UJUMBE WA NDUGU MARK MWANDOSYA, MWENYEKITI WA BODI YA EWURA, ALIOUTOA TAREHE 31 JULAI, 2026 WAKATI WA KIKAO CHAKE CHA MWISHO CHA BODI, KABLA YA KUMALIZA KIPINDI CHAKE CHA UENYEKITI
Ndugu Wajumbe wa Bodi ya EWURA;
Mkurugenzi Mkuu wa EWURA;
Menejimentì na Wafanyakazi wa EWURA;
Mabibi na Mabwana.
Bodi ya Wakurugenzi ya EWURA imeundwa kwa mujibu wa Kifungu cha 8 cha Sheria ya EWURA Sura ya 414 ya Sheria za Tanzania. Jedwali la Kwanza la Sheria hiyo ambalo linatokana na Kifungu cha 8(5) cha Sheria, katika Aya ya pili (2), linafafanua mihula ya Wajumbe wa Bodi. Kuhusu Uenyekiti, Aya hiyo inaeleza kwamba Mwenyekiti atahudumu kwa muhula wa miaka minne. Aidha, katika aya hiyo, inafafanuliwa zaidi kwamba Mwenyekiti, Wajumbe na Mkurugenzi Mkuu wanaweza kuteuliwa tena kwa muhula mwingine mmoja tu. Maana yake ni kwamba kuteuliwa tena kwa Mwenyekiti, na Wajumbe kwa muhula wa pili, kutatokana na utashi wa Mamlaka za Uteuzi.
2. Kwa kuwa niliteuliwa kuwa Mwenyekiti tarehe 15 Agosti 2022, hiki ni kikao changu cha mwisho, Kwani ifikapo tarehe 14 Agosti 2026 nitakuwa nimehitimisha miaka minne ya utumishi katika nafasi hii kama Mwenyekiti. Ninapowaaga leo baada ya kuitumikia Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), nimeona niwaage kwa njia ya kutoa mawaidha au maoni machache kuhusu kazi tulizozifanya pamoja, changamoto tulizozipitia, na mengine ambayo nayatoa kwa ushauri tu. Sina mpangilio wowote wa uwasilishaji, bali nayasema kama yanavyonijia kichwani.
Mniwie radhi iwapo nitachukua muda wenu adimu kunisikiliza. Kama Marko Antonio alivyowasihi Warumi waliokwenda kumsikiliza, nami nasema,"Ndugu zangu nawaombeni masikio yenu".
3. Nitaanza na suala la afya. Mwili wa binadamu hauwezi kueleweka kwa urahisi. Kwa nje mwili unaweza kuonekana uko sawa lakini kwa ndani huwezi kuuona kama una changamoto. Afya ya kila mmoja wetu hatimaye ndio afya ya familia yake, afya ya EWURA na afya ya Taifa kwa ujumla. Katika kuzingatia na kuona umuhimu wa afya za wafanyakazi wa EWURA, Bodi hii iliamua kuanzisha siku maalum ya Afya kwa Wafanyakazi wa EWURA yaani “EWURA Health Day”. Hii ni siku muhimu sana katika kalenda ya mwaka ya EWURA. Nami katika kusisitiza umuhimu huo, nilipata nafasi ya kuongea nanyi kuhusu magonjwa yasiyoambukiza, hususan, kuishi na Saratani, nikiwaeleza yaliyonisibu. Nawashauri wafanyakazi mpime afya zenu kila wakati, hata pale mnapojisikia vizuri.
4. Wafanyakazi wanaolipwa vizuri ndio wanaotoa huduma iliyotukuka. Kwa kuzingatia ukweli huu na ustawi wa EWURA, Bodi hii kwa vipindi viwili tofauti ilipitisha ongezeko la posho na marupurupu stahili kwa wafanyakazi. Lengo lake ilikuwa kutoa motisha, na kupunguza makali ya ongezeko la bei (inflation). Hakika njia hii inawasaidia wafanyakazi kuongeza kipato kwa muda mfupi na wa kati. Hata hivyo ni muhimu kuelewa kwamba kipato hiki hakihesabiwi katika kukokotoa mafao ya kustaafu ya mfanyakazi. Njia pekee inayotumika ni kuangalia namna bora ya kuboresha mishahara ili iwe na faida wakati wa kustaafu. Hivyo basi, nawaachia Menejimenti suala hili kama changamoto, na ikibidi Bodi na Menejimenti husikeni moja kwa moja katika mjadala unaohusu sera hii ya kuboresha mishahara ya wafanyakazi. Moja ya sababu za mafanikio ya nchi ya Singapore ni kuwa na utumishi wa umma bora na uliotukuka. Huko Singapore wafanyakazi wa Serikali na Taasisi za umma wanalipwa vizuri zaidi ya wale walio katika sekta binafsi.
5. Bodi hii tumetoa msukumo wafanyakazi kujiendeleza kielimu na kuongeza uelewa na ujuzi katika maeneo yao. Aidha, tuliamua kuwalipia wafanyakazi wanaosoma katika vyuo mbalimbali tofauti na awali ambapo wafanyakazi walikuwa wanajilipia na baadae kufidiwa na taasisi baada ya kumaliza masomo yao. Mdhibiti anatakiwa awe na uelewa na ujuzi mkubwa zaidi ya wale anaowadhibiti. Vinginevyo kuna hatari ya 'kutekwa'. Msukumo wa kuwataka wafanyakazi wajiendeleze kitaaluma uendelee, tena kwa nguvu zaidi.
6. Bodi hii iliamua pia kuanzisha Kanda ya Magharibi ya EWURA ili kupeleka huduma za kiudhibiti karibu na watoa huduma na watumiaji. Awali, Mkoa wa Kigoma ulikuwa Kanda ya Ziwa (Lake Zone), Tabora ilikuwa Kanda ya Kati (Central Zone) na Katavi ilikuwa ikuhudumiwa na Kanda ya Kusini Nyanda za Juu (Southern Highlands Zone) jambo ambalo lilisababisha huduma kuwa hafifu. Vilevile, Bodi hii imeamua zijengwe ofisi za Kanda ili kuendelea kutoa huduma bora zaidi, hasa baada kukua na kupanuka kwa shughuli za Mamlaka. Ujenzi huo unaanza na ofisi za Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na kufuatiwa na ule wa ofisi za Kanda ya Kaskazini (Nothern Zone). Kanda ya Kati ni muhimu ipewe kipaumbele katika ujenzi wa ofisi. Kwa sasa Kanda ya Kati wanahudumiwa na ofisi za Makao Makuu, ni "wapangaji wasiolipa kodi."
7. Tumeandaa mfumo wa uendeshaji na utawala wa EWURA (Organsational Structure) ambao sasa umepitishwa na Serikali. Changamoto katika utekelezaji zinaweza kujitokeza.
8. Tumesisitiza EWURA iwe mstari wa mbele katika uwiano wa jinsia, hususan kumwendeleza Mwanamke katika udhibiti, uongozi na katika uelewa wa sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati (STEM). Naamini tukifanikiwa basi tutakuwa tumeimarisha misingi ya maendeleo endelevu ya sekta tunazozidhibiti. Tuanzishe, pale ambapo bado, na tuendeleze na tuimarishe, pale tulipoanzisha, ushirikiano na vyuo vya elimu ya juu na vyuo vya ufundi, na taasisi nyingine zinazohusika na maeneo yetu ya kiudhibiti. Mkataba wa maelewano (MoU) kati ya EWURA na Chuo cha Maji ni mwanzo mzuri, sasa mfuatilie MoU na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na vyuo vingine kwa lengo la kuharakisha na kuimarisha ushirikiano. Kuhusu uwekaji wa MoU na UDSM, fuatilieni mazungumzo kati yetu, Bodi ya EWURA na uongozi wa UDSM ya tarehe 23 Julai 2026, nilipoongozana na ujumbe wa ZERA kutoka Zimbabwe tulipozuru UDSM.
9. Katika kusimamia sekta ya Maji na usafi wa mazingira, kwa muda mrefu mkazo mkubwa tumeweka katika sekta ya maji. Tujitahidi kuupa umuhumu usafi wa mazingira (sanitation). Ubora wa usafi wa mazingira ni utu na ni kipimo cha maendeleo.
10. Tutoe msukumo zaidi na kuhimiza kupunguza upotevu wa maji. Ukaguzi maalum wa pamoja wa upotevu wa maji katika eneo la DAWASA umetusaidia sana kuelewa changamoto hii na namna ya kuikabili. Tuendelee na kazi hii katika miji mingine.
11. Kuhusu upangaji wa bei za maji, tumetumia msemo, "pamoja na uhuru wa mdhibiti na udhibiti, mdhibiti lazima awe na uelewa wa hali ya siasa nchini." Uelewa huo umefanya kazi yetu ieleweke kwa urahisi.
12. Tuhusike katika hatua mbali mbali za utekelezaji wa Gridi ya Taifa ya Maji (National Water Grid). Katika jambo hili tuzingatie kwamba wajibu wetu ni wa kiudhibiti. Wizara ya Maji inahusika zaidi. Pamoja na gridi ya kitaifa ya maji, upatikanaji wa maji katika Mji Mkuu wa Dodoma ni changamoto kubwa. Hivyoi basi, EWURA inabidi iendelee kuishauri Serikali katika kutatua changamoto hiyo.
13. Leo, katika yale tutakayojadili ni kazi iliyofanywa na Idara ya Maji kuhusu mpango wa kuanzisha mfumo wa kidigitali wa kuziwezesha Mamlaka za Maji Mijini kupata taarifa zake muhimu za kufanyia kazi (Real Time Data Collection for Performance and Monitoring of Water Supply and Sanitation Authorities). Hii ni hatua muhimu ya kutumia teknolojia mpya kuboresha ukusanyaji na usambazaji wa data na takwimu. Mfumo huu utaiwezesha EWURA kufanya kazi yake kiufanisi. Kitengo cha TEHAMA na Kamati ya Tehama na Ubunifu Kidigitali, wanaweza kuwa na mchango katika mpango huu.
14. Katika sekta ya gesi asilia, ni dhahiri kumekuwa na ongezeko la vituo vya gesi asilia
(CNG) katika kipindi hiki cha miaka minne. Kazi ya kuongeza vituo vya CNG iendelee na
kasi iongezeke. Matumizi ya gesi asilia yaongezeke zaidi.
15. Nakumbuka tulipitisha Kanuni za Mini-LNG. Wawekezaji walikuwa wanasubiri Kanuni hizi. Utekelezaji wake unasubiriwa kwa hamu kubwa. Tumehusika pia na kupitisha Kanuni za kupanga bei ya gesi asilia.
16. Mradi wa kuboresha kidigitali taarifa za hifadhi, usafirishaji, na matumizi ya petroli kwenye vituo (enhanced NPGIS) ni muhimu kiudhibiti. Tuangalie jinsi gani tunaweza kwenda kwa kasi zaidi. Fuatilieni uwezekano wa wenye vituo kufidiwa gharama za kununua Mfumo wa Kielektroniki wa Upimaji wa Kiwango cha Mafuta kwenye Matanki (ATG) ili tuongeze kasi ya kufunga ATGs nchi nzima. Mtakapopitia upya mfumo wa gharama na bei za mafuta ya petroli angailieni uwezekano wa kutekeleza mradi huu kwa njia muafaka, kumwezesha mwenye kituo bila kumbebesha mtumiaji mzigo mkubwa.
17. Tumepitisha Kanuni za ujenzi wa vituo vya petroli vijijini, ikiwa ni pamoja na matumizi ya teknolojia rahisi ya makontena. Tuongeze elimu, matangazo na ushawishi kwa kushirikiana na Wakala wa Nishati Vijijini (Rural Energy Agency - REA). Bado wananchi wa vijijini wako mbali na vituo, na matumizi ya vifaa vya plastiki kusafirisha na kutunza mafuta, yanaendelea.
18. Tumesimamia ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima (Uganda) mpaka Chongoleani, Tanga (East African Crude Oil Pipeline - EACOP) katika masuala ya kiudhibiti, na majukumu yaliyo katika Mkataba baina ya Mwekezaji na Nchi Mwenyeji (Host Government Agreement). Jukumu letu kubwa limekuwa ni kuhakikisha kwa kadri inavyowezekana, kazi za ujenzi wa EACOP zifanywe na Watanzania, na kampuni au taasisi za kitanzania (local content). Huu ni wakati mzuri wa kutathmini tumefanikiwa vipi kujenga uwezo wa Watanzania. Kongamano maalum tulilopanga kuhusu jambo hili inabidi lifanyike. Wenzetu Uganda walijipanga na wamejipanga vizuri. Tumejenga bomba la Tanzania Zambia Mafuta (TAZAMA), Tumejenga bomba la gesi kutoka Madimba hadi Kinyerezi. Sasa tunakaribia kuhitimisha ujenzi wa EACOP. Suala muhimu na la msingi ni, Je tumejenga uwezo wa sisi wenyewe kutekeleza ujenzi bomba la aina hiyo miaka ijayo?
19. Pamoja na kuyumba kwa soko la mafuta duniani baada ya mashambulizi ya Marekani na Israeli dhidi ya Iran, kwa kuishirikisha na Serikali na kuwahusisha wadau wengine muhimu, tumeweza kupanga bei za mafuta ambazo zimekuwa himilivu na zimeleta utulivu. Tuendelee na juhudi hizi.
20. Mgogoro wa mashariki ya kati umetoa msukumo wa kuanzisha hifadhi ya mafuta kitaifa (strategic oil reserve). EWURA inawajibu muhimu katika hili na ihusike ipasavyo. Nakumbuka tumezungumza kuhusu hifadhi hii tangu nikiwa Kamishna wa Petroli na Nishati miaka ya 80, Katibu Mkuu wa Maji, Nishati na Madini miaka ya 90, na Waziri wa Wizara mbalimbali miaka 2000. Haikuwezekana. Huu ni wakati wake.
21. Tumepitisha mwongozo wa matumizi ya mafuta yanayotokana na upatikanaji wa gesi asilia na ule wa matumizi ya mafuta yaliyotumika. Miongozo imeanza kutumika.
22. Katika kipindi hiki cha miaka minne Menejimenti imeandaa, na Bodi imepitisha Sera (policies) 11, Miongozo (guidelines) 15, na nyaraka za utendaji (manuals and others) 19.
23. Tumepitia upya Mwongozo wa Bodi (Board Charter) na kuanzisha Kamati ya Tehama na Ubunifu Kidigitali. Matokeo ya kazi yake yameanza kuonekana. Tuendelee kumshawishi na kumshirikisha Msajili wa Hazina (TR) aone umuhimu wa jambo hili. Tupimwe kwa matokeo. Hatimaye jukumu la kuanzisha Kamati za Bodi kiutaratibu ni la Bodi.
24. Nilipoanza uenyekiti wa Bodi Agosti 2022, vikao vya Bodi vilikuwa vinaanza saa 3 asubuhi na vinaisha saa tatu au saa nne za usiku. Hii haileti tija hata kidogo. Tumetumia Mwongozo wa Bodi na ule wa TR ili tuwe na vikao vyenye tija.
25. Nimefanya kazi kwa karibu sana na Katibu wa Bodi na wale waliomtangulia. Mwenyekiti na Katibu ndio wanaoandaa na kufanikisha mikutano ya Bodi.Hata hivyo, kabla Katibu hajawasiliana na Mwenyekiti kupanga vikao vya Bodi, inabidi amhusishe Mkurugenzi Mkuu.
26. Uandishi wa kumbukumbu za vikao vya Bodi unaendelea kuwa bora mwaka hadi mwaka. Lakini bado nyaraka za bodi ziendelee kuboreshwa. Nyaraka za Bodi huchelewa sana. Katibu wa Bodi na Menejimenti fanyeni bidii zaidi ili nyaraka zifike siku saba kabla, au angalau siku tano kabla.
27. Kamati zetu zote za Bodi ni muhimu. Pamoja na hilo, Kamati inayosimamia ukaguzi, ambayo kwa EWURA ni Kamati ya Bodi ya Ukaguzi na Viashiria Hatarishi (Board’s Audit and Risk Committee) ndiyo pekee iliyoanzishwa kisheria. Ni Kamati hii tu ambayo Mkurugenzi Mkuu hawezi kuwa Mjumbe wa Kamati. Kamati inasaidiwa na Mkaguzi wa Ndani. Kiutaratibu Kamati na Mkaguzi wa ndani wanatakiwa kuwa 'huru'. Katika taasisi na kampuni nyingi, Kamati za Bodi za Udhibiti, na Wakaguzi wa Ndani, mara nyingi hukosa ushirikiano wa Menejimenti.
28. Kupitia Kamati hiyo tumeweka utaratibu wa kuhakikisha maagizo ya Bodi, maagizo na maelekezo ya CAG, na maagizo ya Kamati husika za Bunge, yanatekelezwa na Bodi inataarifiwa.
29. Utekelezaji wa mradi wa kunganisha kidigitali mfumo wa EWURA na ule wa Tanesco ili tupate taarifa za wakati ule ule wa uzalishaji na matumizi ya umeme karibu utakamilika (Real-time Database Management system (RDBMS)). Mradi huu unafadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB). Mradi huu, mradi wa kuboresha usimamizi wa petroli na gesi kidigitali (Enhanced NPGIS), na mpango wa kuweka kidigitali taarifa/takwimu/data za Mamlaka za Maji (WSSAs) ikifanikiwa itaifanya EWURA iwe ya kidigitali. Katika hili, Idara zote ziendelee kufanya kazi na kitengo cha TEHAMA chini ya Kamati ya TEHAMA na Ubunifu Kidigitali ili kufanikisha kuwa na 'DIGITAL EWURA'.
30. Tumeanzisha mpango wa kuhamasisha matumizi ya magari yanayotumua betri (EV). Tayari tumeandaa taratibu za awali. Kazi hii iendelee kwa kushirikisha Wizara na Nishati, Wizara ya Uchukuzi, LATRA, na TANESCO pamoja na wadau wengine. Ikumbukwe kwamba teknolojia hii ni muhimu katika kupunguza matumizi ya petroli na kupunguza gesi ukaa. Matumizi ya EV, pamoja na mipango mingine, ndiyo inaiwezesha China kuhimili mgogoro wa Mashariki ya Kati.
31. Kasi ya ongezeko la matumizi ya umeme ni kubwa. Umeme wa bwawa la Mwalimu Nyerere huenda usitosheleze mahitaji ifikapo 2030. Tuendelee kuishauri Serikali kuhusu utekelezaji wa mpango kabambe wa umeme ili tusirudi kwenye mgao wa umeme na athari zake kubwa kiuchumi, kijamii na kisiasa pia.
32. Bei halisi ya umeme inatokana na kujua gharama za uzalishaji, usafirishaji na usambazaji (Cost of service - CoS). Mtaalamu wa 'Cost of Service Study' apatikane na asimamiwe vilivyo.
33. Tumehusika na tuendelee kuhusika katika Mpango wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.
34. Kawaida safari za nje ni zile zinazohusu taasisi za kikanda na kimataifa ambazo sisi ni wanachama. Nyingine ni za kitaifa. Nyingine pia zinahusu mafunzo maalum. Zile za 'benchmarking' tuwe tunazipanga kimkakati na hasa tujue kile tunachokitafuta. Kuhusu hili, tumeweka utaratibu wa kuhakikisha tunakuwa na hadidu za rejea za safari hizo.
35. Pamoja na kuendelea kupata hati safi, hoja za CAG zimekuwa zikiongezeka mwaka hadi mwaka. Huwa tunazijibu hoja hizo baadaye, lakini hii si dalili nzuri. Mkurugenzi Mkuu ahakikishe viongozi wa Idara na Vitengo wao wenyewe wanahusika vilivyo CAG anapofanya ukaguzi.
36. Kwa muda mrefu, kikanda tulitambulika sana kiudhibiti. Pamoja na taasisi za nje kuendelea kuja EWURA kujifunza, sasa tumeanza kushuka kidogo umaarufu kwa vigezo vya kimataifa. Tujiangalie upya. Tujisahihishe na tujenge utamaduni wa kujitathmini (self- assessment).
37. Tumeanzisha Maktaba ya EWURA. Mwanzo tulipata shida kidogo kuianzisha. Binadamu hufanya kazi kwa mazoea. Ilibidi tuanze na Sera ya Maktaba. Kamati iliyoundwa kusimamia uanzishaji wa maktaba ilifanya kazi nzuri. Tulipoipeleka Bodi ya ZERA kwenye Maktaba ya EWURA walifurahia walichokiona na kupata maelezo mazuri ya Mkutubi (Librarian). Wameamua kuleta watu wao kuja kujifunza zaidi (benchmarking). Endelezeni kitovu hiki cha elimu, habari na uelewa ili kiwe mfano Kitaifa na katika Kanda.
38. Pamoja na wajibu wetu wa kuhakikisha mtoa huduma zinazodhibitiwa mwenye ufanisi anawezeshwa, mtumiaji au mlaji ambaye hana nguvu katika mizania ya udhibiti, alindwe na asaidiwe.
39. Nakumbuka tuliwahi kuamua tuwe na sala ya EWURA, ituongoze ili tupate baraka za Mwenyezi Mungu katika kazi zetu. Rasimu tulipata. Ilikuwa ndefu. Tukaagiza ipunguzwe. Hatukupata mrejesho na ikawa ndio mwisho. Tukamilishe zoezi hilo.
40. Katika kazi zenu zingatieni sheria, kanuni, taratibu, na miongozo mbali mbali. Mkifanya hivyo hamtapungukiwa.
41. Kaulimbiu ya EWURA ni: MATOKEO CHANYA (IMPACT). Vipengele au vijenzi vyake ni: Kutopendelea au Kutokubagua (Impartiality); Maadili (Morality); Weledi au Kuzingatia Taaluma (Professionalism); Kuwajibika (Accountability); Uendelevu wa maamuzi na Kutoyumba (Consistency); na Uwazi (Transparency). Vipengele hivi vya kaulimbiu ndivyo vinavyomtambulisha mfanyakazi wa EWURA. Haya yote yaendelee kuwaongoza na kujenga utamaduni ambao inakuwa fahari kujitambulisha, ‘MIMI NI MWANA EWURA’.
42. Nimehudhuria vikao vyote 48 vya kawaida na vyote 70 vya dharura. Namshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa kuniwezesha kuwaongoza kwa muda huu wa miaka minne.
43. Naishukuru Mamlaka ya uteuzi kwa imani na heshima kubwa niliyopewa. Wizara zote mbili, Wizara ya Nishati na Wizara ya bMaji, wametuongoza kisera na tumefanya kazi kwa ushirikiano na ukaribu.
44. Ndugu Wajumbe wenzangu wa Bodi, Menejimenti na Wafanyakazi wote, nawashukuru kwa ushirikiano mkubwa mlionipa.
Kazi iendelee na matokeo yawe chanya.
Assalamualaikum Warahmatullahi Wabarakatu
Asanteni kunisikiliza.