisha. Amooti na Abwoli ni wazazi wa Chriven Apuuli, Dereck Adyeri, Harriet Abwooli (RIP), Edwin Amooti, Isaac Apuuli, and Lucy Ateenyi.

Kanisa Kuu la Virika la Mama Mtakatifu wa Theruji

Kanisa limezungukwa na ofisi, nyumba ya watawa wa Banyatereza, duka la vitabu, nyumba ya wageni, vyumba vya mikutano, duka la dawa, Seminari ndogo ya Mtakatifu John Mary Vianney, Chuo cha Ufundi cha Mtakatifu Maria, Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mtakatifu Maria Gorette, Shule ya Wauguzi ya Virika, na Hospitali Familia ya Mtakatifu, Virika.




Kuelekea Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mtakatifu Maria Goretti
Hospitali ya Virika ya Familia Takatifu

Kanisa Katoliki pia linamiliki Kiwanda muhimu cha Dawa cha Virika Pharmaceuticals Ltd. Kanisa hututayarishia maisha bora ya kiroho ili tuwe na pumziko la milele. Halituachi wakati wa mpito. Kwani pamoja na misa ya wafu Kanisa linamiliki kampuni ya maziko, Uganda Funerals Ltd.




Kiwanda cha Madawa cha Virika

Kwa muda tuliokuwa Tooro, haikuwa rahisi kutembelea madhehebu zote na kuthibitisha kazi kubwa inayofanywa na madhehebu zote katika maendeleo ya jamii. Maelezo yaliyotangulia yachukuliwa kama mfano tu wa jinsi madhehebu za imani mbali mbali zinavyoshirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Uganda na wananchi katika kukuza huduma za kijamii.


Chuo Kikuu cha Mountains of the Moon (Mountain of the Moon University - MMU)


Moja ya maeneo ambayo walimu, hasa tuliofundisha, na tunaendelea kuwa na uhusiano na taasisi za elimu ya juu, ni vyuo vikuu. Ndivyo ilivyokuwa nilipopata nafasi ya kutembelea MMU, nikiwa mgeni wa Mkuu wa Chuo (Chancellor), Profesa Edward Rugumayo Amooti.


Prof. Edward Rugumayo (kushoto) akimzungusha Prof. Mark Mwandosya kwenye majengo ya madarasa na ofisi za MMU

Profesa Rugumayo ni mmoja ya wanazuoni mashuhuri Uganda, Afrika ya Mashariki na Afrika kwa ujumla. Amewahi kuwa mwanachuo Makerere, Waziri wa Elimu, Balozi, mwanachuo Zambia, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kampala na msimamizi huru wa chaguzi nyingi Afrika.

Prof. Edward Rugumayo (kulia) na Prof. Mark Mwandosya wakikagua Maktaba ya MMU

Baada ya kustaafu na kurudi Tooro, Profesa Rugumayo amejishughulisha na masuala ya maendeleo ya jamii. Yeye na mwenzake Jaji (Mstaafu) Seth Manyindo ndio walioibua wazo la kuanzisha chuo kikuu magharibi ya Uganda ambacho mbali na kuongeza idadi ya wasomi nchini, kingejikita katika utafiti na utatuzi wa changamoto za kipekee za nyanda za juu, bonde la ufa, na milima ya magharibi ya Uganda.


Pamoja na mambo wengine wasomi hawa wawili waliona ni muhimu watoe mchango kwa jamii ya Tooro iliyowasomesha mpaka wakafika chuo kikuu. Kwa kushirikiana na Halmashauri za Kabarole, Ntoroko, na Kasese, walianzisha chuo kikuu na kupata usajili mwaka 2005 kama kampuni isiyo na hisa na isiyojiendesha kibiashara (Company Limited by Guarantee).


Prof. Edward Rugumayo na Prof. Mark Mwandosya wakiwa na baadhi ya viongozi wa taaluma na utawala, MMU

Chuo Kikuu MMU kilianza pembeni kidogo ya mji wa Fort Portal katika mazingira magumu kidogo. Hata hivyo Halmashauri ya Wilaya ya Kabarole imewapatia ekari 75 na idara ya Magereza imewapa ekari 85, katika eneo lililo karibu na Ziwa la Kreta la Saaka mahali ambako kampasi kubwa inaendelea kujengwa. Shughuli za kila siku za Chuo, kama ilivyo vyuo vingine Afrika ya Mashariki zinaendeshwa na Baraza la Chuo, Seneti, Makamu Mkuu wa Chuo, ambaye kwa sasa ni Profesa Kasenene, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo, Wakuu wa Vitivo, Wakuu wa Idara, na wafanyakazi wa utawala. Chuo kinasimamiwa na Bodi ya Wakurugenzi ambao ndio waanzilishi wa Chuo. Mwenyekiti ni Jaji (Mstaafu) Seth Manyindo, na wajumbe wa Bodi ni: Prof. Osward Ndoleriire; Kanali (Mstaafu) Tom Butiime; Prof. Edward Rugumayo; Jaji Percy Night Tuhaise; Ndugu Joseph Katto; Ndugu Yusuf Kamali; Dr. Jockey Nyakaana; Dr. Charlotte Karungi; na Prof. (Emeritus) Dr Semana Arseni. Serikali imeonesha nia ya kukichukua chuo hicho na kukifanya chuo kikuu cha umma.


Mbali na taaluma, kutoa huduma na kufanya utafiti, kama ilivyo kawaida ya vyuo vikuu, MMu ina mradi wa kukusanya, kuandaa, kupanga na kutunza kwa njia ya kidigitali, kumbukumbu zinazohusu masuala ya utawala katika wilaya za Kabarole, Hoima, Masindi, na Ufalme wa zamani wa Tooro na ule wa Bunyoro. Kumbukumbu hizi ni za kutoka mwaka 1850 mpaka Uganda ilipopata uhuru. Ni hazina kubwa katika kuelewa masuala ya uhusiano kati ya utawala wa kikoloni na falme za Uganda; migogoro baina ya jamii mbalimbali, kumbukumbu kuhusu maliasili, kilimo, mifugo, wakimbizi, elimu, na usalama.


Prof. Edward Rugumayo (katikati) na Prof. Mark Mwandosya (kushoto) wakipata maelezo kutoka kwa Moses Akugizibwe, Mratibu wa Mradi wa kukusanya, kupanga na kutunza kumbukumbu na nyaraka za kale.

Mradi mwingine ni ule wa Radio. MMU imeanzisha kituo cha radio (MMU Radio) ambacho madhumuni yake ni kutoa mafunzo na elimu ya mbali kwa wale ambao hawawezi kuwa Chuoni wakati wote. Aidha kituo hicho ni kiungo muhimu kati ya Chuo na jamii.


Ushauri wangu kwa vyuo vikuu vilivyo katika mabonde ya ufa ya Mashariki mwa Afrika ni kushirikiana katika utafiti unaohusu asili ya milima, volkano, udongo, sayansi ya matetemeko (seismology), fizikia na jiolojia ya miamba, maziwa ya kreta, na kilimo. Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST), MMU, na vyuo vilivyo nyanda za juu za bonde la ufa, Kenya, Tanzania na Ethiopia vinashauriwa kuanzisha ushirikiano katika taaluma.


Prof. Mark Mwandosya akipata maelezo kutoka kwa Msimamizi wa Radio ya MMU

Bustani ya Miti na Mimea Tooro (Tooro Botanical Gardens)

Mwenyezi Mungu amempa binadamu uwezo mkubwa wa akili ili, pamoja na mambo mengine, aweze kusimamia na kutunza viumbe wengine ikiwa ni pamoja na miti na mimea. Kasi ya kupotea kwa miti na mimea mingine ni kubwa kiasi cha kwamba inawezekana tukawaachia wajukuu zetu uhaba mkubwa wa miti na mimea ya asili. Miti na mimea ya asili ndio chanzo cha rutuba, mvua, dawa asilia na dawa za kisasa, chakula, matunda, na hifadhi ya ndege, nyuki, na wanyama wengine. Hazina hii imeonekana muhimu kwa nchi zilizoendelea kiasi cha kwamba mbegu za miti na mimea kutoka maeneo ya tropiki imekusanywa na kuhifadhiwa kwa ajili ya vizazi vijavyo. Maana yake ni kwamba hapo baadaye tutaomba au tutanunua mbegu zetu kutoka kwao. Tukiri kwamba katika maeneo mengi ya Afrika ya Mashariki wakoloni walianzisha bustani za kutunza miti na mimea ya asili. Tukuyu ilikuwa na Botanical Gardens nzuri. Amani, Tanga ilikuwa na Botanical Gardens ambazo zilikuwa bustani kubwa za namna hiyo Afrika ya Mashariki. Nilipotembelea Amani mwaka 2009, nilipouliza kuhusu Botanical Gardens za Amani, nikaambiwa ilipokuwa bustani, sasa ni majengo ya wafanyakazi wa kituo cha afya!


Bustani ya Mimea Asilia ya Tooro

Yaliyotangulia yanaweka muktadha wa umuhimu wa kuanzishwa kwa bustani ya Tooro ya miti na mimea ambayo ipo Fort Portal. Bustani ilianzishwa mwaka 2001 baada ya Mamlaka ya Taifa ya Misitu, Uganda, kutoa ekari 100 kwa ajili ya mradi wa Tooro Botanical Gardens (TBG).

TBG imeanzishwa kwa madhumuni makubwa matatu:-


Hifadhi:

kuanzisha hifadhi ya mimea asilia ya Afrika ya Mashariki; kuanzisha na kutunza mimea na miti yenye asili ya Bonde la Ufa Uganda; kueneza uelewa wa faida mbali mbali za miti, vichaka na mimea asilia; kueneza uelewa na faida za madawa yanayotokana na mimea asilia; kuhamasisha utunzaji na maendeleo endelevu ya mimea ya asili kwa ajili ya chakula na matumizi viwandani.


Elimu:

kuanzisha programu ya elimu kuhusu bioanuai ya maeneo yamagharibi ya Uganda; kuandaa na kuendesha semina kuhusu bioanuai kwa kushirikiana na taasisi nyingine na umma; kuwa kituo ambacho wanafunzi wanaweza kuendeleza uelewa na na utafiti.


Ziara na Utengenezaji wa bidhaa:

kuwa na maeneo yaliyotengwa kwa mafunzo na maelezo maalum; kuwa na maeneo yaliyotengwa kwa mapumziko; kutengeneza bidhaa mbali mbali zitokanazo na mimea ikiwa ni pamoja na dawa; kuuza na kusambaza miche na mbegu.


Nilipotembelea TBG kwa mara ya pili mwezi Novemba 2017 nilivutiwa na mradi unaoendelea wa kukusanya, kutunza na kifanya mmea aina ya “Cycad” uwe endelevu. Hii inatokana na wataalam wa bioanuani kuutangaza mmea huu kuwa katika hatari ya kupotea. Ni familia ya mimea inayofanana na michikichi au mtende, ambayo huota katika maeneo oevu, hasa pwani, na kandokando ya mito, mabwawa na maziwa. Tukiwa Shule ya Kati Chunya tuliitafuta aina ya mimea hii majira ya kiangazi, na kuvuna majani yake kwa ajili ya kutengeneza mikeka, vikapu, kofia, na vifaa vingine.

Mradi unahusu kukusanya na kuotesha mbegu na miche ya mimea aina ya michikichi na mitende na “Cycad” ya mashariki ya Afrika, Afrika na duniani kote ili TBG iwe kituo kimoja chenye aina mbalimbali za mimea hii. Mpaka sasa wameweza kukusanya aina 12 za mimea hiyo. Ni mradi wa miaka 10 na TBG inatarajia kushirikiana na Montgomery Botanical Centre, Florida, Marekani katika kutekeleza mradi huu.


Mradi wa hifadhi ya mimea aina ya michikichi,mitende na minazi (Cycad)

Kuanzishwa kwa TBG ni matokeo ya juhudi za Profesa Edward Rugumayo Amooti na wenzake na ushirikiano na Mamlaka ya Taifa ya Misitu ambao uliwezesha Mamlaka hiyo kutoa eneo la kutosha katikati ya mji. TBG inaongozwa na Mkurugenzi ambaye kwa sasa ni Ndugu Godfrey Ruyonga, mtaalam wa mimea (ethno-botanist).


Maziwa ya Kreta za Volkano Tooro


Kabla sijatembelea Tooro, nilidhani Rungwe ndio kwenye maziwa mengi yaliyo katika kreta za volkano. Wilaya ya Rungwe ina maziwa ya kreta za volkano ambayo hayazidi ishirini. Tooro ina maziwa ya aina hiyo zaidi ya 80. Ni maziwa yanayotofautiana ukubwa, kutoka yale unayoweza kuyaita maziwa makubwa mpaka yale yanayofanana na mabwawa madogo ambayo ni sehemu ya mashamba ya watu kama ilivyo katika eneo la Kasiisi, Rutete, km 15 kutoka mjini Fort Portal.


Moja ya maziwa ya kreta tuliyotembelea ni Ziwa Kyaninga, km 10 kutoka Fort Portal. Pamoja nasi alikuwa ni Mzee Agen Mwandosya na Meck Mwakipunga, wakati ule akiwa Mwenyekiti wa Halmashahauri ya Busokelo. Eneo moja la Ziwa Kyaninga limekodishwa kwa mwekezaji ambaye amejenga hoteli ambayo usanifu na ujenzi wake unashabihiana na mandhali ya eneo la Ziwa.

Ziwa lingine la aina hiyo tulilotembelea, Ziwa Nyabikere, ambalo liko pembeni mwa barabara ya Fort Portal-Kamwenge katika eneo la Msitu wa Kibale, km 21 kutoka Fort Portal.




Ziwa la Kreta Nyabikere

Mwekezaji C.V.K. Lakeside Resort, amekodi eneo la kingo ya Ziwa ambapo amejenga nyumba ya mapumziko na mgahawa. Majengo yaliyopo yanaendana na mazingira ya Ziwa. Kwa lugha ya kitooro nyabikere maana yake vyura.




Mgahawa ulio ukingoni mwa Ziwa Nyabikere

Tukiwa Fort Portal tulipata nafasi ya kuzungunza na Dan Rubombora Atenyi kuhusu jinsi ya kuendeleza utalii wa maeneo ya maziwa ya kreta za volkano. Ndipo tulipofahamishwa kuhusu shauri lililofika Mahakama Kuu, la wananchi wanaoishi maeneo ya maziwa ya kreta, dhidi ya Halmashauri ya Tooro, Mwekezaji, na Mwanasheria Mkuu wa Uganda. Mbele ya Jaji Anthony Ojok Oyuko wa Mahakama Kuu ya Uganda, walalamikaji walikuwa wanapinga Halmashauri ya Kabarole kukodisha maziwa ya kreta 23 kwa mwekezaji Ferdsult Engineering Services na kwamba makubaliano ya mwekezaji na Halmashauri ya tarehe 27 Mei 2015 yalikuwa yanapingana na Katiba ya Uganda na Sheria ya Maji. Katika makubaliano hayo mwekezaji alipewa leseni ya matumizi inayozuia watumiaji wengine, kwa ajili ya kuendeleza uvuvi. Ili kutekeleza makubaliano hayo mwekezaji aliajiri walinzi ambao waliwazuia wananchi wa maeneo hayo kutumia maji ya maziwa hayo, matumizi ambayo wamekuwa wakifanya vizazi na vizazi huko nyuma.


Halmashauri ilijitetea kwamba utekelezaji wa mkataba huo: ungeongeza mapato ya Halmashauri na Serikali; ongezeko la samaki lingesaidia jamii kupata protini; mwekezaji angezuia uvamizi wa maeneo ya maziwa; uwekezaji huu ungezuia kuenea kwa kichocho; na uwekezaji ungeongeza ajira.

Katika hukumu yake aliyoitoa tarehe 7 Juni 2017, Jaji alikubaliana na hoja walizotoa walalamikaji. Alihoji pia kwamba mwekezaji hakuwa amethibitisha alikuwa amesajiliwa kisheria. Aidha Halmashauri ilikuwa haijafanya tathmini ya athari kwa mazingira ya mradi huo kama inavyotakiwa kisheria. Aidha Jaji Oyuko aliamuru wananchi wasizuiwe kutumia maji ya maziwa hayo. Shauri hilo HCT - 01 - MC - 0062 la 2016, bila shaka litakuwa rejea katika mashauri yatokanayo na migogoro ya umiliki na matumizi ya maziwa ya kreta Afrika ya Mashariki.


Bonde la Ufa Mashariki ya Afrika Tawi la Magharibi – Vivutio Asilia


Bonde la Ufa la Mashariki ya Afrika, Tawi la Magharibi linaanzia Bahari ya Sham, kupitia Sudan na Sudan ya Kusini, Ziwa Albert, Ziwa Edward, Ziwa Kivu, Ziwa Tanganyika mpaka Ziwa Nyasa. Sehemu kubwa ya Tooro iko katika nyanda za juu za Bonde a Ufa, ikiwa ni sehemu ambayo imeinuliwa kutokana na volkano zilizolipuka karne nyingi zilizopita, kama ilivyo Mbeya na Rungwe.


Kuelekea maeneo mbalimbali yenye umuhimu

Kutoka nyanda za juu za Tooro kushuka kwenye bonde la ufa unashuhudia mandhari ambayo huwezi ukaisahau daima. Kwani ni mandhari na mazingira mazuri sana. Kutoka Fort Portal kwenda Bundibugyo unapita miji midogo ifuatayo: Rwengoma; Butebe; na Nyakasura/Ibonde. Eneo la Bukuuku, Ibonde na Nyakasura lina umaarufu kwa maana ya kuwa na taasisi nyingi za utamaduni na elimu.

Kijiji cha Bukuuku au Bukuku chini ya safu za Milima ya Rwenzori

Taasisi za elimu ni pamoja na zilizoanzishwa na madhehebu ya kanisa la kianglikana wakati wa uongozi wa Askofu Aberi Balya. Balozi Elizabeth Bagaya, dada ya aliyekuwa Omukama Kaboyo Olimi VII, ameanzisha Wakfu wa Batebe (Dada ya Omukama).




Nyumba ya Batebe na Kituo cha Utamaduni cha Wakfu wa Batebe wa Tooro

Shule maarufu ya Sekondari ya Nyakasura iko maeneo hayo. Ni moja ya shule kongwe nchini Uganda. Nyakasura, shule ya sekondari ya Serikali, ilianzishwa mwaka 1926 na Ernest Ebohard Carwell, Mskoti, na mwanajeshi mstaafu, kama shule ya binafsi. Alitokea King’s College Buddo ambako baada ya kutofautiana na Mkuu wa Shule akashawishiwa na wanafunzi wawili kutoka Tooro, Komwiswa na Balya, aenda Tooro akaanzishe shule nyingine. Ndipo Rukirabasaija Daudi Kasagama Kyebambe III, Omukama wa Tooro, akampa eneo la Nyakasura ili aanzishe shule ya wavulana.

Nyakasura ilikuwa ni shule ya kwanza Uganda kutumia umeme kupitia mradi mdogo wa umeme kutumia maji ya Mto Nyakasura uliotekelezwa miaka ya 1930. Mbali na taaluma, umaarufu wa Nyakasura unatokana pia na sare ya shule, ambayo tangu shule ianzishwe ni shati na sketi (scottish kilt), vazi maarufu ya Uskoti, Uingereza. Kwa miaka mingi Nyakasura ilikuwa moja ya shule bora kitaaluma nchini Uganda. Ilikuwa katika ligi moja na shule maarufu nyingine kama: King’s College Buddo, Namilyango, Kisubi, Ntare, Nabumali, Namilyango na St. Leo’s; na shule maarufu za wasichana kama vile: Gayaza (Shule aliyosoma Lucy Akiiki), Maryhill, St. Mary’s College Namagunga, Nabisunsa, na Nabingo. Changamoto mbalimbali zimepelekea kushuka kwa kiwango cha taaluma. Hata hivyo, chini ya uongozi wa Mkuu wa Shule wa sasa, Enock Manyindo, shule imeanza kuwa bora.


Sare ya Shule ya Sekondari ya Nyakasura (Picha kwa hisani ya P. Mugamba)

Wanafunzi wa zamani wa Nyakasura wana umoja wao. Hukutana mara moja kila mwaka na wamesaidia katika kuboresha miundombinu na taaluma. Mwaka 2017, kwa mfano, walichangia shilingi milioni 138 ili kuboresha mfumo wa maji shuleni hapo. Baadhi ya wanafunzi hao wa zamani ni pamoja na; Edward Rugumayo, Mkuu wa Chuo Kikuu MMU, na Chuo Kikuu cha Kampala; Crispus Kiyonga, Daktari na Waziri; Patrick Bitature, Mfanyabiashara maarufu, Jaberi Bidandi Ssali, Mwanasiasa na Mfanyabiashara; Paul Mugamba, Jaji wa Mahakama ya Upeo; Aston Kajara, Mwanasheria na Mwanasiasa; Prof. William Banage; Beatrice Kiraso, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki; Jaji (Mstaafu) Seth Manyindo; na Richard Buteera, Jaji wa Mahakama ya Upeo.

Lango la kuingia Shule ya Nyakasura (Picha kwa hisani ya P.Mugamba)

Baada ya kupita eneo hili barabara inaelekea Karagwe; Kitarasa; Kihondwe; na Kichwamba, ambao uko mpakani mwa Kabarore na Bundibugyo; Kisina; na Karugutu, mji mdogo ambao uko njia panda ya kwenda Rwebisengo hadi Ntoroko, ambayo ni Bandari ya Ziwa Albert; Kibuku; Burondo; Sempaya Hot Springs; Ntandi; Bubukwanga; Humya; Bundibugyo mjini; Busaru; Kirindi Nyahukya; mpaka Lamya ambapo ni mpakani mwa Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.


Bundibugyo iko katika Bonde la Ufa chini ya safu za milima ya Rwenzori. Bundibugyo ni makao makuu ya Ufalme wa Bamba na kiongozi wake ni Omudingiya (Mfalme) Martin Ayongi Kamya Kabla ya Ufalme wa Tooro kugawanyika sehemu tatu, Tooro, Rwezururu na Bwamba, falme hizi zilikuwa chini ya Omukama wa Tooro. Kilimo ni kazi kubwa na kilimo cha kakao kimeshamiri sana. Ni sehemu ya joto na ukiwa huko utadhani uko wilaya ya Kyela. Kilomita 10 kaskazini mwa Bundibugyo unafika Mto Semuliki na daraja lake ndio mpaka kati ya Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Siku tulipopita bonde la ufa kwenda Bundibugyo wananchi wengi walikusanyika njiani wakiwa wameshika maani ya migomba, majani, na matawi ya miti. Ilikuwa ni siku ya ujio wa Omudingiya, Mfalme wao, ambaye alikuwa anarudi kutoka Kampala.


Maeneo mawili ambayo tuliyatembelea na tunashauri msomaji ukifika magharibi ya Uganda utembelee ni Chemchemi za Maji ya Moto za Sempaya ambazo ziko katika Hifadhi ya Taifa ya Semuliki, na eneo la Ziwa Albert.


Chemchemi za maji ya moto za Sempaya

Chemchemi za maji ya moto za Sempaya ziko mita mia mbili tu kutoka barabara kuu ya Bundibugyo. Chemchemi hizo zinaangaliwa na wahifadhi wa Hifadhi ya Taifa ya Semuliki. Bi Prossy Bigabirwe, Mhifadhi, alitupa maelezo ya kitaalaam kuhusu chanzo cha chemchemi hizo. Aidha alitupa simulizi kuhusu jinsi wenyeji wanavyoelezea chemchemi hizo. Kuna maeneo mawili ya chemchemi hizo, chemchemi ya kiume, na chemchemi ya kike. Kufuatana na simulizi za wenyeji, Bamaga, ambao ni jamii ya Bamba, siku moja wanawake waliingia msituni na kukutana na mwanaume ambaye alikuwa mgeni kwao, na alikuwa kama bubu. Walipokimbia kurudi kijijini na kuelezea waliyoyaona, wanaume wakakusanyika na kwenda mahala alipokuwa huyo mgeni. Walimkuta kama walivyoelezwa, hazungumzi bali yuko na mkuki wake.

Chemchemi za Sempaya

Ndipo walipomchukua kijijini ambako walimtunza na baada ya muda mrefu akajifunza mila, desturi na lugha ya wenyeji wake. Wakamwozesha na akawa na familia yake. Siku moja aliondoka kwenda msituni kuwinda. Hakurudi nyumbani, Kesho yake walipomtafuta wakakuta mkuki wake na nguo zake kandokando ya chemchemi ya upande mmoja. Ndipo walipokata tamaa na kubaini kwamba alikuwa amejitosa kwenye chemchemi yenye maji ya moto na udongo wa moto sana. Walipotoa taarifa kijijini, mke wake, Nyansimbi, alihuzunika sana. Naye siku moja akatoka kwenda msituni kutafuta kuni. Hakurudi nyumbani. Kama ilivyokuwa kwa mume wake, wakakuta nguo zake pembeni mwa suhemu ya pili ya chemchemi za Sempaya. Wenyeji wakaita sehemu hiyo kuwa chemchemi ya kike, au Nyansimbi. Mpaka sasa wenyeji huenda mahali hapo kutambika. Mwezi Novemba wanawake hutambika kwenye chemchemi ya kike, na wanaume hufanya matambiko eneo la chemchemi ya kiume.


Kwa mujibu wa Mhifadhi, Hifadhi ya Taifa ya Semuliki ina aina tatu za wanyama wakubwa; tembo, viboko, na chui. Hifadhi ina aina 11 za kima; aina mbili za hao huonekana usiku tu (nocturnal primates). Hifadhi ina aina 415 ya ndege na kati yao aina 35 hazipatikani kokote duniani isipokuwa Hifadhi ya Semuliki tu. Watalii wengi kutoka ng’ambo hutembelea Hifadhi. Watafiti wengi kuhusu wanyama na mimea asilia, ndege, na vipepeo hufika katika hifadhi mara kwa mara.


Sehemu ya pili ambayo msomaji anashauriwa kuitembelea ni Ziwa Albert. Ziwa liko km 50 kutoka Karugutu, njia panda ya barabara ya Bundibugyo. Ziwa liko katika Bonde la Ufa. Kama ilivyo Usangu na Bonde la Ziwa Rukwa, ni sehemu ya joto. Kuelekea Ziwa Albert unapita mbuga ambazo wenyeji wake ni Batuku, jamii inayoishi kwa ufugaji wa ng’ombe. Sehemu ya mbuga hizo ni mwendelezo wa Hifadhi ya Semuliki ambayo hufika mpaka Ziwa Albert. Mji mdogo wa Ntoroko ni bandari ya mizigo iendayo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na ni bandari ya wavuvi wa samaki. Mbali na shughuli bandari, upande wa kusini magharibi wa Ziwa nia shwari. Shughuli za utafutaji na uchimbaji wa mafuta ya petroli zinafanyika maeneo ya Hoima.


Bandari ya Ntoroko, Ziwa Albert

Kugikwatako - Togikwatako


Hata ukiwa mtalii, si rahisi kufunga masikio kuhusu yale yanayotokea mahali ulipo. Ndivyo ilivyokuwa wakati tulipotembelea Tooro mwezi Oktoba 2017. Msomaji anayefuatilia mwenendo wa siasa za Afrika ya Mashariki hawezi kusahau yaliyotokea katika Bunge la Uganda tarehe 27 Septemba 2017. Kwani dunia nzima ilishuhudia vurugu ya hali ya juu iliyotokea Bungeni humo iliyotokana na mjadala mkali kuhusu marekebisho ya Kifungu cha 102(b) cha Katiba ya Jamhuri ya Uganda. Mjadala huo mkali kuhusu kuwepo au kutokuwepo na maerekebisho ya Katiba umeelezwa kutumia maneno mafupi ya lugha ya luganda; Kugikwatako(iguswe) na Togikwatako (isiguswe), au Kugikwataho na Otagikwataho katika lutooro. Kifungu hicho kinaeleza kwamba ukomo wa umri wa mtu kuweza kugombea urais ni kati ya miaka 35 na miaka 75. Pendekezo la marekebisho lililetwa Bungeni kupitia hoja binafsi ya Mbunge wa Igara Magharibi, Raphael Magyezi.


Kwa uzoefu nilionao kama Mbunge Mstaafu, si rahisi kwa Mbunge kutoa hoja nzito ya kurekebisha Katiba ya Nchi bila kuungwa mkono na Serikali na Chama Tawala. Wanaounga mkono hoja wanasema kuweka ukomo wa umri wa raia kugombea urais ni kumnyima raia haki yake ya kulitumikia Taifa katika umri wowote. Wanakumbusha kuwa ilibidi Watunisia, kwa mfano, wamchague kiongozi mwenye umri wa miaka 88 ili kutuliza nchi baada ya mageuzi yaliyotokana kile kinachoitwa ‘’Arab Spring’’. Wanasisitiza pia kwamba kuondoa ukomo wa miaka 75 ambapo mtu akiwa na umri huo hawezi kugombea urais, ni kuifanya Katiba ya Uganda ilingane na katiba nyingine za nchi za Afrika ya Mashariki. Hakika kiongozi mmoja mstaafu Tanzania, ambaye kwa sasa jina lake nalihifadhi, asingeweza kukubaliana na hoja hii. Kwani kwa maoni yake ukomo ni miaka 65. Kwa nini iwe miaka 65 na sio 60 au 64 au 67? Mimi sina jibu la kisayansi.


Wanaopinga marekebisho ya Katiba wanatoa hoja kwamba Katiba ni kama msaafu. Huwezi ukaibadili mara kwa mara kutokana na matakwa binafsi ya viongozi waliopo. Wanasisitiza kwamba marekebisho hayo yameletwa kwa manufaa ya Rais aliyepo ambaye ifikapo mwaka 2019 atakuwa amefikia umri wa miaka 77 na hivyo kwa Katiba ya sasa hawezi kuwa mgombea. Wanaamini pia Kifungu cha ukomo wa umri kiliwekwa ili kumzuia aliyewahi kuwa Rais, Apollo Milton Obote kurudi Uganda na kugombea urais.


Tulipokuwa huko hii ndio ilikuwa habari kubwa. Ilijadiliwa katika vyombo vya habari, vyombo vya usafiri, sehemu za burudani, matanga baada ya maziko, mikutano ya hadhara na mikutano ya faragha. Wabunge walitakiwa waende kwenye majimbo yao ili wakapate maoni ya wananchi. Ili kuwawezesha waifanye kazi hiyo, kila Mbunge alipewa shilingi za Uganda milioni 29. Wabunge wengi wa upinzani walirudisha fedha hizo wakihisi ni aina ya rushwa. Wanaopinga marekebisho walivaa vitambaa vyekundu na wanaounga marekebisho walivaa vitambaa vya manjano.

Pamoja na uwazi na uhuru wa majadiliano kuhusu suala hili yanayowahusisha wananchi, jambo ambalo ni zuri kwa demokrasia, kwa Katiba ya Uganda iliyopo, marekebisho hufanywa na Bunge. Bunge tayari limefanya uamuzi wa mwisho. Limepitisha muswada wa Sheria na Rais ameusaini na sasa umekuwa sheria rasmi ya nchi. Ni imani ya wananchi wa Uganda, na bila shaka wananchi wa Afrika ya Mashariki ni kwamba Bunge limeweka mbele mustakabali wa nchi.


Majumuisho


Safari au matembezi yanakuwa na maana pale tu msafiri anapokuwa na kumbukumbu ya safari kwa ajili ya kuwasimulia wengine ambao hawajafika huko alikofika, au kama wamewahi kufika basi wangependa kujua maendeleo yaliyofikiwa tangu walipofika. Jambo la muhimu zaidi ni kujibu swali “umejifunza nini kutokana na safari hiyo au matembezi hayo?”

Ukarimu ni moja ya sifa za Mwafrika. Tunachopishana kama waafrika ni kiwango tu cha ukarimu. Kwa maana ya kiwango, Watooro ni jamii ya watu wakarimu sana. Wanamfanya msafiri, mgeni au mtalii kujisikia yuko nyumbani. Ukarimu huo kwangu na kwa familia unazidi hasa pale wanapotambua kuwa mke wangu anatoka huko. Moja ya mila wanazoendeleza na ambayo ni kichocheo cha umoja, heshima na upendo ni jamii yote kutumia Empaako, majina kumi na mbili tu. Baadhi ya mila za mwafrika ziliachwa kwa sababu tu zilisemekana ni mila potofu mbele ya watawala wa kikoloni na walioleta na kueneza dini zenye asili ya kizungu. Mila, desturi na utamaduni wa Mwafrika ni vema ukatunzwa, ukaenziwa na kuendelezwa, iwe kwa njia ya simulizi, sanaa, maandiko na taratibu za kawaida za maisha.


Mataifa yaliyoendelea, hasa yale ya ulaya na marekani, wamekusanya mbegu na mimea ya asili kutoka sehemu mbali za dunia ikiwa ni pamoja na kutoka Afrika. Baadhi ya miti hiyo ina faida nyingi ikiwa ni pamoja na kuwa chanzo cha dawa na chakula. Wanafanya hivyo kwa kuwa aina nyingi ya bioanuwai inatoweka katika nchi zinazoendelea kutokana na matumizi ya rasilimali asilia yanayozidi uwezo wa rasilimali hizo kujihuisha. Ndipo unapokuja umuhimu wa kuanzisha na kutekeleza mikakati ya kutunza na kuendeleza maliasili iliyopo na kuhakikisha haipotei kabisa. Pale inapokuwa imetoweka, mikataba ya kimataifa inaweza kutumika kupata na kuotesha upya mimea hiyo. Uanzishwaji wa bustani za mimea ni utekelezaji wa mkakati huu wa utunzaji na uendelezaji wa bioanuwai asilia. Uanzishaji na uendelezaji wa Bustani ya Mimea Asili Tooro ni mfano wa kuigwa na miji, manispaa na majiji Tanzania, na Afrika ya Mashariki. Kuwa na mpango thabiti na kutenga eneo la kuanzisha bustani za mimea asilia iwe ni moja ya vigezo vya kupandisha hadhi ya mji.


Maeneo ya bonde la ufa la mashariki ya Afrika lina maziwa mengi ya volkano. Maziwa mengi zaidi yako magharibi ya Uganda. Maziwa haya huwa na kina kisichobadilika msimu hadi msimu. Maziwa hayana mito au vijito vinavyotoka au kuingia. Yamekuwa chanzo cha simulizi za kila aina zinazorithishwa kizazi hadi kizazi na wakaazi wa maeneo ya jirani. Sera za uwekezaji zimechochea uwekezaji katika maeneo ya kingo za maziwa ili kukuza utalii. Baadhi ya wawekezaji wamekuwa na mipango ya kuendeleza uvuvi. Kuna mgongano wa masilahi baina ya wakaazi wa maeneo hayo, ambao hupata maji na samaki kutoka katika maziwa hayo, na Halmashauri zinazohusika kutaka mapato kutokana na uwezekaji, na wawekezaji kujaribu kuwazuia wananchi kutumia maziwa hayo. Jambo la muhimu kabisa ni utunzaji wa mazingira ya maziwa hayo ya volkano. Uzoefu uliopatikana Tooro ikiwa ni pamoja na hukumu ya kesi kuhusu uwekezaji na matumizi ya maziwa hayo ni somo tosha kwa Halmashauri zetu hapa nchini.


Shukrani


Waraka huu ni matokeo ya mchango wa wenyeji wetu waliotupokea na kututunza na kutusindikiza katika safari zetu huko Uganda na Tooro. Walikuwa wasikivu na wavumilivu wa kujibu maswali mengi tuliyowauliza. Mheshimiwa Jaji Paul Mugamba Amooti, Jaji wa Mahakama ya Upeo (Supreme Court) ya Uganda, Mkewe Grace Mugamba Atwoki, Edward Mugamba Adyeri, na Mcgyver Mugamba Adyeri, wamekuwa wenye msaada mkubwa. Dan Rubombora Ateenyi na Fred Karamagi Abooki nao wametusaidia sana. Shemeji zangu Nesta Abwooki, Bessie Adyeri na Margareth Mbabazi Amooti wamekuwa wenyeji wetu waliotufanya tujisikie tuko nyumbani tukiwa mbali kutoka Lufilyo na Matema. Arthur Isoke (Abooki) na mkewe Alice Isoke Adyeri, wamekuwa wakarimu kupita kiasi kila tunapowatembelea nyumbani kwao Kanyambeho. Profesa Edward Rugumayo Amooti na mkewe Phoebe Rugumayo Amooti wametusaidia kuelewa chimbuko la Bustani ya Mimea, Tooro, na Chuo Kikuu MMU ambao ni mchango wao na wenzao katika kuendeleza Tooro baada ya kustaafu utumishi wa umma na kurudi Fort Portal. Ni mfano wa kuigwa. Prof. J.M. Kasenene, Makamu Mkuu wa Chuo, MMU; Dr. Edmond Kabagambe, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo, MMU; Mukundane Vincent, Mkurugenzi wa Rasilimali watu; Grace Nyakahuma, Msajili wa Taaluma; Kakukulu Yunusi, Msajili wa Fedha; Nkrumah Jimmy, Msajili, Utawala; na Agonzebwe Robinah, Msaidizi, Utawala; walinipa nafasi ya kuwa na kikao ambacho kilituwezesha kupata taarifa za kina kuhusu MMU na kuzungumza kuhusu uwezekano wa ushirikiano kati ya MUST na MMU. Ndugu Godfrey Ruyonga, Mkurugenzi Mtendaji wa Bustani ya Mimea Asili ya Tooro (Tooro Botanical Gardens) kwa taarifa aliyotupa kuhusu chanzo, kukua na maendeleo ya Bustani. Bi Prossy Bigabirwe, Mhifadhi, Hifadhi ya Semuliki alitupa maelezo yake fasaha kuhusu chemchemi za Sempaya na bioanuwai ya Hifadhi. Wote hao waliotajwa tunawashukuru.


Mwisho, lakini sio kwa umuhimu, ni kwa wakaazi wa Kagorogoro na Kasenyi, alikozaliwa Lucy Akiiki. Nilipata nafasi ya kushirikiana nao katika Ibada ya Shukrani ambayo ilifanyika katika Kanisa la Uganda, Kasenyi, Jumapili tarehe 4 Agosti 2013, ili kutuwezesha kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa ahueni kiafya na kwa sala na maombi yao wakati wote wa kipindi kigumu. Waliokuja kutoka Tanzania ambao waliungana na sisi katika Ibada ya shukrani ni: Mzee Agen Mwandosya; Meck Mwakipunga, Dada Christina Masika Mwandosya, Bupe Kamugisha, Mheshimiwa Balozi Dr Ladislaus Komba, aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Uganda na Mama Komba; Asa Mwaipopo; Brigitha Faustin; Ngusa Izengo; na Dr. Mpapalika. Nawashukuru sana. Nilipotoa maneno machache ya shukrani nilisema:


Waitu Omwahule na Bebembezi Abediini Abandi,

Na Bantu ba Ruhanga, inywena mubitinisa byanyu,

Batooro na Batoorokati.

Kubanza mwibara lyomukyara wange Lucy Marunga, neeka yange yoona, nitusiima Ruhanga habwomugisa gunu kuteranira hanu Kasenyi. Nkoku murukumanya ekanisa enu nkuru habwaitu habwokuba maazaara Adyeri yagigonzaga muno kandi akahereza hanyuma ekanisa, yayorora Marunga nuwe aije abe mukyara wange.

Emyaka ebiri enyuma etuberiire ngumu muno muka yaitu. Nyowe nkarwara najanjabwa mu Tanzania na India. Nkoku murukumanya kuba kurungi kwawe nikusigikira ha bintu bisatu: iwe nkomurwaire nabantu orukwikara nabo; abafumu, abakozi abandi mwirwarro, nemibazi; hanyuma ekirukukirayo byona embabazi za Mukama. Embabazi za Mukama niruga mukugonzakwe nesaara mwansabiire. Abantu ba Tooro nimbasiima muno ha bwengonzi zanyu enyingi.

Kumalirra, nsoboire kwemerra mumaiso ganyu kiro kinu habwe mbabazi za Mukama, kandi nengonzi nokurolererwa okurungi kwa Marunga. Kinu ninkigumya kusigikirra ebyomukitabu ekirukwera Enfumo Esuura Asatu nemu(31) Orukarra rwa Ikumi(10):

"Omukazi omwerinzi nooha asobora kumuzoora? Omuhendogwe nigukirra kimu ogwezaabu."

Hati kinu kya Marunga wenka Enfumo Esuura Asatu nemu(31) Orukarra rwa Abiri na mwenda(29): "Abaisiki baingi bakozire ebyokwerinda baitu iwe nobakira boona".

Mukama abalinde kuhikya obutuli tangatangana owaitu Tanzania. Mwebale muno kumpuliriza. Mukama Asiimwe Muno.




Mwebale Muno,

Asante Sana

Mark Mwandosya

Fort Portal, Uganda

Desemba 2017